Majaliwa atoa kauli uamuzi wa Trump kusitisha misaada

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameeleza msimamo wa Serikali ya Tanzania kuhusu mabadiliko ya sera za misaada ya Marekani chini ya utawala wa Rais Donald Trump, akisisitiza kuwa Tanzania lazima ijikite katika kujitegemea kiuchumi.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo, Alhamisi Februari 6, 2025, Majaliwa amesema kuwa Marekani, kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa (Usaid), imesitisha baadhi ya misaada iliyokuwa ikitolewa kwa Tanzania na nchi nyingine zinazoendelea.                                                                          

Amesema kuwa mabadiliko hayo ni sehemu ya sera mpya za mambo ya nje za Marekani, ambazo zinaweza kuwa na athari kwa baadhi ya sekta nchini.

“Ni kweli kwamba Serikali yetu inaheshimu sera za mambo ya nje na tunatekeleza mikataba kwa mujibu wa makubaliano na nchi husika. Hata hivyo, tumeanza kuona mabadiliko katika sera za baadhi ya nchi zenye uwezo mkubwa kama Marekani na haya mabadiliko yanaweza kuathiri baadhi ya nchi ikiwemo Tanzania,” amesema Waziri Mkuu.

Pamoja na hilo, Majaliwa amesisitiza kuwa Tanzania imejipanga kuhakikisha kuwa uchumi wake unajitegemea ili kuepuka utegemezi wa misaada ya nje. Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuimarisha mahusiano ya kimataifa na kuhakikisha Tanzania inaendelea kushirikiana na mataifa mbalimbali duniani.

“Muhimu kwetu ni kuhakikisha tunajiimarisha ndani kwa kuongeza uwezo wetu wa ndani. Tunapaswa kuhakikisha mipango yetu ya maendeleo inatekelezwa kupitia bajeti zetu wenyewe, badala ya kutegemea misaada ya nje. Tunazo maliasili na rasilimali nyingi, na sasa ni jukumu letu kuzitumia kujenga uchumi wetu wa ndani ili kuwezesha utekelezaji wa miradi yetu ya maendeleo katika sekta mbalimbali kama afya, elimu na miundombinu,” ameongeza Majaliwa.

Amendelea kusema kuwa pamoja na hatua zilizochukuliwa na Marekani, Tanzania itaendelea kuimarisha uchumi wake kwa kutegemea vyanzo vya ndani vya mapato. Alitoa wito kwa Watanzania kushirikiana katika kutumia rasilimali zilizopo kwa ufanisi ili kuhakikisha maendeleo ya taifa yanaendelea kwa kasi.

“Hatuwezi kutegemea misaada milele, lazima tujiimarishe na kuwekeza katika vyanzo vyetu vya mapato. Ni lazima tuhakikishe mipango yetu ya bajeti inazingatia mahitaji yetu halisi ili kufidia pengo litakalotokana na mabadiliko haya ya sera za misaada kutoka mataifa yaliyoendelea,” amesema.

Waziri Mkuu amehitimisha kwa kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kupanga na kutekeleza mikakati madhubuti ya kukuza uchumi wa taifa ili Tanzania isitegemee sana misaada ya nje, hasa kutokana na mabadiliko ya sera za mataifa makubwa kama Marekani.

Related Posts