Meneja habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amemtaka winga Ladack Chasambi asivurugwe na bao alilojifunga kwenye mchezo dhidi ya Fountain Gate, leo Februari 6, 2025.
Winga huyo alijifunga bao hilo baada ya mpira mrefu aliourudisha kushindwa kuokolewa na kipa Moussa Camara na kufanya matokeo ya mchezo huo kuwa bao 1-1.
Ahmed Ally amesema kuwa Chasambi anapaswa kukomazwa kiakili na kosa hilo.
“Rasmi leo ndio umekua mtu mzima wa kimpira, ingekua kimaumbile tungesema umebaleghe hii leo. Matusi, kejeli, na dhihaka zote utakazopokea leo ni ukaribisho kwenye ukubwa wako, yasikutishe tamaa na wala yasikuvunje moyo, KARIBU UKUBWANI.
“Umeumiza mioyoo ya Wana Simba, lakini wewe sio wa kwanza kwenye mpira, wapo wenzio makosa yao yaliwanyima Kombe la Dunia
Kosa hili linakuongezea ukomavu,” aliandika Ahmed Ally katika ukurasa wake wa Instagram.
Ahmed pia amewataka mashabiki wa Simba kumsamehe na kumsapoti Chasambi.
“Ndugu zangu Wana Simba najua tunahisira na kijana
wetu lakini kila mtu kazini kwake anakosea.
“Na tukumbuke kabla ya kujifunga alishaisaidia timu kupata goli hivyo sukari na chumvi vimechanganyikana hii leo na bahati mbaya chumvi imezidi.
“Tukasirike lakini tusimchukie, na kama haitoshi tumsamehe na tuanze kumtia moyo. Kipindi hiki anatuhitaji zaidi sisi familia yake kumtetea na kumpigania ili arejee kwenye utulivu wake wa kiakili na aendelee kuipigania Simba yetu. Tunapatia pamoja, tunakosea pamoja, tunajisahihisha pamoja tunasonga mbele,” aliandika Ahmed Ally.