Bunge lataka Serikali iandae mfumo wa kidijitali utambuzi wa bodaboda

Dodoma. Bunge limeazimia Serikali kuandaa mfumo rasmi wa kisasa wa kidijitali kwa ajili ya utambuzi wa waendesha bodaboda ili kukabiliana changamoto za ajali na uhalifu.

Bunge limeazimia hayo baada ya kuulizwa na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson na wengi wao kuitikia ‘ndiooo’ bungeni leo Alhamis Februari 6, 2025.

Hatua hiyo ilitokana na taarifa ya mwaka ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, iliyowasilishwa bungeni na mwenyekiti wa kamati hiyo, Vita Kawawa.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Kawawa amesema kukosekana kwa mfumo wa utambuzi wa waendesha bodaboda kidijitali nchini ni changamoto inayosababisha kutokuwepo kwa takwimu rasmi za waendesha bodaboda.

Amesema kukosekana kwa mifumo ya kidijitali kunachochea kutokuwa na utambuzi wa waendesha bodaboda kwa kudhoofisha usajili, udhibiti na ufuatiliaji wao.

Kawawa amesema hali hiyo ya usajili, udhibiti na ufatiliaji wa waendesha bodaboda inasababisha athari kubwa kwa jamii na maendeleo ya nchi ikiwamo kuongezeka kwa ajali za barabarani ambazo huleta vifo, ulemavu na mzigo mkubwa kwa sekta ya afya kutokana na matibabu ya waathirika katika ajali.

Kawawa ambaye pia ni mbunge wa Namtumbo (CCM), amezitaja athari nyingine ni kushamiri kwa uhalifu wa kutumia bodaboda kutokana na kuwepo kwa waendesha bodaboda wasiosajiliwa ambao hutumiwa na wahalifu kufanya ujambazi, wizi wa simu na uporaji.

Nyingine ni kuongezeka kwa migongano kati ya Serikali na waendesha bodaboda kutokana na taratibu za usajili na utoaji wa leseni, kukosa uwazi na kudhoofisha utekelezaji wa Sheria za Usalama Barabarani na kuhatarisha maisha ya waendesha bodaboda, abiria na watumiaji wengine wa barabara.

Amesema kukosekana kwa utambuzi rasmi kunasababisha sekta hiyo kukosa udhibiti, hivyo waendesha bodaboda hutumia mwanya huo kutofuata sheria mbalimbali za nchi ikiwamo Sheria ya Usalama Barabarani na pia baadhi yao ambao sio waadilifu kushiriki kwenye matukio ya uhalifu pasipo kutambulika kwa urahisi.

“Kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali ilisimamie Jeshi la Polisi ili liweze kushirikiana na Latra (Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhi), halmashauri za miji na wilaya na taasisi nyingine za Serikali pamoja na wadau mbalimbali, kuandaa mfumo rasmi wa kisasa wa kidijitali kwa ajili ya utambuzi wa waendesha bodaboda nchini,” amesema Kawawa.

Kauli ya waendesha bodaboda

Akizungumza nje ya Bunge, Mwenyekiti wa Waendesha Bodaboda Tanzania, Saidi Kagomba amesema mwitikio ni mzuri  wa shughuli ya usajili wa waendesha bodaboda ulioanza Julai mwaka jana.

“Mfumo huu utatufanya kutambulika kwa waendesha bodaboda na kusaidia katika kupambana na uhalifu uliokuwa ukifanyika kwa kutumia bodaboda na pia hata wao watajikinga na uhalifu pia kwa sababu sasa watatambulika katika kituo wanachotoka kwa majina, taarifa na nyingine zitakuwa katika mfumo,”amesema.

Kagomba amesema pia, utawawezesha kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha kwa kuwa watakuwa wanatambulika.

Hata hivyo, ameomba Serikali kuwasaidia katika kuwawezesha kupata sare maalumu kwa waendesha bodaboda ambazo licha ya kuwakinga na baridi, kutawawezesha kutambulika kwa urahisi.

Kagomba  amesema Sh56,000 kwa kila sare, ni ngumu kwa baadhi ya waendesha bodaboda kuelewa kwamba haifanyiki biashara.

“Tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan atusaidie katika hili, maana hatutatoa sare kwa mtu ambaye hana leseni, hajalipa maegesho na ushuru mwingine wa halmashauri, hivyo itasaidia katika kuongeza mapato ya nchi,” amesema Kagomba.

Uchakavu wa miundombinu magereza

Kawawa pia, amesema uchakavu wa miundombinu ya magereza nchini unaongezeka kutokana na ukosefu wa mpango mahususi wa kuboresha miundombinu hiyo.

Amesema hali hiyo ya miundombinu kuendelea kuchakaa inaathiri dhima ya huduma za magereza kutokana na baadhi ya magereza kuwa na wafungwa na mahabusu kuliko uwezo wake jambo linalohatarisha afya na usalama wa wafungwa.

