Sillah aipa Azam FC pointi tatu, Kally akaribishwa kwa kichapo

MATAJIRI wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC wameibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, huku nyota wa kikosi hicho, Gibril Sillah akitupia yote kambani.

Sillah alianza kuiandikia Azam FC bao la kwanza dakika ya 27, baada ya beki wa KMC, Juma Shemvuni kuchanganyana na kipa wake, Ismail Mpank, huku la pili akitupia kwa kichwa kufuatia kupokea krosi iliyochongwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Katika mchezo huo ulishuhudia aliyekuwa kocha wa muda wa Azam FC, Kally Ongala akirejea tena kwenye viunga vya Chamazi kwa mara ya kwanza tangu alipoondoka Julai mwaka 2023, ambaye kwa sasa ndiye mkuu wa benchi la ufundi la kikosi cha KMC.

Ongala alitangazwa na KMC Novemba 14, mwaka jana akichukua nafasi ya aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Abdihamid Moallin, aliyejiuzulu mwenyewe kisha kujiunga na Yanga, baada ya kuiongoza KMC msimu huu katika ya michezo 11, ya Ligi Kuu Bara.

Moallin ambaye pia aliwahi kuifundisha Azam FC alijiuzulu Novemba 11, mwaka jana, huku akiiongoza KMC katika michezo 11, ambapo kati ya hiyo alishinda minne, sare miwili na kuchezea vichapo vitano.

Kally ameiongoza KMC katika michezo sita ya Ligi Kuu Bara ambapo kati ya hiyo alishinda mmoja  wa bao 1-0, dhidi ya Pamba Jiji,  Desemba 16, 2024.

Mitatu amechezea vichapo akianza mbele ya Dodoma Jiji (2-1), Novemba 24, 2024, (2-0) v Tabora United Novemba 29, 2024 na (2-0) v Azam FC.

Michezo miwili ni ya sare akianza na (0-0) v Mashujaa Desemba 12, 2024 na ya bao 1-1, dhidi ya Coastal Union, Desemba 29, 2024.

Mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam, Septemba 19, mwaka jana, Azam FC ilishinda mabao 4-0, yaliyofungwa na Idd Selemani ‘Nado’, Lusajo Mwaikenda na Nassor Saadun huku Fredy Tangalo akijifunga mwenyewe.

Kwa upande wa Azam FC, huu ni ushindi wa tatu mfululizo katika Ligi Kuu Bara tangu mara ya mwisho ilipochapwa mabao 2-1, dhidi ya Tabora United Desemba 13, 2024, ambapo kiujumla ni wa 12, kati ya michezo yake 17, iliyocheza kwa msimu huu.

Tangu Rachid Taoussi ateuliwe kuiongoza Azam Septemba 7, 2024 akichukua nafasi ya Msenegali, Yousouph Dabo aliyetimuliwa Septemba 3, 2024, ameiongoza katika michezo 16 ya Ligi Kuu Bara akishinda 12, sare miwili na kupoteza miwili

Kiujumla Azam imecheza michezo 17, ikishinda 12, sare mitatu na kupoteza miwili, ikifunga mabao 27 na kuruhusu manane, ikiwa nafasi ya tatu na pointi 39, nyuma ya Yanga inayoongoza na pointi 45, ikifuatiwa na Simba pointi 44.

Kwa upande wa KMC inashika nafasi ya 10 na pointi zake 19, baada ya kushinda michezo mitano tu, sare minne na kupoteza minane, ikifunga jumla ya mabao 11 na kuruhusu 23, kufuatia kushuka dimbani hadi sasa katika mechi 17 za Ligi Kuu Bara.

Related Posts