Timu za Prisons na Pamba Jiji zimeanza vizuri ngwe ya lala salama ya Ligi Kuu Bara baada ya kupata ushindi mchana kwenye viwanja viwili tofauti.
Prisons ilikuwa nyumbani jijini hapa na kushinda mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa, wakati Pamba ikiwa ugenini iliinyoa Dodoma Jiji kwa bao 1-0 na kuongeza kibubu cha pointi walizonazo katika Ligi Kuu.
Bao la dakika ya 88 lililofungwa na Meshack Abraham limeihakikishia Prisons kubaki na pointi tatu nyumbani dhidi ya Mashujaa katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa leo Februari 6, 2025 Uwanja wa Sokoine jijini hapa.
Abraham aliingia kutokea benchi akichukua nafasi Abdulkarim Segeja ambaye amebadili mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Nasorro Mwinchui kutoka Tanga na kuibuka mchezaji bora wa mechi hiyo.
Prisons walitangulia kupata bao kupitia Beno Ngassa dakika ya tatu, huku Mashujaa wakisawazisha dakika ya 28 kwa penalti ikiwekwa wavuni na Seif Karihe.
Dakika ya 32, Kipa wa Prisons, Mussa Mbisa alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia na nafasi yake kuzibwa na Sebusebu Samson ambaye alionesha uimara kwa kuokoa hatari kadhaa.
Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa kocha Aman Josiah kuiongoza Prisons akichukua mikoba ya mtangulizi, Mbwana Makata ambaye alisitishiwa mkakataba baada ya matokeo kutokuwa mazuri.
Kocha Mkuu wa Mashujaa, Abdalah Mohamed ‘Baresi’ amesema alihitaji ushindi katika mechi hiyo, lakini anakubali kilichotokea akieleza upinzani ulikuwa mkali kwa timu pinzani.
Amesema mabao mawili waliyoruhusu ni makosa na uzembe wa mabeki wake akieleza kuwa bado hawajapoteza malengo badala yake wanakwenda kusahihisha makosa katika michezo ijayo kuweza kufanya vizuri.
“Tulitarajia ushindi lakini tumekutana na ugumu, tumeruhusu mabao mepesi sana kwa makosa na uzembe wa mabeki, tutaenda kufanyia kazi kwakuwa bado tupo kwenye malengo,” amesema Baresi.
Kocha Mkuu wa Prisons, Aman Josiah amesema pamoja na mwanzo mzuri wa ushindi huo, lakini kazi ni mzito akiwaomba mashabiki kuendelea kushirikiana na timu kuhakikisha wanabaki Ligi Kuu.
Amesema hesabu zake ni kuona timu inashinda kila mechi ili kupunguza presha iliyopo katika vita ya kushuka daraja vinginevyo ligi ni ngumu huku akiwapongeza wachezaji kwa juhudi binafsi.
“Mechi ilikuwa na upinzani sana lakini vijana wamepambana hadi kupata bao la ushindi dakika za mwisho, bado tunahitaji pointi kwakuwa hatujawa salama, mashabiki waendelee kutusapoti timu ibaki Ligi Kuu,” amesema Josiah.
Dodoma Jiji 0-1 Pamba Jiji
Licha ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji, lakini haikutosha kuifanya Pamba Jiji kujinasua kwenye mstari wa kushuka daraja ikiendelea kusalia palepale nafasi ya 14.
Pamba Jiji inayonolewa na Kocha Fred Felix Minziro, imepata ushindi huo kupitia bao la Mathew Momanyi dakika ya 23.
Huo ni ushindi wa tatu kwa Pamba Jiji msimu huu baada ya kucheza mechi 17, imetoka sare sita na kupoteza michezo nane.
Kwa upande wa Dodoma Jiji ambayo ilikuwa ikipambana kupata ushindi, ilijikuta ikiondoka nyumbani na kichapo hicho baada ya duru la kwanza matokeo kuwa 0-0 dhidi ya Pamba Jiji.
Dodoma Jiji imesalia na pointi 16 ikiwa nafasi ya tisa kwenye msimamo.