Dar es Salaam. Wakati Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikitangaza ajira 1,596, wadau wa uchumi na wafanyabiashara wamesema zitasaidia kurahisisha huduma na kuongeza makusanyo ya kodi.
Tangazo la nafasi hizo za ajira limetolewa leo Alhamisi Februari 6, 2025 na kusainiwa na Kamishna mkuu wa mamlaka hiyo, Yusuf Mwenda.
“TRA inapenda kuajiri watumishi wenye sifa, uwezo na maadili kushika nafasi za kazi katika Idara ya Mapato ya Ndani, Forodha na Ushuru, Usimamizi na Utawala wa Rasilimali Watu, Huduma za Sheria, Menejimenti ya Manunuzi, Utafiti na Mipango, Fedha, Ukaguzi wa Ndani, Mambo ya Ndani na Idara ya Vihatarishi na Uzingatiaji. Kwa hiyo maombi yanaalikwa kutoka kwa Watanzania wenye sifa,” imeeleza taarifa ya TRA.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia tangazo hilo, amesema ajira hizo zinalenga kuongeza ufanisi katika ukusanyaji kodi kwani kuna maeneo ambayo yalikuwa hayajafikiwa vizuri, hasa baada ya shughuli za biashara kuongezeka katika wilaya na mikoa.
“Pia hii inaenda sambamba na mipango ya miaka mitano tuliyojiwekea ili tuweze kukusanya kodi zaidi na hili linafanyika kwa kuongeza nguvu katika maeneo ambayo yalikuwa na upungufu,” amesema.
Mbali ya ufanisi, Kayombo amesema ajira hizo zitaongeza nguvu katika maeneo yenye upungufu wa watumishi, akitoa mfano wa waendeshaji wa boti za doria katika maziwa na bahari, ambako ajira hizo zitaongeza nguvu kwenye usimamizi wa maeneo hayo.
“Tunaomba waombaji wachukue tahadhari wasije kutokea matapeli wa kuwalaghai, wafuate utaratibu kwa kutumia link sahihi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania. Kama kuna mtu ana swali apige simu kituo cha huduma kwa wateja. Waombe mtandaoni tu na kwa taratibu ambazo zimeelekezwa. Hakuna malipo yoyote na ikiwa mtu ataambiwa alipe, ajue hiyo siyo TRA,” amesema.
Kwa mujibu wa tangazo la TRA, maombi yote yafanywe kupitia mfumo maalumu wa ajira wa mamlaka hiyo ambao ni: https://recruitment.tra.go.tz/tra careers/User/UserHome.aspx.
Akizungumzia hatua hiyo, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Kariakoo, Severine Mushi amesema huenda ni utekelezaji wa pendekezo la kuongeza watumishi wa mamlaka, lililotolewa na Mwenyejiki wa Wafanyabiashara Taifa, Khamis Livembe wakati wa utoaji tuzo kwa walipakodi.
Hili litakwenda kutatua changamoto ya ucheleweshaji huduma, hususani kwa wafanyabiashara ambao walilazimika kukaa katika foleni kwa muda mrefu kusubiri huduma.
“Ni kama walikuwa na ufinyu wa wafanyakazi, jambo lililosababisha foleni watu wakisubiri huyu ahudumiwe, akimaliza amhudumie na yule, hii ilifanya watu kutumia muda mrefu katika ofisi zao,” amesema.
Amesema ajira hizo zitarahisisha utoaji huduma hasa kwa kuwafuata wafanyabiashara katika maeneo yao.
Amesema wameshawahi kupendekeza Kariakoo kuwekwe walau maturubai maalumu matano kwa ajili ya kurahisisha huduma kwa wafanyabiashara.
“Kuweka ‘point (vituo) katika maeneo yaliyochangamka kutapunguza msururu wa watu kwenda ofisi zao na itafanya tuhudumiwe kwa wakati,” amesema.
Mtazamo huo umeungwa mkono na mfanyabiashara, Venace Nyeri aliyesema kuajiriwa kwa watumishi hao huenda kukaleta ahueni ya huduma na kupunguza mzigo wa kazi.
“Hata huduma huenda zitaimarika maana mtu anachoka, akichoka unategemea lolote linaweza kutokea ikiwemo kujibu vibaya au kushindwa kukuelewesha vyema kama inavyotakiwa. Wakiwa wengi wataweza kugawana majukumu,” amesema.
Hata hivyo, amewataka watumishi hao kupikwa vyema na kukumbushwa miiko ya kazi ili wasiwe chanzo cha mvutano kati ya wafanyabiashara na TRA.
