Fahamu namna ajali za bodaboda na ulaji wa ‘kitimoto’ zinavyosababisha ugonjwa wa kifafa

Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku tatu kuazimisha siku ya Kimataifa ya Kifafa duniani itakayoadhimishwa Februari 10, 2025, imeelezwa ugonjwa huo husababishwa na hitilafu ya kusambaa kwa umeme kupitia mishipa iliyopo kwenye ubongo.

Akizungumza na waandishi wa habari wiki hii kuelekea siku hiyo itakayofanyika Jumatatu ijayo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Fahamu, Ubongo na Mishipa ya Uti wa Mgongo, Patience Njenje, amesema ajali kama za bodaboda na ulaji wa nyama ya nguruwe isiyoiva vizuri ni miongoni mwa sababu za kupata ugonjwa wa kifafa.

Dk Njenje amesema ikitokea sehemu ya ubongo wa binadamu imepata kovu basi kovu hilo litasababisha hitilafu ya kusambaa kwa umeme kupitia mishipa iliyopo kwenye ogani hiyo muhimu.

Amesema kovu hilo linaweza kusababishwa na ajali kama kuanguka na bodaboda ambayo mtu anaweza akijipigiza kichwa au akipata ugonjwa wa kiharusi ambao unapasua au kuziba mishipa ya damu kwenye ubongo.

Kwa mujibu wa Dk Njenje hali hiyo inapotokea, sehemu ya ubongo inayokosa damu itabadilika na kuwa na kovu, na hivyo kushindwa kufanya kazi vizuri.

Amesema sababu nyingine za kovu kwenye ubongo ni mtoto kuzaliwa kwa uzazi pingamizi, ambapo atachelewa kutoka na hivyo kukosa hewa, jambo linaloweza kusababisha mishipa ya ubongo kutengeneza kovu.

Pia, Dk Njenje amesema uvimbe kwenye ubongo unaozuia umeme kupita na ulaji wa nyama ya nguruwe isiyoiva, inaweza kuchangia.

Amesema ubongo ni kama mota ya umeme yenye nyaya zinazopitisha umeme, hivyo kovu linapokutana na umeme, umeme huo husababisha kuzidi kwa mkusanyiko wa nguvu na baadaye kumwagika ghafla, hali inayopelekea kifafa.

Minyoo kwenye nyama ya nguruwe isiyoiva

Dk Njenje pia alielezea kuhusu minyoo inayopatikana kwenye nyama ya nguruwe isiyoiva vizuri.

Alisema minyoo hii ina tabia ya kwenda kwenye ubongo, ambapo inaweza kusababisha kifafa baada ya muda.

Dk Njenje alisema hali ni kwa sababu minyoo hupenda kula chakula cha damu, na mara nyingi damu huenda kwa wingi kwenye ubongo.

Alisema minyoo ikikua, inakandamiza ubongo, na hivyo husababisha kifafa, ingawa tatizo hili linatibika.

Kwa mujibu wa Dk Njenje ni muhimu kuhakikisha nyama ya nguruwe inaliwa ikiwa imeiva vizuri ili kuepuka minyoo.

Pia, Dk Njenje alieleza kuwa ajali nyingine zinazoweza kusababisha kifafa ni pamoja na mtu kuanguka, kuteleza bafuni, au watoto kuanguka na kujipigiza kichwa.

Alisema ajali hizo zinaweza kusababisha kovu kwenye ubongo, na baada ya muda, kuzalisha kifafa.

Pia, amesema malaria kali, homa ya uti, na typhoid ni magonjwa yanayoweza kusababisha matatizo kwenye ubongo wa watoto, kutokana na mabadiliko ya joto la mwili.

Dk Njenje ameelezea aina mbili za kifafa ambazo ni kifafa kikubwa na kifafa kidogo.

Amesema kifafa kikubwa kinahusisha kuanguka, kupungua kwa kumbukumbu, na mwisho kufikia ukichaa.

Kifafa kidogo kinahusisha dalili kama mkono au sura kucheza, na mara nyingi kinahusisha upande mmoja wa ubongo.

“Ingawa kifafa kidogo kinaweza kupona kabisa, kifafa kikubwa husababisha madhara ya kudumu,” amesema.

Kifafa kutokana na ajali za bodaboda

Dk Njenje amebainisha kwamba vijana wenye umri wa kuanzia miaka 15 wanapata kifafa kwa wingi, hasa kutokana na ajali za bodaboda.

Amesema baada ya ajali hizi, mtu anaweza kupata kifafa baada ya miaka kadhaa.

Dk Njenje ameongeza kuwa watu wanaopata kifafa wanapaswa kuepuka matibabu ya waganga wa kienyeji na wachungaji kwemye makanisa wanaotibu kwa mamombi na badala yake wafuate matibabu ya kisayansi ili kurekebisha sehemu ya ubongo iliyopata kovu na kumwezesha umeme kupita vizuri.

Kifafa duniani na Tanzania

Dk Njenje amesema kwa mujibu wa takwimu za kimataifa, kifafa ni ugonjwa wa kudumu wa ubongo unaathiri watu milioni 60 duniani, na Afrika ina idadi kubwa ya waathirika.

Amesema nchini Tanzania, kuna takriban watu milioni moja wanaoishi na kifafa. Ingawa jitihada za pamoja zimeongeza matumaini, kiwango cha vifo kwa wagonjwa wa kifafa bado ni cha juu.

Dk Njenje amesema jamii inapaswa kuepuka kuwanyanyapaa watu wenye kifafa katika maeneo ya elimu, ndoa, na kazi.

Kwa mujibu wa Dk Njenje kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Kifafa hakipaswi kuwa kikwazo kwa maisha ya mtu yeyote. Tusimame wote dhidi ya Kifafa.”

Related Posts