Wafanyakazi wa ndege kunolewa kutambua itifaki kuhudumia viongozi

Dar es Salaam. Shirika la Ndege la Precision limeanzisha utaratibu wa kutoa mafunzo ikiwamo ya itifaki kwa wafanyakazi wake ili kujipambanua zaidi liilenga kuwa miongoni mwa mashirika bora ya usafiri wa anga duniani.

Mkakati huo umeelezwa na Mkurugenzi, Mkuu wa Shirika hilo, Patrick Mwanri leo Jumatano, Februari 5, 2025 wakati akisaini mkataba wa makubaliano na Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania (IoDT).

Makubaliano hayo yanalenga kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa shirika hilo kwa ajili ya kuboresha zaidi huduma sambamba na kuwajengea uwezo watumishi wake juu ya namna bora zaidi ya kuwahudumia viongozi wanaotumia usafiri huo.

Amesema Tanzania imekuwa ikipokea wageni mbalimbali ikiwamo viongozi ambao kuna itifaki za kuwahudumia.

“Wapo wahudumu ambao hawafahamu protocol (Itifaki) za kuwahudumia viongozi, unapowajengea uwezo kuna kitu unamuongea na kukiongeza kwenye Kampuni, ndicho ambacho sisi tunakifanya,” amesema.

Amesema makubaliano hayo yanalenga kuboresha ufanisi wa huduma katika shirika hilo  kuanzia kwenye uongozi wa juu hadi wafanyakazi wa ngazi zote.

“Makubaliano haya yatasaidia kuboresha ufanisi wa kazi na ubora wa huduma zetu kwa ujumla, lengo ni kuwa moja ya mashirika makubwa ya ndege duniani,” amesema Mwanri.

Mkurugenzi wa IoDTa, Said Baraka Kambi, amesema kuwa ushirikiano huu unalenga kuinua maono mbalimbali ya Shirika hilo.

Amesema, wafanyakazi wa Precision Air mbali na kupata ujuzi wa masuala ya itifaki, watafundishwa utawala bora na masuala mbalimbali ikiwamo ya mitazamo.

“Ni muhimu kufahamu protocol, hii itawasaidia wafanyakazi kuhudumia kwa ufanisi zaidi,” amesema.

Related Posts