Kwa mtazamo wake, mtaalamu wa uchumi, Dk Donath Olomi amesema upo uhusiano mkubwa wa ongezeko la makusanyo ya kodi na uwepo wa idadi ya watumishi wa kutosha.
Amesema huenda nafasi hizo zikawa si mpya bali wanataka kujaza zilizoachwa wazi na watumishi walioondoka kwa kuacha kazi, kufariki dunia au kustaafu.
“Unajua nchi inakua na maeneo ya kukusanya kodi yanaongezeka, jambo ambalo linaongeza vituo vya kodi, hivyo inaweka ulazima wa kuongeza rasilimali watu.
“Ukusanyaji kodi pia unategemea uwepo wa watumishi na katika mazingira ya nchi yetu si kwamba watu wanajipeleka wenyewe lazima watembelewe, wakakuguliwe ndiyo maana wametangaza kazi za aina tofauti,” amesema.
Dk Olomi amesema kuongezeka kwa watumishi kunahusiana na malengo ya kuongeza mapato kama ambavyo inakuwa imekusudiwa.
Mtaalamu wa biashara na uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Tobias Swai amesema kila mfanyakazi anatakiwa kuwa na idadi ya watu anaopaswa kuwahudumia ili huduma ziwe nzuri, hivyo wingi wao ndio utarahisisha hilo hasa katika kipindi hiki ambacho shughuli za kiuchumi zinaongezeka.
“Hitaji la ajira ni kubwa, kazi ya kodi inahitaji akili, ujuzi na kujua huduma ambazo mtu anataka, hivyo tukiwa na ajira na watu wengi wanaosimamia masuala ya kodi ni muhimu,” amesema.
Dk Swai amesema kukua kwa uchumi na maeneo ya kikodi kuongezeka kunachochea uhitaji wa ofisi katika baadhi ya maeneo ambayo hayajaguswa na huduma za kikodi kwa maana ya ofisi na ajira.
Mata hivyo, Profesa Abel Kinyondo, mtaalamu mwingine wa uchumi na biashara, amesema wingi wa watumishi siyo, hoja bali namna ambavyo wanaweza kufanya kazi kwa weledi.
“Wenzetu wanafanya kazi kwa kutumia teknolojia kwa kiasi kikubwa ambayo inapunguza mianya ya rushwa lakini sisi bado hatujafikia huko, hivyo watu wana umuhimu wa kuajiriwa kuleta mabadiliko, lakini wafundishwe vizuri,” amesema.
Profesa Kinyondo amesema anaamini waajiriwa watafanya kazi kwa kiwango kinachotegemewa.
Kada ajira zilizotangazwa
TRA katika tangazo hilo, nafasi za ajira zilizotangazwa ni katika kada zifuatazo:
Ofisa Msimamizi Ushuru daraja la II nafasi 573, Ofisa Forodha daraja la II (232), Msaidizi wa Usimamizi wa Ushuru daraja la II (253), Msaidizi wa Forodha daraja la II (154) na Mhadhiri Msaidizi (15).
Ofisa Usimamizi Data daraja la II (20), Ofisa Rasilimali Watu daraja la II (11), Ofisa Utawala daraja la II (3), Ofisa Usafirishaji daraja la II (5) na Ofisa Milki daraja la II (15).
Pia TRA imetangaza nafasi za Wahandisi daraja la II (12), Wajiolojia daraja la II (2), Ofisa Hesabu daraja la II (12), Mhasibu daraja la II (2), Ofisa Mambo ya Ndani daraja la II (10), Ofisa vihatarishi daraja la II (8) na Wachumi daraja la II (6).
Nafasi nyingine ni Watakwimu daraja la II (4), Mwanasheria daraja la II (6), Ofisa Manunuzi, Usambazaji daraja la II (5), Ofisa Maabara (3), Mkutubi daraja la II (4) na Ofisa Taaluma daraja la II (2).
Wamo pia Mkaguzi wa Ndani daraja la II (2), Mlinzi daraja la II (2), Ofisa Uhusiano daraja la II (5), Msaidizi wa Mafunzo (2), Katibu Muhtasi daraja la II (12), Mtaalamu wa Maabara daraja la II (4), Ofisa Hesabu Msaidizi (10) na Msaidizi wa usimamizi wa rekodi daraja la II (10).
Nafasi nyingine ni Mafundi uashi na umeme daraja la II (10), Mwendesha mfumo wa ulinzi daraja la II (9), Nahodha daraja la II (8), Fundi boti (8), Mkutubi msaidizi daraja la II (2), Nahodha msaidizi daraja la II (2), mhudumu wa mapokezi daraja la II (20), Dereva daraja la II (105) na Msaidizi wa ofisi daraja la II (27).