WATAALAMU WA UNUNUZI NA UGAVI WAASWA KUZINGATIA MADILI

Wataalamu wa sekta ya ununuzi wa umma wameaswa kuzingatia maadili ya taaluma ya fani yao katika usimamizi wa miradi ya umma ili kuiwezesha Serikali kupata thamani halisi ya fedha katika miradi yake.  

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Hassan Masala wakati wa kufunga mafunzo ya Moduli ya uwasilishaji na ushughulikiaji wa malalamiko na rufaa (Complaint and Appeal Management Module) katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya Kieletroniki (NeST) yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA).

Mhe. Mtanda ameongeza kuwa kuzingatia maadili ya taaluma ya fani hiyo katika usimamizi wa miradi ya siyo tu kutaiwezesha Serikali kupata thamani halisi ya fedha bali kutaiheshimisha fani ya ununuzi na ugavi pamoja na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Kwa kuwa matumizi ya moduli ya moduli ya kuwasilisha malalamiko na rufaa kieletroniki huokoa muda, gharama na kuongeza uwazi na uwajibikaji katika michakato ya zabuni za umma.  Nendeni mkaitumie elimu hii kuwaelimisha na wengine ili waweze kuielewa na kuitumia moduli, naamini ninyi mlioshiriki mafunzo ya awamu hii mtakuwa mabalozi wazuri wa Moduli hii na PPAA kwa ujumla,” amesema Mhe. Mtanda

Naye Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando amesema baada ya Serikali kujenga mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya Kieletroniki (NeST) na kuweka sharti la lazima kufanya ununuzi wa umma katika mfumo huo, PPAA nayo ilishirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kujenga moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kieletroniki ili kuwawezesha wadau wa ununuzi wa umma kuwasilisha malalamiko na rufaa zao kieletroniki.

“Katika kipindi cha siku tatu washiriki wameweza kujifunza masuala muhimu kuhusu mfumo wa ununuzi wa umma nchini Tanzania ikiwemo kuitazama kwa ufupi Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023, kufanya mapitio ya Mfumo wa NeST pamoja na namna ya Uwasilishaji wa malalamiko na rufaa kwa kutumia moduli katika hatua mbalimbali,” amesema Bw. Sando.

Bw. Sando ameongeza kuwa washiriki wa mafunzo wamejifunza moduli ya uwasilishaji na ushughulikiaji wa malalamiko na rufaa ambayo inajumuisha maeneo ya uwasilishaji wa malalamiko kwa Afisa Masuuli wa taasisi nunuzi iliyotangaza zabuni, uwasilishaji wa Rufaa kwa Mamlaka ya Rufani (PPAA).

Maeneo mengine ni jinsi mzabuni anavyoweza kujiunga katika Rufaa iliyofunguliwa, taratibu za uwasilishaji wa maombi mbalimbali ikiwemo ombi la nyongeza ya muda wa kuwasilisha rufaa nje ya muda ulioainishwa katika sheria, ombi la kutengua uamuzi uliotolewa kwa kusikiliza shauri la upande mmoja na ombi la kukazia hukumu.

“PPAA imejipanga vyema kuendelea kutoa mafunzo ya matumizi ya Moduli kwa wadau wa ununzi nchini kupitia kanda mbalimbali, hivyo wale ambao hawajafikiwa wajiandae kwani tutawafikia kupitia kanda zao zikiwemo kanda ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kusini, Kusini na Kati,” ameongeza Bw. Sando

Mafunzo hayo ya siku tatu yaliyojumuisha washiriki zaidi ya 580 yamefanyika mkoani Mwanza kuanzia tarehe 4 – 6 Februari, 2025 yakijumuisha mikoa ya Mwanza, Geita, Mara, Kagera, Simiyu na Shinyanga.  

Awamu ya kwanza ya mafunzo ya matumizi ya moduli iliyofanyika Mwezi Mei 2024 kwa mikoa ya kanda ya Pwani iliyojumuisha Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Morogoro.

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Hassan Masala akifunga mafunzo ya Moduli ya uwasilishaji na ushughulikiaji wa malalamiko na rufaa (Complaint and Appeal Management Module) katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya Kieletroniki (NeST) yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) Jijini Mwanza

Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando akizungumza na washiriki wa mafunzo ya moduli ya kuwasilisha rufaa kieletroniki (hawapo pichani) wakati wa kufunga mafunzo ya Moduli ya uwasilishaji na ushughulikiaji wa malalamiko na rufaa (Complaint and Appeal Management Module) katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya Kieletroniki (NeST) Jijini Mwanza

Mwenyekiti wa Mamlaka ya Rufani, Jaji Mstaafu Mhe. Sauda Mjsiri akizungumza na washiriki wa mafunzo ya moduli ya kuwasilisha rufaa kieletroniki (hawapo pichani) wakati wa kufunga mafunzo ya Moduli ya uwasilishaji na ushughulikiaji wa malalamiko na rufaa (Complaint and Appeal Management Module) katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya Kieletroniki (NeST) Jijini Mwanza

Related Posts