Licha ya ukuaji wa haraka wa teknolojia ya simu za mkononi barani Afrika, mamilioni ya wanawake bado hawajaunganishwa kidijitali, jambo linalopunguza fursa zao za kiuchumi na ustawi wao wa maisha.
Ripoti ya Shirikisho la Kampuni za Simu (GSMA) ya mwaka 2024 kuhusu pengo la kijinsia katika huduma za simu za mikononi inaonyesha tofauti kubwa, wanawake wa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara wana uwezekano mdogo wa kumiliki simu ikilinganishwa na wanaume kwa asilimia 13, huku matumizi ya intaneti ya simu tofauti ikiwa ni asilimia 32.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa pengo hili lina athari kubwa, likiongeza ukosefu wa usawa wa kiuchumi na kuzuia ushiriki wa wanawake katika uchumi wa kidijitali unaokua kwa kasi. Teknolojia ya simu za mkononi imeleta mabadiliko makubwa katika upatikanaji wa huduma za kifedha, elimu na ajira.
Hata hivyo, mamilioni ya wanawake wa Kiafrika bado hawana fursa ya kunufaika na maendeleo haya kutokana na vikwazo mbalimbali.
Hata hivyo, ripoti hiyo inaonyesha kuwa ingawa umiliki wa simu miongoni mwa wanawake umeongezeka, kwa nchi za kusini mwa jangwa na Sahara asilimia 71 ya wanawake wanamiliki simu ya mkononi ikilinganishwa na asilimia 82 kwa wanaume.
Hata wanawake wanapomiliki simu, mara nyingi huwa ni za kawaida zisizo na uwezo wa kuunganisha intaneti, hali inayowazuia baadhi yao kunufaika na uchumi wa kidijitali, ikiwamo huduma za kifedha. Hii inamaanisha kuwa takriban wanawake milioni 200 Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara bado hawajaunganishwa na huduma za mtandao, huku kwa mataifa yote yanayoendelea idadi ikiwa ni milioni 785.
Vikwazo vya upatikanaji wa simu na intaneti
Pengo hili la kidijitali linasababishwa na vikwazo kadhaa, kwa mujibu wa ripoti hiyo ikiwa ni pamoja na gharama, ujuzi wa kidijitali, kanuni za kijamii na usalama.
Mathalani bei ya simu na gharama za data za intaneti bado ni kikwazo kikubwa kwa wanawake wengi, ambao mara nyingi wana kipato cha chini zaidi kuliko wanaume.
Bei ya simu mahiri ni ya juu sana, hivyo kufanya iwe vigumu kwa wanawake kununua vifaa.
Pili, wanawake wengi hawana ujuzi wa kutosha wa kidijitali kutumia teknolojia ya simu ipasavyo. Mfano wanawake waliohojiwa nchini Senegal, asilimia 56 walitaja suala la ujuzi kama kikwazo kikubwa, ikilinganishwa na wanaume ambao wao ilikuwa ni asilimia 40.
Kadhalika katika jamii nyingi, mitazamo ya kitamaduni huwazuia wanawake kutumia simu za mkononi au intaneti.
Nchini Pakistan, asilimia 19 ya wanawake walitaja utamaduni wa jamii yao kama kikwazo kikubwa cha wao kutumia intaneti ya simu, ikilinganishwa na asilimia nne kwa wanaume.
Na sababu nyingine inayotajwa na ripoti hiyo ni wasiwasi kuhusu unyanyasaji wa mtandaoni, ukiukwaji wa faragha na ulaghai wa mtandaoni.
Ripoti ilionyesha kuwa wanawake wengi wana hofu ya usalama katika matumizi ya intaneti kuliko wanaume.
Mtaalamu wa uchumi na biashara, Profesa Aurelia Kamuzora anasema tatizo hili ni la kidunia na kitaifa, kwani wanawake wamekuwa wakiachwa nyuma, hasa katika umiliki wa mali.
Hiyo ni kutokana na tamaduni zilizopo ambazo zimekuwa zikiwafanya wanawake kubaki nyuma.
Anasema hili hutokea hata ndani ya familia, ikiwa kitapatikana kitu kimoja basi baba ndiyo atakuwa wa kwanza kukimiliki kuliko mwanamke kwa sababu wanaamini ndiye anaweza kuitumia vyema.
“Hata kama ni mwanamke ndiyo alipewa zawadi hiyo, kama mume wake hana atampatia kwanza mwanamume wake ili kuhakikisha kunakuwa na usawa,” anasema.
Anasema suala la kipato ndani ya familia nalo ni changamoto, hali inayofanya kidogo kinachopatikana kuangukia katika umiliki wa mwanamume, huku akitolea mfano kuwa, hata nyumba ikijengwa ataandikwa mwanamume, jambo ambalo huweza kutokea hata kwenye simu ambayo huweza kununuliwa kwa jina la mwanamume, lakini akatumia mwanamke.
