Dodoma. Baada ya Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kutangaza kusitisha utoaji fedha, Serikali imesema inajiimarisha kuhakikisha inakuza uchumi kwa kutumia vyanzo vya fedha na mapato kujazia maeneo yaliyopungua.
USAID imetangaza kusitisha utoaji fedha mpya na usambazaji wa fedha chini ya makubaliano ya malengo ya Maendeleo (DOAGs) hadi uhakiki kwa programu za msaada wa nchi zinazofadhiliwa na USAID utakapokamilika ndani ya siku 85 kuanzia Januari 24, 2025.
Mchakato wa uhakiki unalenga kuhakikisha msaada wa nje unalingana na ajenda ya sera ya nje ya Rais Donald Trump.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akijibu swali la papo kwa hapo bungeni leo Februari 6, 2025 amesema Serikali inajiimarisha kukuza uchumi kwa kutumia rasilimali zilizopo ili kumudu utekelezaji katika maeneo yote muhimu yakiwamo ya sekta ya afya, elimu na maji.
Majaliwa amesema hayo akijibu swali la Mbunge wa Mbozi, George Mwanisongole aliyehoji Serikali inajipangaje kukabiliana na mabadiliko ya sera za nje za Marekani ambazo zinakwenda kuathiri utekelezaji wa sera za Tanzania kwenye maeneo kadhaa yakiwamo ya elimu na afya.
“Serikali inajipanga vipi na sera za mabadiliko ya nchi ya Marekani ambazo tangu Rais Donald Trump aingie madarakani amefanya mabadiliko makubwa ya sera ya nje ya nchi yake ambayo yanakwenda kuathiri utekelezaji wa sera zetu kwenye elimu, afya na kiuchumi,” amehoji.
Mbunge huyo ameitaja miradi hiyo kuwa ni inayofadhiliwa na USAID, Mradi wa Programu ya Kutekeleza Elimu kwa Matokeo (EP4R) na Programu ya kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi (VVU).
Majaliwa amesema Tanzania inaheshimu sera za mambo ya nje na inatekeleza mikataba ya sera hizo kama ambavyo wamekubaliana na nchi husika kwenye maeneo mbalimbali.
“Tumeanza kuona nchi zenye uwezo mkubwa ikiwemo Marekani na mabadiliko haya yanaathiri baadhi ya nchi na hata yetu inaweza kupata baadhi ya athari, lakini kwetu ni muhimu kuzingatia sera za nje kama ambavyo tumekubaliana,” amesema.
Majaliwa amesema: “Uwezo tunao, tunazo maliasili, tunazo rasilimali, kazi ambayo tunayo ni Watanzania kushirikiana kuhakikisha tunatumia maliasili na rasilimali tulizonazo kujenga uchumi wa ndani kuwezesha mipango na bajeti iweze kutekeleza haya.”
Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kueendelea kuifanya Tanzania kuwa na mahusiano mazuri na nchi nyingi duniani ikiwamo Marekani.
“Sisi pamoja na upana wa mahusiano ambayo tumeyaweka ni kuhakikisha kwamba tunajiimarisha na kuwa na uwezo wa ndani. Lazima tujiimarishe kwenye mipango yetu, bajeti zetu ziweze kutekeleza maeneo yote muhimu ikiwemo sekta ya afya, elimu, maji na maeneo mengine kadri walivyokubaliana na nchi husika,” amesema.
Amesema kazi nyingine ni kuwezesha mipango na bajeti iweze kutekeleza yote.
“Niseme kuwa Marekani imeshatangaza na inawezekana na nchi nyingine zikatangaza kukawa na mabadiliko na sisi tunaendelea kujiimarisha kwa kuhakikisha kuwa tunakuza uchumi wetu kwa kutumia vyanzo vya fedha na mapato.
“Tunaweka pamoja na kuingiza hapa bungeni yapangiwe mpango kazi ili maeneo yaliyopungua tuweze kujaziliza, huo ndio mkakati sasa tunatakiwa kuwa nao na tunaweza kujipanga kutokana na mabadiliko ambayo sasa yanaendelea kwenye nchi zilizoendelea dhidi ya nchi zinazoendelea kama Tanzania,” amesema.
Bunge Februari 4, 2025 liliazimia Serikali itekeleze mpango wa kupata rasilimali za ndani kupambana na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi bila kutegemea msaada wa wafadhili.
Azimio la Bunge lilifikiwa baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Elibariki Kingu kuwasilisha taarifa ya kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa shughuli zake katika kipindi cha kati ya Februari 2024 hadi Februari 2025.
Kingu alisema kiwango kikubwa cha utekelezaji wa afua za VVU na Ukimwi nchini hutegemea fedha za wafadhili kutoka nje ya nchi.
“Ufadhili huo ukifikia ukomo unaweza kusababisha kwa kiasi kikubwa nchi kupunguza kasi ya kupambana na janga hilo kwa kukosa fedha za kutosha,” alisema.