Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa, kujiamini, kujitambua na ushirikiano kwa wanawake ni mongoni mwa mambo yatakayochochea kundi hilo kufikia maendeleo mbalimbali ikiwamo ya uongozi mahiri sehemu za kazi hasa katika sekta ya uzalishaji viwandani.
Kuhamasisha wanawake kiuongozi, pia ni sehemu ya juhudi za kimataifa kama vile Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), hasa lengo namba tano kuhusu usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika nyanja zote za maisha.
Akizungumza katika uzinduzi programu ya Girls For Girls, leo Alhamisi Februari 6 2025 Meneja Rasilimaliwatu wa Alaf Tanzania Jumbe Onjero, amesema katika sekta ya uzalishaji wanaume wengi wapo juu kiuongozi kuliko wanawake.
Amesema kwa upande wao, hali hiyo imesababisha waanzishe programu za kuwahamasisha wafanyakazi wa kike kushika nyadhifa katika viwango vya menejimenti, ikiwamo ya Wanawake Katika Uongozi.
“Tunayo programu iliyoanzishwa, lengo lake kubwa ni kuona ni namna gani katika uongozi wa kampuni kunakuwa na wanawake, kwa maana katika sekta ya viwanda, uongozi mwingi upo kwa wanaume, ni wanawake wachache wapo katika nyadhifa za juu za maamuzi kwenye sekta ya uzalishaji,”amesema Onjero.
Amesema lengo ni kwamba ifikapo mwaka 2030 asilimia 30 ya uongozi wa juu wa kampuni hiyo ushikwe na wanawake.
“Tulipanga kwa mwaka angalau kuwe na asilimia tano ya wanawake ambao wamepanda kutoka daraja la chini hadi la juu, lakini mpaka sasa tuna miaka mitatu angalau kuna asilimia 14 ya wanawake ambao wamewezeshwa, kupata mafunzo ya kiuongozi na wapo kwenye daraja la uongozi katika ngazi ya kampuni,” amesema.
Mmoja wafanyakazi wa kike wa kampuni hiyo, Glory Kimaro amesema kupitia mafunzo mbalimbali wanayopatiwa wameweza kupata nafasi za juu pamoja na kujijenga kiuchumi.
“Hata huu muunganiko ni nafasi nzuri kwetu sisi wanawake, sidhani kama tutaondoka hapa kama tulivyokuja. Kama ulikuja umelala, hapa utaondoka umeamka,” amesema Glory.
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Alaf, Hawa Bayumi amesema kupitia Programu ya Wanawake na Uongozi kuna zao la Safal linalowezesha wanawake kusaidiana na kushirikiana ili kukua katika nyanja nzima ya uongozi wa ndani, nje ya kampuni au hata katika maisha binafsi.
“Pia, program hiyo itatuwezesha kukua zaidi kwa kujitambua na kufanya mambo yatakayotusaidia sisi kama viongozi, kwa hiyo tutakuwa na miradi ambayo itatusaidia kutambua na kujua mambo ya fedha na mauzo, afya na kujitunza,” amesema Bayumi.
Meneja huyo amesema miradi hiyo itawasaidia kutatua changamoto zao wenyewe kama watu wa kawaida, lakini pia kama viongozi ndani ya kampuni.
Mtaalamu wa Talanta, Purity Kiyange amesema mabadiliko ya wanawake yanaanzia kwa wanawake wenyewe kwa kuwa kila wanachokifanya wanafanya kwa ajili yao na jamii iliyowazunguka.
Amesema lengo la kuwainua wanawake ni kujiamini katika uongozi na sio ‘ kupigana’ na wanaume; kwa kuwa kama wanawake watajiamini na kuwa viongozi bora, wataweza kutatua changamoto nyingi zinazowakabili na kuongeza mchango wao katika jamii.
Hata hivyo, amesema kinachotakiwa ni kuondoa pengo lililopo baina ya wanawake na wanaume huku akitolea mfano kuwa katika vyuo vikuu vingi nchini wanaoshika nafasi za juu ni wanaume.
“Tunahitaji kuwa wanawake mahiri katika uongozi na kuonyesha matokeo chanya kwa kufanya kitu tofauti katika jamii,” amesema Kiyange.