TETESI ambazo tunazo hapa mtaani ni mchezaji bora wa mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Vijana chini ya umri wa miaka 20 (Afcon U20) kupitia Kanda ya Cecafa, Sabri Kondo anamilikiwa na Singida Black Stars.
Hivyo pale Coastal Union ambako ametambulishwa yuko kwa mkopo tu ambao utamalizika mwishoni mwa msimu huu kisha kijana atarudi zake Singida kuwatumikia chui wa mkoa huo.
Kwa namna dogo alivowasha moto kwenye yale mashindano ilikuwa wazi asingeweza kubakia KVZ, timu ambayo alikuwa anaitumikia na bara palikuwa panamngojea.
Sabri amecheza kama Pele na inahitaji utafakari kwa umakini ili uweze kumuelewa kwa uamuzi wake wa kusaini mkataba Singida BS kisha kukubali kupelekwa kwa mkopo Coastal.
Kwanza Singida BS ni timu ambayo inamwaga fedha kwa sasa na kwa baadhi ya wachezaji inazizidi hata hizo timu kubwa ambazo katika hali ya kawaida zisingekuwa tayari kumpa hela ndefu Sabri Kondo naye anahitaji fedha ndiyo maana amesaini huko.
Pili kuamua kwenda Coastal kwa mkopo kumtamsaidia sana kijana katika maendeleo yake kwa vile kule Tanga hatokuwa na presha kubwa tofauti na iwapo angeamua kucheza katika timu kubwa.
Coastal ni timu ambayo imekuwa ikitoa fursa ya kucheza kwa vijana wenye umri mdogo pasipo kuwabebesha mahitaji makubwa jambo ambalo limekuwa likisaidia kwa kiasi kikubwa maendeleo yao.
Pale anakutana na kocha mzoefu na mkubwa nchini, Juma Mwambusi ambaye ana historia nzuri ya malezi kwa vijana wadogo hivyo kama Sabri Kondo atatuliza akili na kufuata kile anachoelekezwa na benchi la ufundi la Coastal, atakuwa moto wa kuotea mbali.
Mwishowe kijiweni hapa tunamtakia kila la kheri kijana wa Mabibo tukiamini miaka michache ijayo nchi itamuimba.