Durban. Duduzile Zuma-Sambudla, binti wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, amefikishwa mahakamani leo Alhamisi Februari 6, 2025 baada ya kushtakiwa kwa kuchochea vurugu wakati wa ghasia za mwaka 2021 ambapo zaidi ya watu 300 waliuawa.
Wakili wa Zuma-Sambudla amesema amekana mashitaka hayo.
Waendesha mashtaka wanadai kuwa Zuma-Sambudla alichochea watu wengine kufanya vurugu katika machapisho kwenye mitandao ya kijamii Julai 2021 wakati machafuko yalipozuka baada ya baba yake kukamatwa kwa kutotii amri ya Mahakama ya kutoa ushahidi katika uchunguzi wa ufisadi.
Ilianza kama hasira ya kufungwa kwa Zuma, ikageuka kuwa hasira ya kupinga umaskini na ukosefu wa usawa na kusababisha uporaji wa maelfu ya maduka, uharibifu mkubwa wa miundombinu ya umma na vifo vya takriban watu 350.
Uharibifu uliotokana na ghasia hizo unakadiriwa kuwa takribani Dola za Marekani 2.7 bilioni (Sh6.9 trilioni).
Jacob Zuma aliandamana na mwanaye, Zuma-Sambudla hadi Mahakama ya Durban. Hata hivyo, imeelezwa kuwa ameachiliwa kwa onyo hadi kesi nyingine ya Mahakama itakapopangwa Machi 2025.
Baada ya hukumu yake ya kudharau Mahakama kumalizika mwaka 2022, Zuma alikiunga mkono chama kipya cha siasa cha uMkhonto we Sizwe (MK), ambacho kilileta ushindani mkubwa katika uchaguzi wa kitaifa wa mwaka 2024.
MK ilishinda viti 58 vya ubunge na hivyo kuchangia kupungua kwa kasi kwa uungwaji mkono wa chama cha African National Congress (ANC) ambacho Zuma alikuwa akikiongoza.
ANC ililazimishwa kuingia katika muungano na vyama vingine vidogo.
Zuma-Sambudla ni mmoja wa wabunge wa MK katika Bunge dogo la nchi hiyo.
Mwaka 2021, Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini iliagiza Zuma afungwe jela kwa kukataa kutoa ushahidi katika uchunguzi wa ufisadi uliofanyika katika kipindi chake cha uongozi kutoka 2009 hadi 2018.
Zuma (82), alikanusha kuhusika na ufisadi na alisema kuwa ni mwathirika wa njama za kisiasa. Alijikabidhi kwa polisi siku kadhaa baadaye na kupelekwa katika gereza lililo karibu na nyumbani kwake katika jimbo la KwaZulu Natal.
Hukumu dhidi ya Zuma ambayo ni ya kwanza dhidi ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, ilizua mtafaruku wa kisheria na kufuatiwa na maandamano makubwa ya wafuasi na watetezi wa mwanasiasa huyo.
Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini alilazimika kujiuzulu Februari 2018 kutokana na shinikizo la chama tawala cha ANC kwa tuhuma za kuhusika na ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka yake.