Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Kiongozi Mkuu wa 49 wa Madhehebu ya Shia Ismailia na mwanzilishi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), Mtukufu Aga Khan IV.
Mtukufu Aga Khan amefariki dunia akiwa na miaka 88 Jumanne, Februari 4, 2025 jijiji Lisbon, Ureno akiwa amezungukwa na familia yake.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi kwa umma, baada ya kifo cha mfalme huyo, Imamu wa 50 wa madhehebu ya Shia Ismailia, Rahim Aga Khan V ametangazwa kurithi mikoba ya Aga Khan IV.
Taarifa ya CCM iliyotolewa na Amos Makalla, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo imesema chama hicho kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mtukufu Aga Khan IV.
Makalla amesema Mtukufu Aga Khan alikuwa mtu wa dira, mwenye dhamira thabiti ya kuimarisha ustawi wa jamii kupitia elimu, afya na maendeleo ya kiuchumi, siyo tu katika Afrika Mashariki bali pia duniani kote.
“Mchango wake umeacha alama isiyofutika katika sekta mbalimbali, hasa kupitia taasisi za Aga Khan ambazo zimeleta tija kwa watu wa Tanzania na ukanda mzima wa Afrika Mashariki,” amesema Makalla.
Amesema katika kipindi chote cha uongozi wake, alihimiza mshikamano, ustahimilivu na utu, akithibitisha kwamba maendeleo ya watu ni msingi wa jamii yenye mafanikio.
“Kwa dhati, CCM inatambua na kuthamini mchango wake katika kuimarisha sekta muhimu zinazogusa maisha ya watu moja kwa moja, hususan elimu, habari na afya, ambazo zimekuwa nguzo muhimu kwa ustawi wa taifa letu.
Kwa niaba ya viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi, tunatoa pole kwa familia ya Mtukufu Aga Khan, jumuiya ya waumini wa Shia Ismailia, na wote walioguswa na msiba huu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awape nguvu na faraja katika kipindi hiki kigumu,” amesema.
Makalla amehitimisha taarifa hiyo akisema: “Tunamuombea apumzike kwa amani, Mtukufu Aga Khan.”