Waziri wa Trump kutohudhuria mkutano wa G20 Afrika Kusini

Reuters. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio amesema hatashiriki mkutano ujao wa G20 utakaofanyika nchini Afrika Kusini.

Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kutishia kukata misaada kwa nchi ya Afrika Kusini.

Afrika Kusini inayoshika urais wa G20 kuanzia Desemba 2024 hadi Novemba 2025, itakuwa mwenyeji wa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo kuanzia Februari 20 hadi 21 jijini Johannesburg.

Trump alisema Jumapili, bila kutoa ushahidi, kwamba “Afrika Kusini inachukua ardhi na makundi fulani ya watu yananyanyaswa”.

Alisema atakata ufadhili hadi suala hili lichunguzwe.

Rais Cyril Ramaphosa alitetea Sera ya Ardhi ya Afrika Kusini baada ya tishio la Trump, akisema Serikali haijachukua ardhi yoyote na sera hiyo inalenga kuhakikisha upatikanaji sawa wa ardhi kwa umma.

“Afrika Kusini inafanya mambo mabaya sana. Inachukua mali binafsi. Inatumia G20 kukuza mshikamano, usawa na ustahimilivu. Kwa maneno mengine: DEI na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Rubio kwenye chapisho lake kwenye X, bila kutoa maelezo zaidi.

Trump amekuwa akilalamikia sera ya ardhi ya Afrika Kusini, huku bilionea Elon Musk, aliyezaliwa Afrika Kusini na ambaye ni rafiki wa karibu wa Trump naye ameikosoa nchi hiyo bila ushahidi, akidai kuwa sheria za kumiliki mali zina ubaguzi wa wazi na kwamba watu weupe ndio wanaoathiriwa.

Masuala ya kumiliki ardhi ni nyeti kisiasa nchini Afrika Kusini kutokana na urithi wa enzi za kikoloni na ubaguzi wa rangi, ambapo Wafrika walinyang’anywa ardhi zao na kukataliwa haki za kumiliki mali.

Wamiliki wa ardhi weupe bado wanamiliki robo tatu ya ardhi ya kilimo ya Afrika Kusini.

Hii inalinganishwa na asilimia 4 inayomilikiwa na Wafrika, ambao ni asilimia 80 ya idadi ya watu ikilinganishwa na takribani asilimia 8 kwa watu weupe, kulingana na ukaguzi wa ardhi wa 2017.

Kama sehemu ya juhudi za kurekebisha usawa huu, Ramaphosa alisaini sheria Januari inayoruhusu Serikali kuchukua ardhi kwa manufaa ya umma.

Utawala wa Trump umejaribu kubomoa mipango ya utofauti, usawa na ushirikishwaji (DEI) katika Serikali ya Marekani.

Related Posts