Amesema ukosefu wa huduma bora za majisafi, vyoo na usafi wa mazingira unasababisha magonjwa ya mlipuko.

Pia, amesema unapunguza ufanisi wa ulinzi na kusababisha hatari ya wafungwa kutoroka au kushambulia maofisa wa magereza.

Kawawa amesema ukosefu wa mazingira bora ya kuwezesha huduma za urekebu ambalo ni jukumu la msingi la Jeshi la Magereza na changamoto za lishe na huduma za kijamii zinazotokana na miundombinu duni ya maghala ya chakula, jiko na huduma za msingi.

Kawawa amesema ukosefu wa ofisi bora, makazi na vifaa vya kazi unaweza kushusha morali ya maofisa na askari wa magereza na mzigo kwa Serikali wa gharama kubwa za uendeshaji kutokana na kuharibika kwa miundombinu mara kwa mara na matibabu ya magonjwa yanayoweza kuzuilika.

“Bunge linaazimia kwamba, Serikali iandae mpango mahsusi unaotekelezeka wa kuboresha miundombinu ya magereza,” amesema.

Kawawa pia, amesema kutokutumika kwa teknolojia ya kisasa katika udhibiti wa ajali za barabarani kunasababisha ugumu wa kuwabaini madereva na watumiaji wengine wa barabara wanaokaidi sheria za usalama barabarani.

Amesema matokeo ya kutokutumika kwa teknolojia ya kisasa ili kudhibiti vichocheo vya ajali yanasababisha vifo, ulemavu na mzigo kwa Serikali kugharamia matibabu ya waathrika wa ajali.

Ametaka Bunge kuazimia kwamba, Jeshi la Polisi lifanye tathmini ya mpango wake wa kudhibiti na kuzuia ajali barabarani kwa lengo la kubaini kama mpango huo unafanikisha tija iliyokusudiwa katika kudhibiti na kuzuia ajali za barabarani.

Ametaka Bunge kuazimia pia,  Serikali iweke mpango mkakati unaotekelezeka wa ununuzi wa vifaa vya kisasa kwa kuzingatia teknolojia mahsusi kwa uhalisia wa barabara na kuvifunga kuanzia barabara kuu ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupambana kudhibiti ajali za barabarani.

“Serikali iandae mpango wa kuwapatia mafunzo askari wa usalama barabarani ili kuwa na uelewa na ujuzi wa kutumia na kufuatilia vifaa vya kiteknolojia vitakavyofungwa kwa ajili ya usalama barabarani,” amesema Kawawa.

Upungufu wa mafuta na sukari

Akiwasilisha bungeni taarifa ya mwaka ya utekelezaji wa majukumu ya Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deodatus Mwanyika, amesema kutokana na kutopatikana kwa sukari ya kutosha kunaweza kusababisha upungufu wa sukari:

Pia, amesema kutowafikia walaji kwa wakati na bei kuwa juu, hivyo Bunge linaazimia Serikali iendelee kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya sukari ili kuongeza uzalishaji.

Aidha, Bunge linaazimia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) uwezeshwe kununua, kutunza na kusambaza sukari uhaba unapotokea.

Pia, Mwanyika amesema kamati inaishauri Serikali kuendelea na mikakati ya kuhakikisha sukari ya kutosha inazalishwa nchini ili kupunguza kutegemea kutoka nje ya nchi na kuzalisha bidhaa zaidi ya moja yaani sukari, umeme na methanol.

“Serikali ihakikishe kuwa miundombinu ya barabara za mashambani na ya umwagiliaji katika mashamba ya miwa ya wakulima wadogo inatengenezwa ili kurahisisha usafirishaji. Kamati inashauri uwekezaji ufanyike ili uzalishaji wa sukari ya viwandani ufanyike hapa nchini,” amesema.

Kuhusu hali ya mafuta ya kula nchini, amesema bado kuna upungufu wa mafuta ya kula unaosababishwa na wakulima wengi kusitisha kilimo cha alizeti kutokana na kukosa soko la uhakika.

Amesema upungufu huo wa mafuta unasababisha wafanyabiashara kuingiza shehena kutoka nje ambayo huuzwa kwa bei ya juu.

“Bunge linaazimia Serikali iendelee kuhamasisha, kuendeleza na kujenga viwanda vya kutosha vya kuzalisha mafuta ya kula nchini ili kupunguza utegemezi wa uingizaji wa mafuta ya kula na kujihakikishia usalama wa chakula nchini,”amesema.

Pia, amesema Bunge linaazimia Serikali iendelee kupitia upya vivutio ilivyotoa kwa wazalishaji wa ndani wa mafuta ili kuondoa athari zilizojitokeza kwa wakulima wa alizeti.

Mwanyika amesema alizeti kama ilivyo kwa mazao mengine, iwekewe bei ambazo zitawavutia wakulima ili wahamasike kulima kwa wingi.

Related Posts