Serikali yaialika sekta binafsi uwekezaji wa nishati nchini

Arusha. Serikali imezialika sekta binafsi, hususan wamiliki na waendeshaji wa viwanda juu ya fursa mpya ya kutumia mabaki ya malighafi ambayo kwa kawaida hutupwa, ili kuzalisha nishati ya umeme nchini.

Serikali imesema kuwa matumizi ya taka katika kuzalisha umeme, mbali na viwanda kujitosheleza kwa umeme na kupunguza gharama za uendeshaji pia itaweza kujipatia kipato cha ziada kwa kuiuzia serikali nishati hiyo.

Kauli hii ilitolewa leo Februari 6, 2025 jijini Arusha na Mratibu wa Mradi wa Ufanisi wa Nishati katika Wizara ya Nishati, Emilian Nyanda, kwenye warsha ya wadau wa sekta mbalimbali kuhusu maendeleo ya teknolojia ya kubadili mabaki ya taka ya kilimo kuwa nishati ijulikanayo kama ‘Waste to Energy’.

Nyanda amesema matumizi ya taka kuzalisha umeme si tu yatasaidia Serikali kufikia malengo yake ya kuongeza uzalishaji wa umeme, bali pia yatajenga mazingira endelevu kwa kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Warsha hiyo iliandaliwa kwa ushirikiano na Shirika la Maendeleo la Viwanda la Umoja wa Mataifa (Unido) na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), ikilenga kukuza teknolojia ya kubadilisha taka kuwa nishati (Waste to Energy – WtE) katika viwanda vya kilimo.

Mradi huu ni sehemu ya juhudi za Serikali na sekta binafsi kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi, kuaminika, na endelevu.

Nyanda amesema kuwa kwa sasa Serikali inazalisha zaidi ya megawati 3,400 za umeme na ina mpango wa kuongeza hadi megawati 5,000.

Amesema kuwa viwanda vya sukari na bidhaa za misitu vimekuwa vikizalisha umeme wao kwa kutumia mabaki ya malighafi, na baadhi ya viwanda kama vile kiwanda cha sukari cha TPC vimekuwa vikichangia zaidi ya megawati 10 kwenye gridi ya taifa.

Akichangia mjadala huu, mmoja wa wadau wa sekta binafsi, David Shilatu ambaye pia ni meneja wa Kiwanda cha Sukari cha TPC, amesema Serikali inapaswa kupitia upya sera yake ya nishati ili kuweka bayana manufaa yanayopatikana kwa mtu binafsi anayechangia umeme kwenye gridi ya taifa, ili kuvutia uwekezaji zaidi.

Amesema kiwanda cha TPC, wamekuwa wakizalisha zaidi ya megawati 18  kutoka kwa mabaki ya miwa, ambapo zaidi ya megawati 5 huingizwa kwenye gridi ya taifa baada ya kutosheleza mahitaji yao ya nishati.

Amesema ili kuvutia uwekezaji zaidi, ni muhimu kuwepo na mazingira bora ya kisera yatakayoleta manufaa kwa upande wa sekta binafsi.

Awali, Ofisa Msimamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (Unido) nchini Tanzania, Lorence Ansermeta amefafanua kuwa mafunzo haya ni sehemu ya mradi wa miezi mitano (Desemba 2024 – Aprili 2025) unaoitwa “Kukuza Matumizi ya Teknolojia ya Kubadili Taka Kuwa Nishati (WtE) katika Viwanda vya Kilimo Tanzania”, unaofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Kimataifa (GEF).

Lorence amebainisha kuwa mradi huu unalingana na Lengo la Maendeleo Endelevu (SDG) 7, linalotaka kuhakikisha “upatikanaji wa nishati nafuu, kuaminika, endelevu na kisasa kwa wote,” pamoja na SDG 13, linalotaka “hatua za dharura kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake ifikapo mwaka 2030.”

Amesema Tanzania inaweza kufanikisha malengo haya ikiwa Serikali itashirikiana na sekta binafsi kuzalisha umeme endelevu kwa mazingira.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha NM-AIST, Profesa Anthony Mshandete amesisitiza umuhimu wa usalama wa nishati kwa sekta mbalimbali za uchumi na kuahidi kuendelea kufanya tafiti zinazosaidia uzalishaji wa nishati ya kutosha.

Related Posts