Dar es Salaam. Idara ya Uhamiaji Tanzania imetangaza majina ya vijana 331 waliochaguliwa kujiunga na mafunzo ya idara hiyo kuanzia Machi 1, 2025.
Tangazo la kuitwa kwenye mafunzo hayo limetolewa leo Alhamisi Februari 6, 2025 na Kamishna Jenerali wa idara hiyo.
“Kamishna Jenerali wa Uhamiaji anawatangazia vijana ambao wamechaguliwa kujiunga na Idara ya Uhamiaji kuripoti Chuo cha Uhamiaji cha Raphael Kubaga kilichopo Boma Kichakamiba, Wilaya ya Mkinga – Mkoani Tanga, Jumamosi Machi mosi 2025 kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana,” imeeleza taarifa hiyo.
Pia, kwa walioomba na kuchaguliwa kupitia Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, wanatakiwa kuripoti Afisi ya Uhamiaji Mkoa wa Kusini Unguja (Tunguu) Jumatatu Februari 24, 2025 saa 2:00 asubuhi.
Katika taarifa hiyo vijjana waliochaguliwa kujiunga na mafunzo hayo wametakiwa kuripoti wakiwa na vyeti halisi vya elimu na fani mbalimbali.
“Vyeti na nyaraka zinazotakiwa ni kama ifuatavyo: Cheti cha kuzaliwa, kitambulisho cha Taifa (Nida) au Namba ya Nida, vyeti halisi vya elimu ya kidato cha nne, cha sita na shahada na vyeti vya ujuzi wa aina mbalimbali (kwa wale wenye ujuzi),” imeeleza taarifa hiyo.
Kamishna Jenerali ameongeza kuwa, mwanafunzi anatakiwa kuripoti akiwa na fedha Sh50, 400 kwa ajili ya bima ya afya kwa asiyekuwa nayo na mwenye nayo ambayo inaisha uhai wake kabla ya Desemba 31, 2025 atatakiwa kwenda na Sh25, 000 kwa ajili ya vipimo vya afya.
“Pia kijana aje na fedha za kujikimu kwa ajili ya matumizi binafsi, Truck suit (2) rangi nyeusi na dark blue, raba za michezo jozi (2) rangi yoyote, Nguo nadhifu za kiraia jozi (3), mashuka (4) rangi ya bluu, mto wa kulalia (1), foronya (2) rangi ya bluu, chandarua (1) rangi ya bluu, madaftari makubwa (4) 4QRs, sanduku la chuma (Trunker) na ndoo (2) za plastiki (moja ya lita 10 na moja ya lita 20).
Mahitaji mengine ni “Fulana (2) rangi ya dark blue zenye shingo ya duara, viatu vya mvua (rainboot,) jozi (1), taulo (1), kandambili jozi (1) pamoja na vifaa vya usafi ikiwemo jembe (1) na mpini wake, fyekeo (01), panga (01) na reki (1),”imeeleza taarifa hiyo.
Pia, gharama za usafiri kutoka nyumbani kwenda chuoni zitagharamiwa na mwanafunzi mwenyewe na waliochaguliwa kujiunga na mafunzo watafanyiwa uchunguzi wa afya kabla ya kuanza mafunzo, na wale wote watakaobainika kuwa na changamoto za kiafya hawataruhusiwa kujiunga na chuo.