Siri CCM kuendelea kudunda madarakani

Morogoro. Mwanasiasa mkongwe aliyewahi kushika nyadhifa kadhaa za uongozi ndani ya CCM na serikalini, Stephen Mashishanga amesema ili chama hicho kiendelee kushika dola lazima wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi wawe wenye kukubalika na wananchi.

Amesema licha ya chama hicho kuendelea kuongoza nchi na kutimiza miaka 48 tangu kuzaliwa kwake, bado kinapaswa kuboresha eneo la uteuzi wa wagombea kwenye nafasi kama za ubunge na udiwani.

Mashishanga amesema hayo kwenye mahojiano na Mwananchi alipokuwa akizungumzia kuhusu maadhimisho ya miaka 48 ya CCM ambayo husherehekewa Februari 5 ya kila mwaka.

Amesema CCM katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba mwaka huu, kinapaswa kuteua wagombea wanaokubalika kwa wananchi.

Amesema kikifanya hivyo, kinaweza kujihakikishia kuendelea kushinda chaguzi zote zitakazoendelea kufanyika nchini kutokana na mtaji wa wanachama walio nao.

Hata hivyo, Mashishanga hakutoa mfano wa kauli yake hiyo, lakini kumekuwa na malalamiko ndani ya CCM kuteua wagombea ambao hawakushinda kura za maoni ndani ya chama na wakati mwingine hawakubaliki kwa wananchi.

Mashishanga ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 91, amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado chama hicho kinapaswa kuhakikisha kinamaliza changamoto zinazowakera wananchi, lakini pia kurudisha majina ya wagombea wanaokubalika na wananchi kwenye maeneo yao.

“Huu mtindo wa kurudisha majina ya wagombea ambao hawakubaliki na siyo chaguo la wananchi, kunaweza kukawa na madhara na tukajikuta tunapigwa.

“Lakini kama chama kitarudisha majina ya wagombea wanaokubalika na wananchi, basi tutaendelea kupata ushindi na sisi wakongwe wa siasa tupo, kazi yetu ni kushauri na kukipigia debe chama,” amesema Mashishanga.

Amesema mafanikio mengine ndani ya chama ni kuongeza idadi ya wanachama zaidi ya milioni 12, lakini pia kuwa na ilani bora ya uchaguzi inayojali zaidi kero za wananchi na kujua namna bora ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Kwa upande wa mafanikio ndani ya Serikali, Mashishanga amesema katika awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni mwenyekiti wa CCM Taifa, ameweza kuleta mageuzi kwenye taasisi mbalimbali na kuboresha utawala bora.

“Katika kipindi cha miaka 48, CCM kwa sababu ya sera zake nzuri, kumekuwa na uboreshaji mzuri wa mazingira ya uwekezaji wa nchi, lakini pia kwa mtu mmoja mmoja,” amesema Mashishanga.

Akieleza uzoefu wake wa uongozi ndani ya chama na Serikali, Mashishanga amesema alijiunga na Tanu mwaka 1958 na nafasi alizowahi kushika ni pamoja na ukatibu wa CCCM katika baadhi ya mikoa na baadaye ukuu wa mkoa wa Morogoro.

Mashishanga ameeleza matumaini yake kwa mgombea mwenza wa urais, Dk Emmanuel Nchimbi kwamba anamfahamu ni mmoja wa vijana waliopita kwenye mikono ya wanasiasa wakongwe akiwemo yeye, hivyo mkutano mkuu wa CCM umekitendea haki chama kwa kumchagua Nchimbi.

“Kwanza ni kijana, tena ni msomi pia anaijua vizuri siasa ya Tanzania, kwa sababu alishapita kwenye nafasi mbalimbali ikiwemo ya ubalozi, sina shaka naye na uongozi wake,” amesema Mashishanga.

Amewataka wananchi wakiwemo wanaCCM kumuunga mkono Rais Samia ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM ili pamoja na Serikali yake, aweze kutekeleza ilani ya CCM.

Related Posts