UKISIKIA kata mti panda mti, ndicho kilichofanywa na Yanga baada ya mabosi wa klabu hiyo kushtushwa na uamuzi wa ghafla wa kocha Sead Ramovic aliyeomba kuvunja mkataba kisha juzi Jumanne akawaaga wachezaji na maofisa wengine wa timu.
Hata hivyo, chapu mabosi hao wa Yanga wakambeba kocha mpya Hamdi Miloud kutoka Singida Black Stars ambaye jana asubuhi alitua jijini Dar es Salaam kutoka Arusha ilipo kambi ya timu na kukutana na vigogo wa klabu hiyo ya Jangwani ili kumalizana kabla ya jioni kwenda KMC kuiangalia timu ikicheza.
Yanga jana jioni ilikuwa uwanjani kupambana na KenGold ya Mbeya katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, lakini mapema mchana kikosi kizito kilifanya eneo la Salamander ili kumalizana na kocha huyo raia wa Ufaransa mwenye asili ya Algeria.
Hamdi alijiunga na Yanga saa chache baada ya Ramovic kuwaaga wachezaji na maofisa wenzake akiwatoa kwamba amepata ofa nono huko Algeria na walipombana zaidi kujua anakwenda timu ipi, ikafahamika kwamba atajiunga na CR Belouizdad.
Inaelezwa kwamba Waalgeria wamemwekea mzigo wa maana Ramovic ikiwamo ofa ya kulipwa mshahara wa Dola 40,000 (zaidi ya Sh101 milioni) kwa mwezi tofauti na kiwango alichokuwa anapokea Yanga kinachodaiwa kuwa ni Dola 15,000 (zaidi ya Sh38 milioni).
Pia Ramovic katika kusitisha kwake mkataba aliokuwa nao na klabu hiyo ameilipa Yanga mshahara wa mwezi mmoja tu, ambao ni Sh38 milioni tofauti na taarifa zilizozagaa kwamba klabu ya Belouizdad imeilipa Yanga Dola 50,000 (zaidi ya Sh127 milioni) katika dili la kocha huyo Mjerumani.
Ramovic alitua Yanga Novemba 15, mwaka jana akitokea TS Galaxy ya Afrika Kusini na kuiongoza katika mechi 13 tofauti zikiwamo sita za Ligi Kuu Bara na nyingine kama hizo za Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na moja ya Kombe la Shirikisho (FA).
Katika Ligi Kuu, Ramovic alishinda zote sita timu ikifunga mabao 22 na kufungwa mawili pamoja na kuvuna pointi 24, huku kwenye michuano ya CAF, ilishinda mechi mbili na kupoteza mbili na mbili nyingine ziliisha kwa sare, timu ikivuna pointi nane na kufunga mabao matano na kufungwa sita.
Kwa mechi za Kombe la Shirikisho iliyocheza dhidi ya Copco ya Mwanza, watetezi hao walishinda kwa mabao 5-0 na kutinga hatua ya 32 Bora.
Kocha huyo aliyetambulishwa na Singida Desemba 30, mwaka jana kuchukua nafasi ya Patrick Aussems aliyetimuliwa, huku akiwa hajawahi kuitumikia timu hiyo katika mechi yoyote ya mashindano, zaidi ya kuisimamia kucheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya timu za Ligi ya Championship.
Hamdi alipewa mkataba wa mwaka mmoja na nusu akiwa sambamba na wasaidizi wake Nassim Anisse na David Ouma na kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Mbuni na TMA zote za Arusha na kushinda kwa mabao 4-1 na 2-1 mtawalia kabla ya kuibukia Yanga.
Kocha huyo ana rekodi nzuri ya kufika hatua ya fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Robo Fainali mara mbili Ligi ya Mabingwa Afrika na Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika
Vilevile, Hamdi ana uzoefu mkubwa na soka la Afrika kwa kuzinoa klabu mbalimbali kwa mafanikio makubwa barani Afrika zikiwemo USM Alger na JS Kabylie za Algeria, Al- Salmiya ya Kuwait, TP Mazembe ya Congo, Athletico Marseille na ES Vitrolles za Ufaransa na Al- Ettifaq FC ya Saudia Arabia.
Ukiacha wasifu huo wa kuwa na uzoefu wa soka la Afrika na mafanikio makubwa aliyonayo kupitia timu kadhaa alizowahi kuzinoa, kocha huyo ana Leseni Daraja A iliyotolewa na Umoja wa Vyama vya Soka barani Ulaya (UEFA).
Kama Bodi ya Ligi Kuu Tanzania na Idara ya Ufundi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) watasimamia vyema kanuni za Ligi Kuu msimu huu, hakuna namna Miloud atalazimika kushushwa cheo na kuwa kocha msaidizi kwa daraja la leseni haliyonayo, kwani kwa sasa haimtoshi kumfanya awe kocha mkuu wa timu inayoshiriki Ligi Kuu.
