Mwanza. Wanafunzi wawili wa Shule ya Blessing Modern iliyopo Nyasaka wilayani Ilemela jijini Mwanza wametekwa na kupelekwa kusikojulikana na mtu ambaye hajafahamika mara moja wakiwa kwenye basi la shule wakienda shuleni.
Wanafunzi hao ni Magreth Juma (8) mwanafunzi wa darasa la pili mkazi wa Hesawa Capri Point na Fortunata Mwakalebela (5) mkazi wa Bugando jijini humo.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbdroad Mutafungwa amesema tukio hilo la utekaji limetokea leo Jumatano Februari 5, 2025 saa 12 asubuhi eneo la Nasa Drive Capri Point jijini Mwanza wakati wakiwa kwenye basi la shule Toyota Hiace.
Akitoa taarifa ya tukio hilo mbele ya waandishi wa habari, Mutafungwa amesema mtekaji huyo licha ya kutofahamika, alipewa lifti kwenye basi hilo la shule lililokuwa na wanafunzi sita (mmoja wa chekechekea na watano wa msingi) na matroni, kisha kufanya tukio hilo.
“Watoto hao sita tayari walikuwa wameshakabidhiwa na wazazi wao kwa dereva wa gari hilo pamoja na matroni na walikuwa tayari kupelekwa shule. Dereva aliamua kwa sababu yake mwenyewe alimsaidia usafiri mtu wa jinsia ya kiume ambaye aliketi siti ya nyuma ya dereva na safari ya kuelekea shuleni ilianza,” amesema Mutafungwa.
Amesema:”Umbali kidogo tu abiria huyo ghafla alibadilika na kumkaba dereva shingo na katika vurugu hizo abiria huyo alifanikiwa kufungua mlango na kubeba watoto wawili na kuondoka nao kwa kutumia pikipiki mbili ambazo zilitokea.”
Amesema namba za usajili za pikipiki hizo na madereva wake walioshiriki kwenye utekaji huo hazijafahamika, lakini wanafunzi wanne waliobaki hawakupata madhara yoyote na tayari wameshakabidhiwa kwa wazazi wao.
Mutafungwa amesema dereva wa basi la shule, Richard Mtui (34) na matroni (msimamizi wa watoto), Rebeka Kijazi (23) wanashikiliwa kwa mahojiano kuhusu tukio hilo, huku uchunguzi zaidi ukiendelea ili kuwakamata wahalifu wote waliohusika.
“Chanzo cha tukio hili ni tamaa ya fedha kwa sababu katika ufuatiliaji wetu uongozi wa shule umeanza kupokea ujumbe mfupi kutoka kwa mtu ambaye anataka fedha ili awaachie watoto hao. Ufuatiliaji mkubwa wa makachelo wa polisi unaendelea tangu asubuhi,” amesema Mutafungwa.
Ameongeza:”Tunaomba wananchi watupatie ushirikiano utakaosaidia kupatikana watoto hawa wakiwa salama ili watuhumiwa wachukuliwe hatua stahiki. Mpango kazi umewekwa utekelezaji unaendelea ili kuhakikisha watuhumiwa hawa wanatiwa mbaroni.”
Kamanda huyo amewataka wamiliki wa shule kuhakikisha magari ya shule hayatumiki kubeba abiria ambao ni tofauti na watoto ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi pamoja na kuajiri madereva na wasimamizi makini wa watoto.