Dar es Salaam. Kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu amefanya uteuzi wa kamati ya kuandika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025 ya chama hicho itakayokwenda kuuzwa kwa wananchi.
ACT Wazalendo kimekuwa chama cha kwanza nchini kuanzisha michakato ya uchaguzi mapema na tayari kimefungua dirisha kwa wanachama wake wenye nia ya kuwania kiti cha urais, kufanya hivyo na walianza Januari, 2025.
Leo Alhamisi Februari, 2025, chama hicho kimeunda timu ya kuandaa ilani ya uchaguzi itakayonadiwa na wagombea wake kwa wananchi wakati wa kampeni zitakapoanza.
Katika uteuzi huo, Dorothy amemteua Emmanuel Mvula kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo huku, Idrisa Kweweta akitajwa kuwa katibu wa kamati.
Sambamba na hao, Dorothy amewateua wajumbe 12 sambamba na sekretarieti ya watu wanne ambao ni Mshenga Juma, Jasper Sabuni, Jackline Ndonde na Said Mahalifa.
Kwa upande wa wajumbe, Dorothy amewateua Dk Elizabeth Sanga, Profesa Omar Fakih, Mary Mongi, Mtutura Abdallah Mtutura, Pavu Abdallah, Edgar Mkosamali, Abdul Nondo, Yasinta Awiti na Seif Suleiman Hamad. Wengine ni Shangwe Ayo, Humphrey Mrema, Maharagande Mbarala
Mpaka sasa, makada wa chama hicho waliojitokeza kuwania nafasi za uongozi ni pamoja na Othman Masoud Othman ambaye ametangaza nia ya kugombea urais wa Zanzibar wakati Dorothy naye akiwa ametangaza nia ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.