Mauya: Uzoefu mdogo umetuponza | Mwanaspoti

KIUNGO wa KenGold, Zawadi Mauya amesema kucheza na timu kongwe kama Yanga inahitaji ukomavu wa akili na uzoefu wa kutosha wa kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi, kitu ambacho juzi hawakuwa nacho na kujikuta wakifumuliwa mabao 6-1 kwenye Uwanja wa KMC Complex.

KenGold iliyofanya usajili wa kishindo dirisha dogo ilifungwa mabao hayo ukiwa ni mchezo wa raundi ya 17 wa Ligi Kuu Bara, huku sehemu kubwa ya mastaa waliosajiliwa na timu hiyo ya Mbeya wakikosekana kwenye mchezo huo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mauya ambaye ni nahodha wa timu hiyo, alisema walifungwa na Yanga kutokana na wachezaji wengi walioanza kukosa uzoefu wa kutosha kulinganisha na wenyeji ambao karibu wote ni wazoefu na wanaocheza timu za taifa.

Mauya alisema katika mchezo wa juzi wachezaji wazoefu katika kikosi hicho walikuwa wachache, jambo lililowawia vigumu kupata matokeo ya ushindi na kufungwa mabao mengi.

“Ndiyo maana katika mchezo huo nilionekana katika maeneo mengi, lengo ilikuwa ni kuhakikisha naziba baadhi ya mianya ya kushambuliwa zaidi,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa Kagera Sugar, Yanga na Singida Black Stars.

Katika mchezo huo wa juzi, Mauya pekee ndiye aliyekuwa mchezaji mzoefu wa Ligi Kuu kulinganisha na wenzake wenye uzoefu wa Ligi ya Championship na ni wachezaji wanne wapya akiwamo yeye waliosajili dirisha dogo walioanza kabla ya wengine akiwamo Seleman Bwenzi kuingia kipindi cha pili na kufunga.

Wachezaji wengine wazoefu wa Ligi Kuu kwa upande wa KenGold kwa juzi ni moja na James Msuva na Abdallah Masoud ‘Cabaye’, tofauti ya Yanga ambayo kuanzia kipa Diarra Djigui hadi mabeki, viungo na washambuliaji asilimia kubwa ni wachezaji wa timu za taifa na kufanya mchezo kuwa wa upande mmoja tofauti na mechi ya kwanza iliyopigwa mwaka jana na Yanga kushinda bao 1-0, huku KenGold wakiupiga mpira mwingi.

Katika mchezo huo Yanga ilianza na Diarra, Israel Mwenda, Chadrack Boka, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Khalid Aucho, Clement Mzize, Mudathir Yahya, Prince Dube, Staphane Aziz Ki na Pacome Zouzoua, ambao asilimia kubwa ni nyota wa timu za taifa wa nchi za Mali, Tanzania, Uganda, Burkina Faso na Zimbabwe.

Mauya alisema timu hiyo ilisajili wachezaji wengi wazoefu dirisha dogo akiwamo Bernard Morrison, Obrey Chirwa na wengine ambao hawajatumika katika mchezo huo, huku akiamini wangekuwepo huenda Yanga wasingepata idadi kubwa ya mabao.

“Soka la kisasa linahitaji kasi, nguvu na akili kwa pamoja, kuna sehemu yanahitajika maarifa kuamua cha kufanya badala ya nguvu, hiyo inahitaji mchezaji mkomavu ama kikosi kikiwa na mchanganyiko wa damu changa na wakongwe kinakuwa na ubora zaidi,” alisema Mauya na kuongeza;

“Tuna kazi ya kufanya kutokana na nafasi iliyopo KenGold, ndiyo maana nasema ukomavu na maarifa ni muhimu katika harakati zetu za kuhakikisha haishuki daraja.”

Timu hiyo iliyopanda Ligi Kuu msimu huu kutoka Ligi ya Championship, inaendelea kubaki mkiani ikiwa na pointi sita baada ya mechi 17, ikifungwa mabao 35 na kufunga 12 tu, wakati Yanga imefikisha alama 45 kwa idadi ya mechi kama hizo ikijiweka pazuri kutetea ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo.

Related Posts