MCHENGEWA ANG’AKA NA WAKANDARASI WASIOMALIZA KAZI NDANI YA MUDA WA MKATABA.

Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma

Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Mohammed Mchengerwa amewataka Wakurugenzi wote wa Majiji hasa Jiji la Dodoma ambako ndio makao makuu ya Nchi kujipanga vizuri katika kuwapokea watu wanaoingia na kutoka katika Majiji hasa katika eneo la Stesheni ya Reli kwa Jiji la Dodoma kwani utaratibu haujakaa vizuri kwa Watanzania wanaoingia na kutoka hivyo utaratibu uendane na uwekezaji uliofanywa na Serikali.

Mchengerwa ameyasema hayo leo hii Jijini Dodoma Februari 6,2025 katika hafla ya Utiaji Saini Mkataba wa Ujenzi wa soko kuu la Majengo pamoja na ujenzi wa kituo cha daladala eneo la Mshikamano, Kizota na Nzuguni.

Na kumuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Mkuu wa Wilaya kujipanga vizuri katika eneo hilo kwa kufanya mazungumzo na Wizara ya Uchukuzi na Tarula ili kuweka utaratibu mzuri kuendana na hadhi ya Jiji.

“Maelekezo yangu kwa Wakurugenzi wa Majiji ninawataka wote wa Mjiji lakini hasa Jiji la Dodoma ambapo ndio makao makuu ya Nchi,Mkuu wa mkoa na Mkuu wa Wilaya nendeni mkajipange hasa pale kwenye lile eneo la Stesheni ua reli utaratibu wa watu kuingia na kutoka haujakaa vizuri nenndeni mkakae na TRC muweke utaratibu mzuri”.

“Ninyi na Tarula mkajipange vizuri mzungumze na Wizara ya uchukuzi kuweka utaratibu Watanzania wanaokwenda na kurudi waweze kuingia na kupita lile kwa utaratibu mzuri”.

Aidha Nchengerwa Amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara mijini na Vijijini (TARURA) kutowapa kazi Wakandarasi wote ambao wamekuwa wakisusua katika ukamilishaji wa kazi zao hasa wale waliopaswa kukamilisha Mikataba yao ndani ya mwezi Februari lakini bado wako chini ya asilimia hata 50, kuwa wasipewe kazi yeyote chini ya Tarura hata kama wametoka Kampuni za ndani au nje ya Nchi mpaka pale watakapo kamilisha miradi hiyo.

“Sasa maelekezo yangu Wakandarasi wanaochelesha miradi wasiruhusiwe kupewa kazi kokote ndani ya ndani ya Tarura na ninaomba mniletee tathmini ya maeneo mengine yote ambayo miradi ilipaswa kukamilika mwezi Februari na haijakamilika”.

“Hatuwezi kuwa na watu ambao hawawazi fikra za Rais wetu,anatafuta fedha na kuleta lakini bado wanakuwa goigoi,hatuwezi kukubali hata kidogo”.

Akitoa salamu za shukurani kwa niaba ya wakazi wa Dodoma Mbunge wa Dodoma mjini Mhe Anthony Mavunde ameishukuru Serikali kwa kazi kubwa ambayo imefanyika na kusema katika Halmashauri zote nchini, Halmashauri ya Jiji la Dodoma ndio inayoongoza kwa mtandao mtefu wa barabara za kiwango cha lami kwani Jiji lina kilomita 249.12 ikifuatiwa na Halmashauri ya Kinondoni ambayo ina Barabara yenye urefu wa kilomita 223 ambayo imefanya Dodoma kuwa Kinara.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema Dodoma imekuwa ikifanya vizuri katika usimamizi wa miradi na kumuahidi Waziri kuwa atasimamia kwa umakini mkubwa miradi hii na kuhakikisha miradi inakamilika vizuri kwa ubora na kwa wakati kwani miradi hii inaipa heshima Jiji na Mkoa wa Dodoma kwa ujumla.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Mijini na vijini Mhandisi Victor Seff amesema malengo makuu ya mradi huu wa Tactic ni kuboresha usimamizi wa ukuaji wa miji pamoja na kuziwezesha Halmashauri za miji na majiji kutoa huduma bora kwa wananchi na kuongeza mradi huu unahusisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali zikiwemo Barabara na miundombinu mengine kulingana na kipaumbele cha Halmashauri.


Related Posts