Wafanyabishara waadhimisha sherehe za CCM wakichangamkia fursa Dodoma

Dodoma. Wajasiriamali wa Jiji la Dodoma leo Jumatano Februari 5, 2025 ikiwa ni maadhimisho ya miaka 48 ya Chama cha Mapinduzi (CCM) tangu kuzaliwa kwake, wamepata fursa ya kufanya biashara za kuuza kofia, mifuko na wengine kuuza begi za kuvaa zenye majina ya Samia Suluhu Hassan, Dk Hussein Mwinyi na Dk Emmanuel Nchimbi.

Kila gari iliyosimama ilikuwa ikikimbiliwa kwa ajili ya kuwapata wateja wao kabla ya kuingia uwanja na wengi walionekana kununua bidhaa hizo.

Ndani ya uwanja wauzaji wa uji na chai mapema asubuhi walifanya biashara ingawa katika jukwaa maalumu ambalo walikaa watu waliokuwa na kadi maalumu kulikuwa na chai, uji na kahawa maalumu kwa ajili ya wajumbe.

Biashara nyingine nje ya uwanja ambayo ilionekana kupata wadau wengi ni wauza miamvuli kutokana na mvua nyepesi iliyokuwa ikinyesha.

Hata hivyo, hakukuwa na ruhusa ya wafanyabiashara kuvuka kamba iliyokuwa imefungwa na polisi kwa ajili ya usalama.

Wapigapicha waliendelea kunufaika na wateja wao ambao walipenda kusimama mbele ya mabango yenye picha za Rais Samia Suluhu Hassan na Dk Emmanuel Nchimbi.

Tofauti na wakati mwingine, polisi leo walionekana kuwa watulivu katika maeneo mengi bila kuwabughudhi watu isipokuwa wale wanaotaka kuvuka kamba ya kizuizi.

Ndani ya uwanja kuna minong’ono kuwa huenda baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wakatambulishwa kwenye mkutano huu na kujiunga na CCM.

Related Posts