Maandalizi teknolojia mpya matibabu ya selimundu yaanza

Dodoma. Serikali imesema imeanza maandalizi ya wataalamu na teknolojia mpya ya matibabu ya ugonjwa wa selimundu kwa kutumia teknolojia ya CRISPR Cas 9 (Gene Editing).

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Februari 6, 2025, na Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kawe (CCM), Josephat Gwajima, kuhusu lini serikali itaanza matibabu ya selimundu kwa kutumia teknolojia hiyo.

Dk Mollel amesema Serikali inafuatilia na kutathmini maendeleo ya teknolojia bora duniani, ikiwemo ya CRISPR Cas 9, ambayo imeanza kutumika duniani.

Amesema wakati wa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Marekani mwaka 2022 na ile ya mwaka 2024, suala hilo lilifuatiliwa kwa karibu. Pia, katika mkutano wa Umoja wa Mataifa, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alimwakilisha Rais Samia, ajenda hiyo ilijadiliwa katika mikutano na taasisi za tiba na teknolojia za Kimarekani, huku baadhi ya wagonjwa waliopokea matibabu kupitia teknolojia hiyo walishiriki.

“Mara tu teknolojia hii itakapotangazwa rasmi kama tiba duniani kote, Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi za kwanza kuipokea, kwa sababu tumeanza maandalizi tangu mwaka 2022,” amesema Dk Mollel.

Kwa sasa tiba inayotolewa kwa wagonjwa wa selimundu nchini ni ya upandikizaji wa uloto, matibabu hayo yanapatikana katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo jijini Dodoma.

Katika swali la nyongeza, Mbunge Gwajima alihoji ni kwa namna gani serikali itahakikisha usalama wa wagonjwa dhidi ya uwezekano wa kuharibiwa kwa vigezo vya msingi vya utu wao, kama rangi ya macho, ngozi, nywele au akili, kupitia teknolojia ya gene editing.

Dk Mollel alisisitiza kuwa ni muhimu kuweka sheria za kulinda wananchi dhidi ya matumizi mabaya ya teknolojia hiyo.

“Mabadiliko ya vinasaba yanaweza kurithiwa kizazi hadi kizazi, hivyo ni lazima kuwepo na uangalizi wa kina ili kuhakikisha usalama wa wananchi,” amesema Dk Mollel.

Related Posts