Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UN) linajiandaa kufanya kikao cha dharura kesho Ijumaa, kuujadili mgogoro wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
Msemaji wa baraza hilo, Paschal Sim amewaambia waandishi habari mjini Geneva kwamba kikao hicho kimeitishwa kufuatia ombi la serikali ya Kongo inayoongozwa na Felix Tchisekedi lililotolewa Jumatatu wiki hii.
Baraza hilo kimsingi ndio chombo cha juu zaidi katika Umoja wa Mataifa kinachohusika na masuala ya haki za binadamu na kwa hakika kilikuwa hakina ratiba ya kukutana hadi mwishoni mwa Februari mwaka huu.
Lakini ombi la serikali ya DRC kufuatia hali inayoendelea mashariki mwa nchi yake, kumelifanya baraza hilo lenye jumla ya wanachama 47, Kongo ikiwa ni miongoni mwa wanachama hao, kuitisha mkutano huo wa dharura huku Rwanda chini ya Paul Kagame ikishutumiwa kuwasaidia waasi wa M23 nao kukanusha.
Stori: Elvan Stambuli | GPL