Hatimaye sakata la wachezaji watatu nyota wa timu ya Singida Black Stars (SBS) kupewa uraia wa Tanzania, limetinga kortini.
Wakili Peter Madeleka amefungua kesi ya kikatiba akidai utoaji huo wa uraia ulikiuka Katiba ya Tanzania.
Kesi hiyo ya kikatiba imesajiliwa Mahakama Kuu Masjala ya Dodoma na kupewa namba 2729/2025 na Jaji Evaristo Longopa ndiye ataisikiliza kwa tarehe itakayotajwa kupitia wito wa mahakama.
Wakili Madeleka alipotafutwa na Mwananchi leo Alhamisi Februari 6, 2025 azungumzie hilo, amekiri kufungua kesi hiyo ya Kikatiba na alipoulizwa kama wadaiwa wamejulishwa amesema; “Summons zitatolewa siku chache zijazo kupitia ofisi ya Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dodoma.”
Wachezaji waliopewa uraia wa Tanzania kwa tajnisi na kuibua minong’ono ni pamoja na Emmanuel Keyekeh ambaye ni raia wa Ghana, Josephat Bada wa Cote d’Ivoire na Muhamed Camara, raia wa Guinea.
Katika kesi hiyo aliyoifungua jana Jumatano Februari 5, 2025, Madeleka pamoja na mambo mengine, anaiomba Mahakama itoe amri raia hao kulipa fidia ya adhabu ya Sh200 milioni kutokana na matendo yao yaliyokiuka Katiba.
Pia anaiomba mahakama itamke kuwa wachezaji hao hawana sifa za kupewa uraia, kwamba Waziri wa Mambo ya Ndani, Kamishina Jenerali wa Uhamiaji (CGI) na wachezaji hao walishiriki kugushi na kutenda jinai, ili kuwapatia wachezaji hao uraia huo.
Katika kesi hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ameshtakiwa kama mdaiwa wa kwanza, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji mdaiwa wa pili na mwanasheria mkuu wa Serikali (AG) akiunganishwa kama mdaiwa wa tatu.
Wengine waliounganishwa ni wachezaji hao kama wajibu maombi wa nne, tano na sita huku mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) akiunganishwa kama mdaiwa wa saba na Mkurugenzi wa Huduma za Uhamiaji akiunganishwa kama mdaiwa wa nane.
Taarifa za raia hao wa kigeni kupewa uraia zilianza kujadiliwa katika mitandao ya kijamii na baadaye kuchapishwa katika vyombo vya habari kabla ya Januari 23, 2025 Idara ya Uhamiaji kujitokeza kufafanua jambo hilo.
Katika taarifa yake kwa umma iliyotiwa saini na Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji (SSI), Paul Msele, alisema wachezaji hao waliomba na kupewa uraia chini ya vifungu namba 9 na 23 vya Sheria ya uraia wa Tanzania, sura ya 357.
Hoja za Madeleka
Katika shauri hilo, Madeleka akiwakilishwa na Wakili John Seka anadai kati ya Juni 24 na Januari 23, 2025, wachezaji hao wakiwa raia wa kigeni, waliwasilisha kwa CGI na mkurugenzi huduma za uhamiaji, ombi la kupatia uraia.
Ili kuunga mkono maombi yao, waliwasilisha wachezaji waliwasilisha hati zao za kusafiria na vibali vya kufanya kazi nchini kwa ajili ya kupitiwa na kuhakikiwa na CGI na Mkurugenzi wa huduma za uhamiaji.
Baada ya kupitiwa, katika taarifa isiyofahamika, Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye ndio mdaiwa wa kwanza, CGI na Mkurugenzi wa Huduma za Uhamiaji, waliyakubali maombi ya wachezaji hao na kuwapa uraia wa Tanzania kwa tajnisi.
Wakili Madeleka anadai kuwa wadaiwa walipopelekewa nyaraka kwa ajili ya uhakiki, walipaswa wazingatie kuwa wachezaji hao hawakuwa wameishi nchini mfululizo kwa kipindi cha miezi 12 kabla ya siku ya kuwasilisha maombi yao.
Kwamba Waziri, CGI na Mkurugenzi wa Huduma za Uhamiaji wafahamu kuwa wachezaji hao hawakuwa wameishi nchini katika kipindi cha miaka isiyopungua saba na pia hawana ufahamu wa kutosha wa lugha ya Kiswahili au Kiingereza.
Mbali na kutokuwa na ufahamu wa kutosha wa lugha hizo mbili, Madeleka amedai maombi ya wachezaji hao hayakuchapishwa katika gazeti linalosomwa zaidi na taarifa walizoziwasilisha uhamiaji zina maudhui ya uongo au ya kutia shaka.