“Tukiweza kupunguza hili tunaweza kuwa tumesaidia wanawake na kuwapa uwezo mkubwa kwa sababu mawasiliano ndiyo biashara, elimu na uwezeshaji, anayewasiliana lazima awe anahitajika katika jamii kwa sababu ana uwezo, hivyo mwanamke akisaidiwa mawasiliano ataweza kusaidia familia, kulea familia vizuri, kukuza uchumi kwa kufanya biashara,” anasema Profesa Kamuzora.
Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania, inakiri kuwa matokeo ya utafiti huo yanaakisi hali ya Tanzania na katika ripoti yao ya uendelevu (ESG) wameeleza jinsi wanavyoshughulikia changamoto ya kumaliza pengo la kijinsia katika matumizi ya huduma za kidijitali.
Kampuni hiyo yenye wateja zaidi ya milioni 26.3, hadi kufikia Desemba mwaka jana, inaeleza kuwa inaamini katika kuunganisha watu na huduma za kidijitali katika kukuza uchumi, hivyo inakusudia kutomuacha mtu yeyote nyuma.
Kwa upande wa kuwawezesha wanawake kiuchumi, kampuni hiyo inaeleza kuwa kwa kushirikiana na Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania, wametoa suluhu ya mawasiliano, ikiwa ni pamoja na huduma za intaneti, simu za mkononi, SMS za jumla, M-Pesa na zaidi.
Na huduma hizo zinapatikana kote Tanzania ili kuhakikisha hakuna mwanamke anayeachwa nyuma.
Vodacom inalenga kuhakikisha inamaliza changamoto ya uwezo mdogo wa kumiliki simu miongoni mwa wanawake kwa kutoa simu za bei nafuu ili kutomwacha yeyote nyuma, kwa kuwa wanaamini katika nguvu ya kuunganisha watu na huduma za kidijitali katika kuimarisha uthabiti wa kiuchumi.
“Ushirikiano kati ya Vodacom Tanzania, Benki ya NMB na Google ulifanya simu za 4G za bei nafuu zipatikane kote Tanzania, zikinufaisha wateja 13,317, wengi walinunua simu hizo kupitia mpango wa ‘Miliki Simu Lipa Mdogo Mdogo,” inaeleza ripoti, ambayo pia ilibainisha kuwa kwa mwaka 2023 pekee, walitoa vifaa vya kidijitali 199,710.
Kadhalika ripoti ya ESG ya Vodacom inaeleza kuwa wana mpango wa kupunguza gharama ya intaneti, kuongeza thamani ya vifurushi ili kuwasaidia watumiaji, ikiwa ni pamoja na vijana na kaya za kipato cha chini. “Just4You hutoa ofa za kipekee kwa wateja kulingana na matumizi yao ya sauti, SMS na intaneti ili kuwasaidia kuokoa pesa. Kwa mwaka wa fedha wa 2023 asilimia 56 ya wateja wao walikuwa wakitumia Just4You,” inaeleza.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa wanatumia simu za mkononi kuboresha maisha ya wanawake kupitia programu zinazorahisisha upatikanaji wa kifedha, afya na ustawi, elimu, ujuzi na ujasiriamali.
“Katika nchi nyingi za Afrika, kupata taarifa bora za afya na huduma ya uzazi ni changamoto. Tumetambua ukosefu wa taarifa kama moja ya sababu kuu za vifo vya watoto na kina mama na tunafanya kazi ya kuziba pengo hili kupitia programu za simu kama m-mama,” inaeleza ripoti hiyo, iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wao, Philip Besiimire.
Athari za kutokuwa na ujumuishi
Kulingana na ripoti hiyo ya GSMA, kumaliza pengo la kijinsia katika matumizi ya simu ni jambo muhimu kiuchumi, kwani inakadiriwa kuwa nchi 32 za kipato cha chini na cha kati zinaweza kupoteza zaidi ya dola bilioni 500 katika Pato la Taifa (GDP) ndani ya miaka mitano ijayo kutokana na pengo la kidijitali la kijinsia
Huduma za kifedha za simu, zimeleta mapinduzi katika sekta ya benki barani Afrika.
Hata hivyo, pengo la kijinsia katika umiliki wa simu linamaanisha kuwa wanawake wengi hawawezi kufikia huduma hizi, na hivyo kuendelea kuwa nyuma kiuchumi.
Katika sekta ya kilimo, teknolojia ya simu huwapa wakulima taarifa za mara moja kuhusu bei za soko, hali ya hewa na mbinu za kilimo.
Ripoti hiyo iliongeza kuwa, wanawake, ambao ni sehemu kubwa ya wafanyakazi wa kilimo, mara nyingi hukosa fursa hizi kutokana na ukosefu wa upatikanaji wa simu, jambo linalopunguza uzalishaji wao na mapato.