Dodoma. Mawaziri wameshambulia kujibu hoja za wabunge, huku Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo akitaja mikakati ya kutatua changamoto ya ajali nchini.
Hoja hizo zilitolewa na wabunge wakati wakiwasilisha na kuchangia taarifa za kamati za Kudumu za Viwanda, Biashara, Kilimo, Uvuvi na Mifugo na ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama leo Alhamisi Februari 5, 2025.
Akijibu hoja hizo, Sillo amesema Jeshi la Polisi lina mikakati katika kupambana na ajali za barabarani ikiwemo kufanya marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani na wako katika hatua za mwisho kwa kupata maoni ya wadau ili iweze kuendana na wakati.
Amesema jambo jingine ni usimikaji wa kamera za kisasa 9,500 ambapo kwa kuanzia tutasimika katika majiji ya Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza na Arusha na mikoa mingine itafutia.
“Jambo la tatu ni ukaguzi wa lazima wa magari, mradi huu karibia unaanza katika hili kukagua magari yote yanayoingia nchini na yanayotumika nchini kuangalia kama inafaa katika kuzuia ajali,” amesema.
Amesema jambo jingine ni kutoa elimu kwa umma na wanafunzi shuleni na sokoni na maeneo mbalimbali.
Sillo amesema wamepewa fedha na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kununua vifaa ambapo wamenunua magari 50 kwa ajili magari ya wakuu wa wilaya wa polisi na Februari mwaka huu wanapokea magari 122 kwa ajili ya waliobakia.
Amewahakikishia wabunge kuwa maazimio yote tisa yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama wameyachukua kwa ajili ya utekelezaji.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo amesema mradi wa Mchuchuma na Liganga ameusikia tangu alipoingia bungeni mwaka 2010 lakini sasa chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha utofauti mkubwa ambapo zaidi ya Sh15 bilioni zimetolewa kwa wananchi.
“Mradi huu unaenda vizuri na si muda mrefu kwa mwaka huu wa fedha tunaondoka nao Imani yetu kwa mara ya kwanza inaweza Tanzania tunakwenda kuzalisha chuma ambayo ni maligjhafi muhimu sana katika maendeleo ya viwanda,” amesema.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Serikali iliwapa watu mashamba, wakayaacha bila kuyaendeleza yakawa mapori na wengine waliyakopea fedha benki.
“Tumewapa watu mashamba hawayayatumii, viwanda wameviua, timu yetu ya udhamini imeshamaliza kazi yake wametuletea draft ya kwanza, hawa wawekezaji wanayo commitment (ahadi) ya mikataba ambayo kama hawataitekeleza,” amesema.
“Tumefanya tathimini ya thamani ya mashamba na hali ya viwanda walivyovitekeleza, tutayachukua kwa mujibu wa sheria na kuwagawia wakulima wadogo. Niwaombe ni tuwe na subira, ni suala la muda tusije tukaonekana ni Taifa lisilofuata sheria,” amesema.