Arusha. Kukosekana kielelezo kuhusu uzito wa bangi na nyaraka za ushahidi kusomwa kwa sauti ya chini kiasi cha mtuhumiwa kushindwa kusikia ni kasoro zilizoifanya Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Dar Es Salaam, kumuachia huru Ally Madenge, aliyekuwa akitumikia kifungo cha miaka 30 jela.
Madenge ambaye tayari ametumikia sehemu ya adhabu kwa kukaa jela kwa takriban miaka nane, alihukumiwa kifungo hicho Desemba 18, 2017 na Mahakama ya Wilaya ya Temeke katika kesi ya jinai namba 1100/2017, baada ya kukamatwa na bangi.
Uamuzi wa kumuachia huru Madenge ulitolewa Februari 3, 2025 na Jaji Elizabeth Mkwizu, aliyekuwa akisikiliza rufaa hiyo ya jinai namba 55 ya mwaka 2023.
Jaji Mkwizu alifikia uamuzi huo baada ya kubaini dosari ya kisheria katika mwenendo wa kesi hiyo.
Dosari iliyobainika ni kukosekana kwa taarifa muhimu, hasa uzito wa bangi inayodaiwa kupatikana kwa Madenge.
Kwa mujibu wa Jaji Mkwizu dosari nyingine ni kuwa vielelezo vya maandishi kikiwemo cheti cha ukamataji na fomu ya maabara, vilikubaliwa bila ya yaliyomo kusomwa kwa sauti mahakamani ili kumpa nafasi mshtakiwa kujua yaliyokuwa yameandikwa.
Alidai kuwa maelezo muhimu yalikosekana katika kesi iliyomkabili, hasa uzito wa bangi alizodaiwa kukutwa nazo, ambayo ni muhimu kwa kutathmini ukubwa wa kosa na hukumu inayofaa na kuwa Hakimu alishindwa kueleza ipasavyo vipengele muhimu vya shtaka na matokeo yanayoweza kusababishwa na hatia.
Sababu nyingine ni kuilaumu mahakama kwa kumtia hatiani kwa kesi ya dawa za kulevya ilhali hakuna bangi aliyodaiwa kukutwa nayo haikuwasilishwa mahakamani kama kielelezo.
Nyingine ni kuwa vielelezo vya maandishi kikiwemo cheti cha ukamataji na fomu ya maabara, vilikubaliwa bila ya yaliyomo kusomwa kwa sauti mahakamani ili kumpa nafasi mshtakiwa kujua yaliyokuwa yameandikwa.
Baada ya kusikiliza sababu za rufaa Jaji Mkwizu alisema mahakama kutokana na kumbukumbu za kesi hiyo kutokuonyesha kiasi cha bangi aliyokutwa nazo mrufani hiyo, huku hati ya kukamata na taarifa ya Mkemia Mkuu wa Serikali, kutokusomwa kwa sauti wakati kesi inasikilizwa, mrufani hakujua kilichokuwa kimeandikwa humo.
Amesema licha ya kuombwa na upande wa mashtaka kuwa aamuru kesi hiyo kusikilizwa upya, anaona kuamuru kusikilizwa upya kutaruhusu upande wa mashtaka kurekebisha kasoro zake kwa kutafuta ushahidi wa bangi, ambao unaweza usiwepo na kufanya kesi nzima kutokuwa na maana.
Awali katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Madenge alishtakiwa na kutiwa hatiani kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi isivyo halali kinyume na kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.
Baada ya kutoridhishwa na hukumu hiyo Madenge alikata rufa iliyokuwa na sababu saba za kupinga hukumu hiyo ikiwemo hakimu aliyesikiliza kesi hiyo alikosea kisheria kwa kumtia hatiani kulingana na ombi la hatia ambalo halikuwa ombi lisilo na shaka.
Alidai kuwa shtaka dhidi yake liliposomwa kwake, alirekodiwa kuwa alisema. “ni kweli nimekamatwa na bangi hiyo na kuwa hili halikuwa sahihi kwa sababu, katika kesi hiyo ya dawa za kulevya, alitakiwa kutaja wingi na uzito wa bangi anazodaiwa kukutwa nazo.
Mrufani huyo aliiomba mahakama hiyo kuruhusu rufaa, kufuta hukumu na kutengua adhabu iliyotolewa dhidi yake na kumwachia huru.
Upande wa mjibu rufaa, waliunga mkono rufaa hiyo akiegemea uamuzi wa rufaa ya jinai namba 14 ya mwaka 2020 ya Richard Lionga dhidi ya Jamhuri, na kusema upande wa mashtaka unabeba mzigo wa kueleza mshtakiwa kwa uwazi na ipasavyo mazingira ambayo kosa hilo lilitendeka na jinsi lilivyotendwa, kwa nyaraka na vielelezo vinavyohusika.
Amesema katika kesi hiyo dawa hizo za kulevya zilipaswa kutolewa mahakamani kama vielelezo, lakini haikutolewa kwa hiyo hakuna uhakika kama iliwahi kuwepo au na kuiomba mahakama hiyo kurejesha jalada hilo katika mahakama ya chini kwa ajili ya kusikilizwa tena.
Jaji Mkwizu amesema ili kumtia hatiani mshitakiwa ni muhimu ukweli kuhusu kesi ambayo inaunda vipengele vya kosa linaloshtakiwa vinapaswa kusomwa kwa maelezo ya kutosha kwa mshtakiwa kuhusu mambo yote yanayojumuisha kosa katika lugha ambayo anaweza kuelewa.
Amesema hakimu anapaswa kueleza kwa mshtakiwa vipengele vyote muhimu vya kosa linaloshtakiwa na iwapo mshtakiwa anakubali vipengele hivyo vyote muhimu, hakimu anapaswa kuandika maneno yote.
Jaji Mkwizu amesema hakimu anapaswa kumtaka mwendesha mashtaka aeleze ukweli wa kosa linalodaiwa na maelezo yanapokamilika, ampe nafasi mshtakiwa kubishana au kueleza ukweli.
Amesema ni jambo lisilopingika kuwa maelezo ya kosa hilo yaliyosomwa kwa mshtakiwa ambaye alionekana kuyakubali ila maelezo hayo yalikosa taarifa muhimu hasa uzito wa bangi inayodaiwa kupatikana kwa Madenge.
“Zaidi ya hayo, ukubwa wa kosa na bangi zilizoainishwa hazikujumuishwa kwenye rekodi za mahakama hiyo ya chini, hivyo kuzuia mahakama kuthibitisha kuwepo kwao,” amesema.
Jaji Mkwizu amesema wakati upande wa mashtaka ukifanya jitihada za kuwasilisha hati ya kukamata na taarifa ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuhusu mali iliyochukuliwa, nyaraka hizo hazikusomwa kwa sauti mahakamani, hivyo kumzuia mrufani kuelezwa kikamilifu kilichokuwamo.
“Rufaa ni kwa sababu iliyo hapo juu inaruhusiwa hatia na hukumu iliyotolewa dhidi ya mrufani zinabatilishwa, na mrufani aachiliwe kutoka gerezani isipokuwa awekwe humo kwa sababu nyingine halali,”amesema Jaji Mkwizu.