Kanuni ya 77 ya Ligi Kuu imefafanua sifa za kocha mojawapo ikiwa ni hadhi ya leseni inayofafanua kuwa kocha mwenye Leseni kutoka nje ya Afrika anapaswa kuwa na ngazi ya Pro Diploma ambayo kwa Afrika ni sawa na Diploma Daraja A.
“(1) Kila klabu inapaswa kuajiri Kocha Mkuu na wasaidizi wenye sifa na ujuzi kwa timu ya kwanza (wakubwa) na za vijana (U20 na U17) wanaokubalika kwa mujibu wa taratibu za TFF na mikataba yao kusajilia TFF.
“(2) Kocha toka nje ya nchi atathibitishwa kwanza na TFF kwa kuzingatiwa pia kupatikana kwa kibali stahili cha kuishi na kufanya kazi chini kabla ya kuingia mkataba na klabu.
“(3) Kocha Mkuu anatakiwa kuwa na angalau Diploma A ya CAF au inayolingana na hiyo iliyotolewa na Mashirikisho ya mabara mengine yanayotambuliwa na FIFA. Kocha Msaidizi anatakiwa kuwa na angalau Diploma B ya CAF au inayolingana na hiyo iliyotolewa na Mashirikisho ya mabara mengine yanayotambulia na FIFA.
“.1 Kocha mkuu wa klabu ya Ligi Kuu kutoka nje ya bara la Afrika anatakiwa kuwa na angalau Pro Diploma au inayolingana nayo. 3.2 Kocha msaidizi wa klabu ya Ligi Kuu kutoka nje ya bara la Afrika anatakiwa kuwa na angalau A Diploma au inayolingana nayo.
“Kocha wa timu ya Ligi Kuu kutoka nje ya Tanzania ni lazima awe amefundisha klabu ya Ligi Kuu au timu ya Taifa katika nchi yoyote ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita,” inafafanua kanuni hiyo.
Hata hivyo, hii sio mara ya kwanza kwa klabu kumtambulisha kocha mkuu, lakini katika makaratasi yaliyopo TFF yakamtambua kama kocha msaidizi, kwani ilishatokea kwa makocha wa Azam FC, Yousouf Dabo na Ferry Bruno na hata kipindi cha Kally Ongala na Dani Cadena.
Hivyo, hata kwa sasa licha ya vigezo kumkataa Hamdi, lakini katika benchi la Yanga kuna watu wenye cv ya kutosha wanaoweza kumbeba akiwamo kocha msaidizi Abdihamid Moallin ambaye ana sifa stahiki za kuliongoza benchi la ufundi la Yanga kwa vile ana Leseni Daraja A inayotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Mara baada ya Yanga kutangaza kumnyakua, Hamdi, Singida Black Stars kupitia Idara ya Habari na Mawasiliano ilitoa taarifa kushangazwa na kitendo cha kuchukuliwa kocha kienyeji na hata jana mchana ilipoulizwa juu ya jambo hilo, Ofisa Habari Hussein Massanza alisema wanashikilia walichoandika katika taarifa yao, huku viongozi wa Yanga wakikosekana kufafanua hilo.
Kocha hupo mpya wa Yanga atakuwa na kazi kubwa kutokana na rekodi zilizoachwa na makocha wenzake walioondoka klabuni hapo kuanzia, Gamondi hadi Ramovic.
Gamondi mwanzoni mwa msimu huu aliiongoza Yanga kucheza mechi nane mfululizo bila kupoteza wala kuruhusu bao, kabla ya kutibuliwa na Azam FC iliyomtungua 1-0 kisha Tabora United kufunga 3-1 na kukamilisha kibarua chake Jangwani na kurothiwa na Ramovic.
Balaa la Gusa Achia la Ramovic limemfanya kocha huyo kuingoza Yanga katika mechi sita mfululizo bila kupoteza, timu ikishinda mabao 22 na kufungwa mawili, kitu kinachompa wakati mgumu Hamdi ambaye ana mechi tano kwa sasa ndani ya Febaruari kabla ya kukabiliana na Simba Machi 8.
Ramovic hadi anaondoka Yanga hajakutana na Simba katika mchezo wowote wa Dabi ya Kariakoo, tofauti na Gamondi aliyeshinda mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu dhidi ya Simba, zikiwamo mbili za msimu uliopita na moja ya awali kwa msimu huu.
Kama atatoboa katika mechi hizo zijazo na kushinda Dabi ya Kariakoo inaweza kumpa heshima Hamdi, lakini mambo yakienda kinyume atakuwa na kazi kubwa ya kujenga imani kwa Wanayanga waliokuwa wanatamba kitaani kwa kuwanyamazisha Simba tangu msimu uliopita walipoifumua 5-1.
