Arusha. “Ilikuwa imesalia siku moja Jackson aripoti kazini (Februari 3, 2025)…ndiyo maana alikuwa anakuja na kurudi kwa haraka,”
Huyo ni Janeth Lema, shemeji wa marehemu Jackson Justine (25) aliyefariki dunia kwa ajali ya gari alipokuwa akimsaidia kuliendesha mama wa rafiki yake aliyekuwa ameenda jijini Dar es Salaam kupokea gari lake jipya alilonunua kutokana na fedha za mafao.
Akimzungumzia Jackson enzi za uhai wake leo Alhamisi Februari 6, 2025, Lema anasema hawakutegemea kama tukio hilo litamkuta shemeji yake aliyefariki dunia Februari Mosi, mwaka huu eneo la Mdawi Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro akiwa na rafiki yake, Mark Exaud(22) na mama yake, Apaikunda Ayo (61) mwalimu mstaafu wa Shule ya Msingi Imbaseni wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Ajali hiyo ilitokea asubuhi baada ya gari lao aina ya Toyota RAV4 kugongana na basi la kampuni ya Esther Luxury wakitokea Dar es Salaam.
Akiendelea kusimulia maisha ya Jackson anayezikwa leo nyumbani kwao eneo la Kikatiti, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Lema anasema amefariki dunia akiwa amebakiza siku moja kuripoti kazini baada ya kuhitimu Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) mwaka 2024 kisha kupata ajira mwishoni mwa Januari, mwaka huu.
“Jackson alipata kazi mwishoni mwa Januari, alisaini mkataba Januari 30, 2025 na alitakiwa kuripoti kazini Februari 3, 2025 kama meneja wa kitengo cha vijana katika moja ya Shirika la Kimataifa lililopo jijini Dar es Salaam. Ilikuwa imesalia siku moja ndiyo maana alikuwa anakuja na kurudi kwa haraka ili Jumatatu aripoti kazini,”anasema Lema
Nakuongeza kuwa, “Hatukutegemea hiki kitu kitamkuta, Jackson alikuwa kijana mtulivu, msikivu, mcha Mungu na alikuwa na upendo na marafiki zake. Alikuwa radhi kupoteza kitu chake, lakini amfurahishe rafiki yake, alikuwa mwepesi wa kutumwa huwezi kumwambia kitu akasema hapana,”
Anasema baada ya kuhitimu chuo Julai, 2024 ilipofika Septemba mwaka huo alianza kutafuta kazi sehemu mbalimbali, huku akiendelea na shughuli ndogondogo za kujiingizia kipato.
“Kiimani inatufundisha tujiandae kwa maana hakuna ajuaye siku wala saa, inatuumiza sana Jackson amekufa ghafla, hakujua pale ndiyo ilikuwa pumzi yake ya mwisho. Tumtegemee Mungu katika maisha kwa sababu kesho yetu hatuijui,”ameongeza
Jackson alivyomuaga kaka yake
Lema anaendelea kusimulia kuwa, Ijumaa ya Januari 31, 2025 Jackson alimpa taarifa kaka yake kwamba rafiki yake ambaye na wao kama familia wanamjua (Mark), mama yake amenunua gari hivyo wamemuomba kwa sababu yeye ana uzoefu wa kuendesha umbali mrefu wamsindikize kumleta mama yake Arusha.
“Kaka yake alimpa ruhusa na baada ya kuongea naye alimpa ushauri asafiri asubuhi ila jioni Jackson aliomba sana asafiri usiku huo, kwa hiyo aliondoka nyumbani akapita kwa rafiki yake anaitwa Paul kisha akaenda kuchukua gari wakaondoka,”anaeleza
Nakuongeza, “Saa tisa usiku alipost status kwenye whatsapp na kuandika ‘On the way to Arusha’, alikuwa ana imani atafika salama na atarudi kuanza kazi yake mpya na ni kazi ambayo ameisubiri kwa muda mrefu,”
Kuhusu taarifa za msiba, Janeth amesema walizipata kupitia mitandao ya kijamii na baada ya kuoanisha namba za usajili za gari lililopata ajali na alilokuwa amepost kwenye mtandao (whatsapp) na majina yalipotajwa walibaini ndugu yao amefariki dunia.
“Kiukweli imetuchukua muda kuamini kweli Jackson amefariki, juzi baada ya kusikia rafiki yake na mama yake wamezikwa ndiyo nimeamini shemeji yangu hayupo…njia nzima wakati tunatoka Dar es Salaam kuja hapa kwa ajili ya mazishi tulidhani labda ni ndoto,”
Tayari, Apaikunda na Mark wamezikwa Februari 4, 2025 katika Kijiji cha Imbaseni wilayani Arumeru ambapo mstaafu huyo na mumewe Exaud Mbise waliagiza gari hilo nchini Japan.
“Mke wangu alistaafu mwaka jana,akawa amelipwa mafao yake,tukakaa na kushauriana kwamba katika mafao,tulipanga vitu vingi.Mimi hela yangu na mke wangu ni zetu wote.Kati ya vitu tulivyopanga ni kununua lile gari,kisha mipango mingine,”amesema Mbise
Juzi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Imbaseni, Mwalimu Naetwe Emmanuel, akimzungumzia Ayo alisema amefanya naye kazi kwa miaka miwili kabla hajastaafu Oktoba mwaka jana,na kama ofisi walifanya sherehe ya kumuaga Desemba 6, 2024, na kwamba bado walikuwa wakishirikiana naye katika masuala ya kijamii.
Siku ya tukio Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari dogo kujaribu kuyapita magari mengine, bila kuchukua tahadhari na kugongana uso kwa uso na basi hilo la abiria.