Wanafunzi wapewa ujasiri kufichua vitendo vya ukatili

Siha. Mkuu wa Shule ya Sekondari Ormelili, Hapriday Msomba amewataka wanafunzi wa shule hiyo kutokaa kimya bali wapaze sauti dhidi ya vitendo vya ukatili pale wanapovibaini.

Amesema hata wakipatiwa elimu ya kujilinda dhidi ya ukatili wa kijinsia, watoe elimu kwa wenzao ambao hawajabatika kupata elimu hiyo ya kulinda na vitendo hivyo vikiwamo vya ubakaji na ulawiti.

Msomba ametoa rai hiyo leo Alhamisi wakati wa kampeni ya msaada wa kisheria inayojulikana kama Mama Samia Legal Aid, ilipotembelea shule hiyo kwa lengo la kuwaelimisha wanafunzi kuhusu changamoto zinazowakabili na kuwajengea uwezo wa kupambana na vitendo vya ukatili.

Hata hivyo, Msomba amewashukuru waandaaji wa kampeni hiyo na kuwasisitiza wanafunzi kueneza elimu waliyoipata.

“Msiwe mabubu, endeleeni kufundisha wengine. Mlichopata hapa, waelimisheni wadogo zenu na wazazi wenu. Wambieni kwamba wageni walitutembelea shuleni na kutufundisha mambo muhimu kuhusu ukatili,” amesema Msomba.

Amesema kuendeleza kampeni hiyo kutasaidia kupunguza ukatili kwa sababu jamii itakuwa na uelewa mkubwa kuhusu haki na usalama wa watoto.

Baadhi ya wanafunzi, akiwamo Godlight Mollel amesema ukatili mwingine unaoathiri jamii yao ni ndoa za utotoni kwa wasichana na ajira hatarishi kwa wavulana.

“Baadhi ya mabinti wadogo huozeshwa pale wanaposhindwa mtihani wa kidato cha pili. Hili halikubaliki. Tuendelee kusoma ili kupata wasomi watakaoliendeleza taifa,” amesema Mollel.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya hiyo, Peter Msaka amesisitiza kuwa matukio ya ukatili dhidi ya watoto yanaongezeka, hivyo ni muhimu kwa watoto kuchukua tahadhari.

Amewataka wanafunzi kuchukua hatua wanapoona viashiria vya ukatili kwa kukimbia, kupiga kelele kuomba msaada, au kutoa taarifa kwa watu wanaowaamini kama wazazi, viongozi wa dini, viongozi wa serikali na walimu.

Hatua hizi ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha watoto wanakuwa salama na wanapata fursa ya kusoma bila hofu ya kufanyiwa ukatili.

Related Posts