Watu 35,000 wang’atwa na mbwa 2024, wizara yahaha kusaka chanjo

Dar es Salaam. Wakati watu 900 wanafariki dunia kila mwaka kwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa nchini, takwimu zimeonyesha kwa mwaka 2024, takribani watu 35,000 waling’atwa na mbwa huku Wizara ya Afya ikiendelea utafuta chanzo hadi kufikia mwakani.

Takwimu hizo zimetolewa leo Alhamisi, Februari 6, 2025 na Mkurugenzi wa huduma za afya ustawi wa jamii na lishe kutoka Tamisemi, Dk Rashid Mfaume wakati wa uzinduzi rasmi wa mpango wa pamoja kati ya serikali na wadau kuangalia namna ya kudhibiti kichaa cha mbwa ifikapo mwaka 2030.

Mpango huo wa mradi wa utekelezaji, utakua ni sehemu ya mpango wa Taifa wa chanjo ambao utafadhiliwa kwa karibu na shirika la uzalishaji chanjo duniani, Gavi Alliance, pia kupitia watafiti.

Dk Mfaume amesema magonjwa ya wanyama, yasipodhibitiwa vizuri yakaja kwa binadamu huwa na madhara na ugonjwa mmojawapo ni kichaa cha mbwa.

“Ukiangalia takwimu za mwaka 2024, watu waliong’atwa na mbwa walifikia 35,000 lakini kwa tafiti mbalimbali zilizofanyika kwa Tanzania peke yake, watu 900 hufariki kila mwaka kwa sababu ya kung’atwa na mbwa,” amesema.

Dk Mfaume amesema wanatekeleza mradi huo wa pamoja kwa kushirikiana Tamisemi, Wizara ya Afya, watafiti na GAVI, “Tunataka kushirikiana kwa pamoja ili kufikisha chanjo hizi katika ngazi za mikoa na halmashauri.”

“Tumeona chanjo upande wa binadamu pia vilevile kuwe na uchanjaji, inahitaji hamasa kubwa kati ya wataalamu wa afya na wenzetu wa mifugo. Kikubwa ni hamasa, kujua ukubwa wa tatizo, kutoa elimu na kuangalia vitu gani vinaathiri ufuatiliaji wa changamoto hiyo,” amesema.

Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo, Wizara ya Afya, Dk Georgina Joachim amesema program hiyo ni kwa ajili ya kuhakikisha wanaongeza kasi ya upatikanaji wa chanjo ya kichaa cha mbwa.

Amesema Serikali imekua ikitoa huduma ya upatikanaji wa chanjo kuzuia kichaa cha mbwa kwa muda mrefu, lakini kwa sasa wameona ni muda muafaka kuhakikisha upatikanaji wa chanjo hii unaenda kwenye jamii kwa kiwango kikubwa zaidi.

“Serikali ipo kwenye jitihada ya kuhakikisha chanjo inapatikana mpaka kwenye vituo vya afya, kama ambavyo tumekuwa tukitoa huduma zingine za chanjo, kuhakikisha hatubaki nyuma tupo katika harakati hii ya kutokomeza kichaa cha mbwa mpaka ifikapo 2030,” amesema.

Akitaja jitihada ambazo Serikali imechukua ni pamoja na kutanua wigo wa upatikanaji wa chanjo, kwa kufanya jitihada mbalimbali za kutafuta fedha kwa ajili ya kuongeza upatikanaji kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za chanjo nchini.

Mtafiti mwandamini kutoka Taasisi ya Afya Ifakara, Maganga Sambo amesema tafiti zilizofanywa zinaonyesha wagonjwa wengi wanaong’atwa na mbwa hushindwa kufika vituoni kwa ajili ya matibabu.

Kuhusu upatikanaji wa chanjo amesema awali upatikanaji wake ulikuwa mgumu, chanjo zilipatikana kwa nadra katika hospitali za wilaya na gharama yake ikiwa kubwa na hivyo wengi walizipata hospitali za mikoa na ikikosekana walifika Mnazi Mmoja iliyopo jijini Dar es Salaam kwa uhakika zaidi wa chanjo.

“Mpaka sasa chanjo moja ni wastani wa Sh30,000 na unatakiwa kupata chanjo tano. Siku ya kwanza, ya tatu, ya saba, ya 14 na siku ya 21 hali iliyochangia gharama ya usafiri, chakula na malazi kwa waliokuwa katika dozi.

“Kufuatia huu uwekezaji wa GAVI, chanjo zitapatikana kwa bei ndogo, kwa sasa tunafanya kazi kwa karibu na Wizara ya Afya hizi chanjo zipatikane kwenye vituo vya afya,” amesema.

Sambo amesema kwa sasa kuna matibabu mapya, badala ya kutumia chanjo ya kwenye msuli iliyochukua muda wa siku tano, njia mpya ya chanjo ya ngozi mgonjwa atachanjwa mara tatu pekee siku ya kwanza, ya tatu na ya saba.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya wanatarajia kufikia mwaka 2026, chanjo itakuwa imepatikana.

Related Posts