KOCHA wa Azam FC, Rachid Taoussi amevutiwa na viwango vya wachezaji wake wapya, Landry Zouzou na Zidane Sereri waliosajiliwa dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15, 2025.
Taoussi ameonyesha kuridhishwa na uwezo wa wachezaji hao kutokana na kufanya vizuri mazoezini huku shauku yake kubwa ni kuwaona watakachokifanya kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA).
Kesho Alhamisi, Azam inatarajiwa kushuka Uwanja wa Azam Complex kucheza dhidi ya KMC huku Taoussi akitarajia nyota hao wapya watakuwa na mchango mkubwa kwenye mchezo huo.
“Tuna furaha nao, wamekuwa wakisaidiwa na wenzao kuhakikisha wanajisikia vizuri, ni wachezaji wazuri na tuna imani wataongeza kitu kwenye timu,” alisema kocha huyo.
Zouzou aliyesajiliwa kutoka AFAD Djékanou ya Ivory Coast, anatarajiwa kuongeza ushindani kwenye eneo la beki wa kati wanapocheza Yeison Fuentes na Yoro Diaby.
Kwa upande mwingine, Sereri aliyesajiliwa kutoka Dodoma Jiji, atakuwa na jukumu la kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji ya Azam FC akisaidiana na nyota wengine kama Gibril Sillah na Nassor Saadun.
Kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, Azam inakamata nafasi ya tatu ikiwa na pointi 36 baada ya michezo 16.