Kipigo chamzindua Mgunda | Mwanaspoti

KIPIGO cha mabao 2-1 ilichopewa Namungo kutoka kwa Tabora United, kimemuamsha Kocha Juma Mgunda aliyesema ameona mwanga ambao akirekebisha kidogo tu mambo yatakuwa matamu kwa Wauaji hao wa Kusini.

Namungo ilipokea kipigo hicho ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora huku ikitangulia kupata bao la mapema kupitia nahodha wake, Jacob Massawe kabla ya wenyeji kupindua meza na kuibuka na ushindi huo uliopoza machungu ya kufumuliwa 3-0 na Simba wikiendi iliyopita.

Akizungumzia mchezo huo uliochezwa kwenye uwanja uliotibuliwa na mvua kubwa iliyonyesha mjini humo, kocha Mgunda alisema licha ya kipigo, lakini amebaini kikosi cha Namungo kimeimarika, licha ya makosa madogo waliyoyafanya yamewagharimu.

“Kuna mabadiliko makubwa ukiondoa ushindi waliopata wapinzani wetu timu yangu ilikuwa bora kwenye maeneo mengi na imecheza mchezo mzuri, bahati haikuwa upande wao tutarudi uwanja wa mazoezi na kufanyia kazi,” alisema na kuongeza;

“Huu ni duru la lala salama ukiteleza kidogo unaadhibiwa nimeona mapungufu waliyoyafanya vijana wangu licha ya kucheza mchezo mzuri ugenini nitayafanyia kazi kabla ya mchezo ulio mbele yetu.”

Mgunda alisema bado wapo katika nafasi mbaya wanahitaji kupambana ili kujiondoa kwenye nyakati ngumu wanazopitia sasa huku akiweka wazi timu yao ina nafasi ya kufanya vizuri wakishikamana.

“Ukiangalia msimamo timu zimepishana poiti chache hivyo nikiiongoza Namungo kuishinda mechi mbili mfululizo naweza kupanda kwa nafasi nne hadi sita hivyo mipango thabiti ndio itaiondoa timu kwenye changamoto ya presha iliyonayo sasa.”

Kipigo hicho kimeiacha Namungo kubaki nafasi ya 12 katika msimamo ikicheza mechi 17, ikishinda michezo mitano, sare mbili na vipigo 10 imekusanya pointi 17 na timu hiyo inajiandaa kukabiliana na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.

Related Posts