Licha ya kuondoka kwa Ramovic kumewashtua wanayanga kama ambavyo Singida ilivyoshtushwa kwa kuondoka kwa Hamdi kwenda Yanga, lakini hata katika dunia iliyoendelea katika soka, japo si jambo la kawaida, lakini makocha kuhama klabu katikati ya msimu hutokea kutokana na sababu mbalimbali.
Moja ya sababu hizo ni matokeo mabaya, tofauti za kiutawala, au fursa mpya zinazojitokeza na mikataba ya makocha huundwa kwa namna inayowapa uhuru wa kuondoka, mradi wanazingatia vipengele vilivyowekwa katika makubaliano yao na klabu husika.
Moja ya vipengele muhimu vya makocha katika mikataba ni; 1) Kifungu cha Kuvunja Mkataba (Release Clause): Hiki ni kipengele kinachoweka kiwango cha fidia ambacho klabu inayotaka kumsajili kocha inatakiwa kulipa kwa klabu anayoifundisha kwa wakati huo. Iwapo klabu mpya inakubali kulipa kiasi hiki, kocha anaruhusiwa kuondoka kabla ya kumaliza mkataba wake.
2). Makubaliano ya Pande Zote (Mutual Agreement): Klabu na kocha wanaweza kukubaliana kuvunja mkataba kwa ridhaa ya pande zote mbili. Katika hali hii, masharti ya kifedha na muda wa kuondoka hujadiliwa na kukubaliwa pamoja.
3. Kifungu cha Uaminifu (Loyalty Clause): Baadhi ya mikataba hujumuisha kipengele kinachomlazimu kocha kutohama kwenda klabu pinzani ndani ya muda fulani baada ya kuondoka. Hii inalenga kulinda maslahi ya klabu dhidi ya ushindani wa moja kwa moja.
Mifano ya Makocha waliowahi kuhama katikati ya msimu barani humo ni; Brendan Rodgers: Mnamo Februari 2019, Rodgers aliondoka Celtic katikati ya msimu na kujiunga na Leicester City ya Ligi Kuu ya England. Uhamisho huu ulifanyika baada ya Leicester kulipa fidia kwa Celtic ili kuvunja mkataba wake.
Thomas Tuchel: Mwezi Januari 2021, Tuchel aliteuliwa kuwa kocha wa Chelsea baada ya klabu hiyo kumtimua Frank Lampard katikati ya msimu. Tuchel alikuwa huru baada ya kuachana na Paris Saint-Germain mwezi Desemba 2020.
Julian Nagelsmann: Mnamo Machi 2021, ilitangazwa kuwa Nagelsmann angeondoka RB Leipzig mwishoni mwa msimu na kujiunga na Bayern Munich. Bayern ilikubali kulipa fidia kubwa kwa Leipzig ili kumruhusu kocha huyo kuondoka kabla ya kumaliza mkataba wake.
Ruben Amorim aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa Manchester United mnamo Novemba 2024, akitokea Sporting CP. Uhamisho huu ulifanyika baada ya makubaliano kati ya klabu hizo mbili, ambapo Manchester United ilikubali kulipa fidia ili kuvunja mkataba wa Amorim na Sporting.
Tangu awasili Amorim amekutana na changamoto kadhaa, ikiwamo majeraha ya wachezaji muhimu kama Lisandro MartÃnez atakayekuwa nje ya uwanja kwa miezi sita hadi minane kwa jeraha la goti.
Wengine ni Erik ten Hag na Graham Potter ni mifano ya makocha waliohanma klabu zao katikati ya msimu, wakitekeleza vipengele vya mikataba yao ili kujiunga na timu mpya.
Erik ten Hag: Mnamo Aprili 2022, Erik ten Hag alikubali kujiunga na Manchester United akitokea Ajax. Alikamilisha msimu na Ajax kabla ya kuanza rasmi majukumu yake na Manchester United msimu uliofuata. Hata hivyo, baada ya matokeo yasiyoridhisha, alifutwa kazi mnamo Oktoba 2024.
Graham Potter: Mnamo Septemba 2022, Graham Potter alihama Brighton & Hove Albion katikati ya msimu na kujiunga na Chelsea, akichukua nafasi ya Thomas Tuchel. Baada ya kipindi kifupi cha matokeo yasiyoridhisha, Potter alifutwa kazi mnamo Aprili 2023.
Mifano hiyo inaonyesha jinsi makocha wanavyoweza kuhama klabu katikati ya msimu kwa kufuata masharti ya mikataba yao kama vile kulipa fidia au kwa makubaliano ya pande zote mbili yaani mwajiri na mwajiriwa.
Mikataba ya makocha wa soka huundwa kwa namna inayowapa uhuru wa kuhama, mradi wanazingatia vipengele vilivyowekwa. Ingawa kuhama katikati ya msimu si jambo la kawaida, linawezekana endapo masharti ya mkataba yatatekelezwa ipasavyo, hivyo hata kwa Ramovic na Hamdi sio kitu kipya sana!