Waume wadaiwa kutegesha wake zao wafumaniwe kujipatia kipato

Geita. Baadhi ya wame wilayani Bukombe Mkoa Geita wamedaiwa kutegesha wake zao kwa wanaume wengine kwa lengo la kufanya fumanizi na kudai fedha.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Katente wilayani Bukombe, Issa Shaban ameyasema hayo jana Februari 5, 2025 baada ya watoa huduma za msaada wa kisheria wa Mama Samia kutembelea ofisi yake.

Shaban amesema matukio mengi ya fumanizi ‘feki’ hufanyiwa vijana wanaojishughulisha na shughuli za uchimbaji wa dhahabu.

“Haya mambo ya ugoni kwa sasa imekuwa kama biashara au tuseme ‘dili’mke na mume wanakubaliana na aliyefumaniwa akishaona hivyo anakubali yaishe bila kujua wanandoa hao walipanga mtego, tumegundua hili na sasa tunawaelimisha waache haya mambo” amesema Shaban.

Bila kutaja idadi ya kesi ambazo amepokea za fumanizi ‘feki’ mtendajii huyo amesema ugoni ni miongoni mwa kesi nyingi zinazoripotiwa katika eneo hilo na ili kuondoa aibu aliyefumaniwa hukubali kumalizana kimyakimya ili kesi isiripotiwe.

“Mara nyingi kwenye ugoni wanataka mtu alipwe kuanzia shilingi milioni moja, au milioni moja au zaidi inategemea yule anaefumaniwa kipato chake kiko vipi na humalizana wao kwa wao ”amesema Shaban.

Amesema ukosefu wa elimu ya sheria ni miongoni mwa sababu zinazochangia mambo kama hayo kujitokeza kwenye jamii.

Mtoa huduma za msaada wa kisheria (ParaLegal), Stephano Kazyoba akizungumzia sula la kukamata ugoni amesema ili mtu akamatwe ugoni ni lazima kuwe na ushahidi wa moja kwa moja kwa wahusika kukutwa wakiwa faragha wakishiriki tendo la ndoa.

“Mtu hapaswi kutoa tuhuma za ugoni kwa kuhisi au kwa kusikia badala yake ni kwa ushahidi ama ushuhuda unaojitosheleza na taarifa zitatolewa kwa mashahidi wengine na kisha kwenye baraza la usuluhishi,” amesema Kazyoba

Naye wakili wa kujitegemea kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Esther Safari akizungumzia sula la wanandoa  wanaoingia kwenye mgogoro wa ugoni ameshauri kuzingatia hatua za kisheria na sio kujichukulia maamuzi wenywe.

Kampeni ya Msaada wa kisheria ya mama Samia imefanya kazi kwa siku tisa katika halmashauri zote sita za Mkoa wa Geita

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa kampeni hiyo leo Februari 6,2025 kwa katibu tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati, mratibu wa kampeni hiyo mkoani hapa Candid Nasua amesema kwa siku tisa wamehudumia wananchi 161,154.

Amesema kwa siku tisa wamepokea migogoro 584 na kati ya hiyo 86 imetatuliwa huku 498 ikiendelea kushughulikiwa.

Related Posts