TEA YAKABIDHI MIRADI ILIYOKAMILIKA WILAYANI MTAMA NA MASASI.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Dkt. Leonard Akwilapo, amekabidhi vyeti kwa shule tatu zilizonufaika na miradi ya Mfuko wa Elimu wa Taifa baada ya kukamilika kwa ujenzi wake katika Halmashauri za Wilaya ya Mtama na Masasi.

Dkt. Akwilapo alikabidhi vyeti hivyo wakati wa ziara yake ya kikazi kwenye halmashauri hizo, ambapo alikagua maendeleo ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na TEA kwa ufadhili wa Mfuko wa Elimu wa Taifa.

Akizungumza na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Masasi, Bw. James Chitumbe, Dkt. Akwilapo alisema ameridhishwa na ubora wa miradi iliyokamilika na kukabidhi vyeti hivyo kama ishara ya kuwakabidhi rasmi miradi hiyo kwa ajili ya matumizi na usimamizi.

“Katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, nitakabidhi cheti kwa ajili ya mradi wa nyumba nne za walimu katika Shule ya Sekondari Lupaso, ambayo pia ina mradi mwingine wa jengo la utawala ambalo kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 80,” alisema Dkt. Akwilapo.

Aidha, aliongeza kuwa katika Wilaya ya Mtama, amekabidhi vyeti kwa miradi ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika Shule ya Msingi Songambele na bweni moja la wanafunzi lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 katika Shule ya Sekondari Mnara, ambalo limekamilika kwa asilimia 100.

Kwa niaba ya wanufaika wa miradi hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Bw. James Chitumbe, aliishukuru TEA kwa kufadhili miradi hiyo, akisema imechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira ya elimu katika shule husika.

Mbali na kukabidhi miradi hiyo iliyokamilika, Dkt. Akwilapo pia alitembelea miradi mingine inayoendelea kutekelezwa, ikiwemo ujenzi wa maabara ya sayansi na nyumba za walimu katika Shule ya Sekondari Ngongo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Lindi.

Mwenyekiti wa Bodi ya TEA, Dkt. Leonard Akwilapo (wa pili kulia), akiwasili katika Shule ya Sekondari Lupaso kwa ajili ya ukaguzi wa miradi ya elimu
Mwenyekiti wa Bodi ya TEA Dkt. Leonard Akwilapo akikagua ujenzi wa jengo la utawala katika Shule ya Sekondari Lupaso, ambapo ujenzi huo umefikia asilimia 80.
Mwenyekiti wa Bodi ya TEA Dkt. Leonard Akwilapo akijadiliana jambo na Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Bw. Lusekelo Mkubwa, kabla ya kukabidhi vyeti kwa miradi iliyokamilika.
Muonekano wa jengo la utawala linalojengwa katika Shule ya Sekondari Lupaso, Wilayani Masasi, kwa ufadhili wa Mfuko wa Elimu wa Taifa.

Dkt. Leonard Akwilapo akikabidhi cheti kwa Mwl. Andrea Magani, aliyepokea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtama na Masasi. Kulia ni Mwl. Hussein Chilwa kutoka Shule ya Sekondari Chiwata, na kushoto ni Mwl. Zawadi Mdimbe kutoka Shule ya Sekondari Chidya.

Mwenyekiti wa Bodi ya TEA Dkt. Leonard Akwilapo akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukagua utekelezaji wa miradi ya elimu na kukabidhi vyeti kwa miradi iliyokamilika Wilayani Masasi na Mtama.

Related Posts