Kahama. Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Chona kwenye Halmashauri ya Ushetu Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Pendo Williamu (16) amefariki dunia, huku wenzake watatu wakijeruhiwa baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba waliyokuwa wamepanga.
Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kahama, Stanley Luhwago amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia Februari 5, 2025 akieleza mwanafunzi huyo alifariki dunia papo hapo.
Akizungumza kwa simu leo Alhamisi Februari 6, 2025, Luhwago amesema chanzo ni ukuta wa chumba walichokuwa wanaishi wananfunzi hao wakike kutokuwa imara na baada ya kunyeshewa na mvua usiku huo ndipo ulipoanguka kwa ndani ya chumba hicho na kusababisha athari hizo.
“Ni kweli kabisa sisi kama Jeshi la Zimamoto na Uokoaji tulipata taarifa ya wanafunzi wanne wa shule ya sekondari Chona kwamba wamedondokewa na ukuta wa nyumba kwa hivyo mara moja tulifika eneo la tukio na kukuta kweli tukio hilo limetokea likihusisha wanafunzi wanne wa jinsi ya kike wote wa Shule ya Sekondari Chona,” amesema Luhwago.
Mkuu wa Shule hiyo, Lucy Kibela amesema wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo ambao wanatoka umbali mrefu wanalazimika kupanga vyumba jirani na shule (mageto), lakini kutokana na uwezo mdogo wa wazazi huwapangishia watoto wao nyumba za bei rahisi ambazo sio imara.
Amesema alipata taarifa ya maafa hayo saa 7 usiku wa Februari 5, 2025 ambapo Sharida Shija (15) kidato cha kwanza, Neema Shija (16) kidato cha tatu na Regina Eliasi (16) kidato cha tatu walijeruhiwa maeneo mbalimbali ya miili yao baada ya kuangukiwa na ukuta huo.
Amesema lengo la wazazi hao kuwapangia ni kuwaepusha watoto wao na changamoto wanazokutana nazo wakati wa kwenda na kurudi shuleni, ikiwemo ubakaji.
“Wanafunzi watatu walijeruhiwa na hali zao zinaendelea vizuri na wameruhusiwa kurejea shuleni, lakini suluhisho la janga hili ni kukamilishwa kwa ujenzi wa bweni la wanafunzi unao endelea hapa shuleni,” amesema Lucy.
Ameongeza,“Kuna ujenzi wa bweni la wanafunzi lenye uwezo wa kubeba wanafunzi wa kike 80 na limejengwa kwa nguvu za wananchi, sasa lipo hatua ya lenta. Tunaomba Serikali kuangalia namna ya kulikamilisha ili litumike na kuwasaidia wanafunzi kuondokana na changamoto za magetoni,”
Hatahivyo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita ametoa muda wa wiki moja kwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Hadija Kabojela kuhakikisha wanapitia na kukagua mageto yote ya wanafunzi na kuhakikisha yapo salama, iwapo si salama wawahamishe mara moja na kuwatafutia maeneo salama wakati jitihada za ukamilishaji wa mabweni ukiendelea.
Mboni aliyekuwa akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Ushetu kilichofanyika leo amesema, “Nyumba nyingi zimejengwa katika mfumo ambao mvua ikinyesha kwa saa 24 inamomonyoka inaanguka kwa sababu nyingi wameweka plasta kwa nje lakini ndani ni udongo ambazo kwa namna moja ama nyingine zinaendelea kuleta maafa”