Goma. Zikiwa zimepita siku mbili tangu waasi wa Kundi la M23 watangaze kusitisha mapigano dhidi ya vikosi vya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa kile walichotaja ni kuwepo janga la kibinadamu, waasi hao wameibuka na kuuteka mji wa Nyabibwe ulioko Jimbo la Kivu Kusini nchini humo.
Waasi wa M23, wanadaiwa kufadhiliwa na Serikali ya Rwanda, huku Rais wa Rwanda, Paul Kagame akikanusha madai hayo na kusema askari wa Jeshi la nchi yake (RDF) wako mipakani mwa DRC kwa lengo la kulinda mipaka yake na siyo kuwafadhiri waasi hao.
Shirika la Habari la Reuters limeripoti leo Februari 6, 2025, kuwa M23 wameibuka na kuushikilia Mji wa Nyabibwe ulioko kwenye ukingo wa Ziwa Kivu jimbo la Kivu Kusini nchini DRC.
Mji wa Nyabibwe uko takriban Kilometa 70 kutoka Mji wa Bukavu, mji ambao awali waasi hao walitangaza kuwa hawana nia ya kuuteka na kuuweka chini ya usimamizi wao.
Vyanzo nane vya habari wakiwemo wafanyakazi wa Mashirika ya Kuhudumia Jamii eneo la Nyabibwe wamethibitisha mji huo kutwaliwa na waasi wa M23.
“Kulikuwa na mapigano makali kuanzia saa 11:00 jioni (jana) na ilikuwa mida ya saa 3:00 usiku mji wa Nyabibwe ulipoangukia mikononi mwa waasi. Sasa tunavyozungumza wako katikati ya mji,” amesema kiongozi wa shirika moja ka kuhudumia umma linalofanya shughuli zake Jimbo la Kivu Kusini nchini DRC.
Nyabibwe, ni mji wa Kivu Kusini ni maarufu kwa uzalishaji wa madini ikiwemo dhahabu, coltan na aina nyinginezo huku ukiwa mji maarufu unaounganisha Mji wa Goma Jimbo la Kivu Kaskasini na Bukavu jimbo la Kivu Kusini.
Waziri wa Mawasiliano wa DRC, Patrick Muyaya alilieleza Shirika la Reuters kuwa waasi hao wamekiuka masharti ya kusitisha mapigano na kuwa wamekuwa wakikumbana na upinzani mkubwa kutoka vikosi vya Jeshi la Serikali vya FARDC.
Hata hivyo, Corneille Nangaa, ambaye ni kiongozi wa umoja wa makundi ya waasi ikiwemo M23, amethibitisha wapiganaji wake kuuzingira mji wa Nyabibwe.
“Walitushambulia ila tulijibu mapigo na kujilinda tusidhurike,” Nangaa alilieleza Shirika la Reuters.
Kutokana na uvamizi huo, Waasi wa M23, huenda wakarejesha uvamizi na malengo yao ya kuuchukua Mji wa Bukavu baada ya kuuteka Mji wa Goma ulioko Mashariki mwa DRC.
Tayari Mahakama ya Kijeshi ya DRC, imetoa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa kiongozi wa waasi wa M23, Corneille Nangaa, jana Jumanne, ikimtuhumu kwa uhalifu wa kivita na kufanya mapinduzi ya Serikali.
Baada waasi wa M23 kuyateka maeneo ya mashariki mwa DRC ikiwemo Goma, maelfu ya raia walianza kuyakimbia makazi yao kuvuka mipaka kuingia nchini Rwanda huku wengine wakikimbilia kwenye kambi za wakimbizi zilizoko nchini humo.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mapigano kati ya waasi na FARDC, yameleta madhara kwa binadamu katika Mji wa Goma sambamba na kuleta uharibifu wa miundombinu ikiwemo makazi na nishati.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya kibinadamu inakadiria kuwa hadi kufikia jana Jumatano Februari 5, 2025, mapigano hayo yamesababisha vifo zaidi ya 2,800 katika mji wa Goma nchini humo.
Pia, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilitoa taarifa kuwa inafuatilia kwa ukaribu yanayoendelea nchini DRC huku ikidai imeanza kufuatilia uwezekano wa kuwepo uhalifu wa kivita eneo hilo.
Kwa upande wao, Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundi nayo ilidai kuwa jengo lake lilivamiwa katika mji wa Goma na watu wanaohisiwa kuwa waasi na kwamba uharibifu uliofanyika utaichukua miezi kadhaa kulirejesha katika hali yake.
Hata hivyo, kiongozi wa kiroho katika Mji wa Goma, Willy Ngumbi amesema kuwa mapigano hayo yalisababisha uharibifu kwenye wodi ya wazazi baada ya kurushwa bomu ndani ya wodi hiyo.
Katika hatua nyingine, Bunge la nchi hiyo walikutana jana jijini Kinshasa kujadiliana mustakabali wa mapigano hayo kuelekea mkutano wa viongozi wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika unaotarajiwa kuanza kesho Februari 7, 2025 jijini Dar es Salaam.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.