Dar es Salaam. Mkazi wa Jiji la Dar es Salaam, Nargis Omar(70) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka mawili ya kughushi wasio wa mama yake.
Nargis anadaiwa kughushi wosia wa marehemu mama yake mzazi kisha kujipatia nyumba kinyume cha sheria.
Mshtakiwa huyo amefikishwa mahakamani hapo leo, Alhamisi Februari 6, 2025 na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Neema Moshi.
Neema amesomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franko Kiswaga.
Mshtakiwa huyo amesomewa mashtaka yake na kuunganishwa na mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Mohamed Omar (64) ambaye alishasomewa mashtaka hayo Novemba 4, 2024.
Siku ambayo Mohamed alisomewa mashtaka yake mahakamani hayo, dada yake huyo hakuletwa kutokana kuruka dhamana ya polisi, hivyo upande wa mashtaka uliwasilisha ombi mahakamani hapo kuomba itoe hati ya kumuita Nargis asomewe mashtaka yake.
Nargis ni dada yake Mohamed na kwamba washtakiwa hao wanatetewa na Wakili Steven Mosha.
Akimsomea mashtaka yake, wakili Neema amedai katika shtaka la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kughushi wosia, tukio wanalodai kulitenda kati ya Julai 29, 1997 na Oktoba 28, 1998 katika Jiji la Dar es Salaam.
Wakili Neema amedai kuwa, washtakiwa wanadaiwa katika kipindi hicho, kwa lengo la kudanganya walighushi wosia ulioandikwa na marehemu Rukia Ahmed Omar, maarufu kama Rukia Sheikh Ali, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Shtaka la pili ni kuwasilisha nyaraka ya uongo mahakamani, tukio wanalodaiwa kulitenda tarehe hizo katika Jiji la Dar es Salaam.
Inadaiwa siku hiyo ya tukio, Omar na dada yake huku wakijua wanadanganya, waliwasilisha wosia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakionesha kuwa marehemu mama yao, Rukia Ahmed Omar alitoa nyumba moja kwa Nargis iliyopo kiwanja namba 35, eneo la Kariakoo na pia alitoa nyumba kwa Mohamed iliyopo Kiwanja namba 60 kitalu M, eneo la Magomeni, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Nargis baada ya kusomewa mashtaka yake amekana na upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi bado unaendelea.
Wakili Neema amedai kuwa, mashtaka yanayomkabili mshtakiwa yanadhaminika ila Mahakama itoe masharti magumu yatakayomfanya mshtakiwa afike mahakamani na pia awasilishe hati ya kusafiria.
Kufuatia ombi hilo hakimu Kiswaga alitoa masharti matatu ya dhamana dhidi ya Nargis.
Amesema mshtakiwa huyo anatakiwa awe na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh5 milioni kila mmoja.
Pia, wadhamini hao wanatakiwa kuwa na barua za utambulisho, kama ni wafanyakazi wanatakiwa wawe na barua ya mwajiri na kama hawana kazi basi wawe na barua kutoka Serikali za mitaa.
Pia, mshtakiwa anatakiwa asitoke nje ya nchi bila ruhusa ya Mahakama.
Mshtakiwa amefanikiwa kupata dhamana na kesi yake imeahirishwa hadi Machi 6, 2025 kwa kutajwa.