AfDB yaahidi Sh6.4 trilioni ujenzi wa miundombinu Tanzania

Dar es Salaam. Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeahidi kutoa Dola za Marekani 2.5 bilioni sawa na Sh6.4 trilioni, kwa ajili ya kufadhili miradi ya kipaumbele ya miundombinu nchini Tanzania.

Taarifa iliyotolewa jana Februari 6, 2025, na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kutiwa saini na Afisa Mwandamizi wa Mawasiliano ya Umma na Masuala ya Umma wa Idara ya Mawasiliano ya Shirika, Simon Owaka, imebainisha kuwa fedha hizo zitatumika kuboresha barabara, reli na viwanja vya ndege nchini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hatua hiyo inalenga kurahisisha usafiri wa watu na bidhaa, jambo litakalochochea biashara katika ukanda huo.

Mhandisi Mkuu wa Usafiri wa AfDB nchini Tanzania, Mumina Wa-Kyendo, amesema kuwa zaidi ya asilimia 70 ya fedha hizo zitatengwa mahsusi kwa miundombinu ya usafiri, ikiwemo barabara, reli na viwanja vya ndege.

“Baadhi ya miradi itakayonufaika na ufadhili huu ni sehemu ya Tanzania ya Barabara ya kimataifa ya kilomita 400 inayounganisha Bagamoyo–Pangani–Tanga–Horohoro/Lunga Lunga–Mombasa–Malindi (Kenya), ambayo kwa sasa inajengwa katika nchi zote mbili,” amesema Wa-Kyendo.

Barabara hiyo ni sehemu ya Ukanda wa Usafiri wa Pwani ya Afrika Mashariki, unaoanzia Lamu, Kenya hadi Mtwara, Tanzania.

Wa-Kyendo pia amethibitisha kuwa benki hiyo imetenga dola milioni 100 kwa ajili ya sehemu ya barabara hiyo inayopita Tanzania.

“Mara itakapokamilika, barabara hii inatarajiwa kupunguza umbali wa safari kati ya Dar es Salaam na Tanga kwa takriban kilomita 90, na kuokoa zaidi ya saa moja ya muda wa safari,” amesema.

Hii pia itawapa wasafiri njia mbadala ya kupita Bagamoyo na Pangani badala ya kutumia Ukanda wa Kati.

“Miradi mingine muhimu inayopokea ufadhili wa AfDB ni barabara ya Nyakanazi–Kabingo–Kasulu–Kumnazi katika eneo la magharibi, barabara ya Newala–Masasi kusini, reli ya Tabora–Kigoma–Uvinza itakayopanuliwa hadi Musongati nchini Burundi, na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dodoma (Msalato),” ameongeza Wa-Kyendo.

Wa-Kyendo ameyasema hayo akiwa Tanga, ambako timu ya wataalamu wa sekta mbalimbali kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Wizara ya Ujenzi ya Tanzania, na Wizara ya Barabara na Miundombinu ya Kenya walihitimisha ziara ya siku mbili ya ukaguzi wa barabara ya Bagamoyo–Pangani–Tanga.

Timu ya ukaguzi iliongozwa na Mkurugenzi wa Miundombinu katika Sekretarieti ya EAC, Robert Achieng.

Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Mkurugenzi wa Miradi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Japherson Nnko, huku timu ya Kenya ikiongozwa na Katibu wa Wizara ya Barabara na Usafiri, Kimeli Kipchumba.

Wengine waliokuwepo kwenye ukaguzi huo ni Luka Kimeli kutoka Wizara ya Barabara na Usafiri, Kenya; Moikan Mollel kutoka Wizara ya Ujenzi, Tanzania; na Naibu Mkurugenzi wa Miundombinu wa EAC, Lucy Mburu.

Walikuwepo pia Ismail Abdalla kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Tanzania; wawakilishi wa Mamlaka ya Barabara Kuu ya Kenya (KENHA), Cleophas Makau; Mamlaka ya Kuratibu Usafiri wa Ukanda wa Kaskazini (NCTTCA), Peter Bol Deng; na Mamlaka ya Kuratibu Usafiri wa Ukanda wa Kati (CCTTFA), Faraji Yassin Kondo.

Akizungumzia mikakati ya utekelezaji wa miradi hiyo Wa-Kyendo amebainisha kuwa ufadhili wa AfDB unategemea ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya miundombinu.

Amesisitiza kuwa kukamilisha miradi kwa wakati na ndani ya bajeti ni muhimu ili kupata ufadhili zaidi kwa miradi ya siku zijazo.

Pia, ameeleza umuhimu wa miundombinu ya usafiri katika kuwezesha biashara na ushirikiano wa kikanda, huku akihimiza ushirikiano wa karibu na ubadilishanaji wa maarifa kati ya mamlaka za usafiri za Ukanda wa Kaskazini na Ukanda wa Kati.

“Mafanikio ya utekelezaji wa miradi kama vile barabara za Arusha-Namanga-Athi River na Arusha-Holili/Taveta–Voi, zilizokamilika kwa wakati na ndani ya bajeti, yanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa miradi ijayo,” amesema.

Hata hivyo, Wa-Kyendo ameeleza wasiwasi wake juu mamlaka inayopaswa kusimamia ukanda unaounganisha Ukanda wa Kati na Ukanda wa Kaskazini bado haijafahamika wazi, akisisitiza kuwa pengo hilo linapaswa kushughulikiwa haraka na nchi wanachama wa EAC.

Kwa upande wake, Achieng, akimwakilisha Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva, amesema kuwa kipaumbele cha EAC ni maendeleo ya njia kumi za kimataifa zinazounda Mtandao wa Barabara wa Afrika Mashariki, huku msisitizo ukiwekwa kwenye njia tatu kuu.

Njia hizo ni ukanda wa kati (Dar es Salaam–Morogoro–Dodoma–Singida–Nyakanazi–Rusumo–Kigali–Rubavu–Nyakasanza–Kabanga/Kobero–Bujumbura–DRC), ukanda wa Kaskazini (Mombasa–Nairobi–Malaba–Kisumu–Kampala–Kigali–Juba–DRC) na ukanda wa LAPSSET: (Lamu Port–Sudan Kusini–Ethiopia).

Achieng amesema kuwa EAC kwa sasa inafanya upembuzi yakinifu na kutathmini chanzo cha ufadhili kwa barabara mpya ya kimataifa ya Kisumu–Busia/Jinja–Kakira–Malaba kati ya Kenya na Uganda, itakayorahisisha usafiri wa bidhaa na watu katika Ukanda wa Kaskazini.

Amebainisha kuwa maendeleo ya barabara na reli katika njia hizi ni kipaumbele kwa jumuiya hiyo, huku ufadhili ukitoka katika mapato ya ndani ya nchi wanachama na msaada wa maendeleo kutoka AfDB na washirika wengine wa maendeleo.

“Taarifa ya ukaguzi huu itawasilishwa katika kikao kijacho cha Baraza la Sekta ya Usafiri, Mawasiliano na Hali ya Hewa la EAC kwa ajili ya uamuzi zaidi na mwongozo wa kisera,” amesema Achieng.

Related Posts