Pamoja na dosari zote hizo, Madeleka anadai bado Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi aliidhinisha wapewe uraia na kwamba tangazo la Idara ya Uhamiaji, lilitaka kuonyesha kuwa waziri ana kinga ya kutoheshimu Katiba na sheria za nchi.
Amedai kuwa DPP anayo mamlaka ya kikatiba na kisheria ya kuanzisha uchunguzi wa kubaini viashiria vyovyote vya jinai katika kupata au kushughulikia wachezaji hao kupata uraia wa Tanzania, licha ya dosari ambazo anadai zilikuwa za wazi.
Madeleka anadai kuwa AG kama mshauri mkuu wa sheria wa Serikali ana mamlaka ya kuishauri taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na hata Rais, kuchunguza kama kulikuwepo njama za kufanikisha suala hilo.
Kiapo cha Madeleka
Katika kiapo chake, Wakili Madeleka ameeleza kuwa yeye ni wakili wa mahakama ya Tanzania na mtetezi mshauri wa haki za binadamu na kutokana na sifa hizo, anaamini ni wajibu wake wa kikatiba kulinda haki zake na za raia wengine.
Mbali na kuwa mtetezi wa haki za binadamu kwa muda mrefu, yeye pia ni shabiki wa mpira wa miguu na yuko makini kufuatilia ligi kuu Tanzania ikiwamo ‘misuli’ ya ajabu ya kifedha ya Singida Black Star hadi kuweza kununua wachezaji wa kigeni.
“Kama nilivyojieleza ushiriki wangu katika utetezi wa haki za binadamu na utawala wa sheria, kitendo walichokifanya wadaiwa kimeniathiri mimi binafsi na nafsi inaniambia kilichofanyika sio sawa na utoaji wa uraia ulifanyika kimakosa.”
“Kwa kutegemea kinachoweza kutokea kutokana na shauri hili, sifa yangu itaathiriwa vyema au vibaya kwa vile kwa msimamo huu wa hadharani na nimenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa nimefanya vibaya.”
Nini anachokiomba Madeleka
Wakili Madeleka anaiomba mahakama itamke kuwa kinga aliyopewa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia kifungu cha 23 cha sheria ya uraia, hakiendi mbali kiasi cha kufikia hatua ya kukiuka Katiba na kifungu cha 9 cha sheria ya uraia.
Mbali na hilo, anaiomba Mahakama itamke, kwa kupendekeza wachezaji hao wapewe uraia, CGI ambaye ni mdaiwa wa pili na mkurugenzi wa huduma za uhamiaji ambaye ni mdaiwa wa 8, walikiuka Katiba ya nchi na sheria ya uraia.
Halikadhalika, anaiomba mahakama itamke kuwa kwa kuwapa uraia wachezaji hao ambao ni wadaiwa wa 4,5 na 6, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alikiuka ibara ya 26(2) ya Katiba ya nchi na kifungu cha 9(1) cha sheria ya uraia Tanzania.
Ukiacha hayo, anaiomba Mahakama itamke kuwa wachezaji hao hawana sifa ya kupewa uraia na kwamba, Waziri wa Mambo ya Ndani, CGI na wachezaji kwa pamoja walishiriki kugushi au kutoa uraia katika mazingira yasiyokubalika.
Hivyo, anaiomba Mahakama itoe amri kwa Waziri wa Mambo ya Ndani na CGI kutaifisha mara moja vyeti vya uraia walivyopewa wachezaji hao au iwaamuru kuvisalimisha kwa msajili wa mahakama wakati hukumu ikisubiriwa.
Wakili huyo anaiomba Mahakama imwamuru AG kama mshauri mkuu wa Serikali, kuchukua hatua stahiki zitakazowezesha ‘kumulikwa’ kwa waziri wa mambo ya ndani, CGI na mkurugenzi wa uhamiaji na waliko chini yao.
Anaiomba mahakama kumwagiza DPP kuanzisha uchunguzi kuhusiana na vitendo na ushiriki wa Waziri wa Mambo ya Ndani, CGI, wachezaji hao na Mkurugenzi wa Huduma za Uhamiaji kuona kama jinai yoyote ilitendeka na kuchukua hatua.
Madeleka hakuishia hapo, bali anaiomba mahakama itoe amri kwa waziri, CGI na mkurugenzi wa huduma za uhamiaji kulipa Sh500 milioni kama fidia ya adhabu kwa matendo yao ambayo hayakuzingatia Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.
Mdai huyo ameomba pia mahakama iwaamuru wachezaji hao nao kulipa Sh200 milioni kama fidia ya adhabu ya kufanya matendo yanayokiuka Katiba na pia wadaiwa walipe gharama za kesi na itoe amri yoyote inayoona inafaa.