ASASI ZA KIRAIA WALILIA AMANI DR CONGO, BUTIKU ATOA NENO KWA VIONGOZI

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

WAKATI wakuu wa nchi za Maziwa Makuu wakitarajiwa kukutana nchini Tanzania kujadili hali ya usalama katika Nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Asasi za kiraia katika nchi hizo zimesema zitaunga mkono yale yote ambayo yatajadiliwa na viongozi kuhakikisha amani katika nchi hiyo inarejea.

Kwa sasa kuna hatua mbalimbali za mazungumzo ambazo zinaendelea kuchukuliwa na viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na Jumuiya ya Maendeleo Kusini kwa Afrika (SADC), kuleta amani na utulivu nchini DR Congo.

Wakizungumza leo Januari 7,2025 jijini Dar es Salaam viongozi wa asasi hizo wameonesha kusikitishwa na mapigano yanayoendelea Mji wa Goma katika Nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kwamba iko haja ya kuhakikisha wananchi wanaungana na viongozi wao katika kukomesha mapigano hayo.

Akizungumza wakati wa kikao cha Asasi za kiraia, Mwanasheria wa Kamati Amani na Ulinzi nchini DR Congo, Eloi Bugoye amesema iwapo nchi za Maziwa Makuu na Afrika kwa ujumla wakiamua kumaliza kinachoendelea Goma inawezekana bila shida yoyote.

“Kinachoendelea DR Congo kikiachwa matokeo yake yatakuwa mabaya siku zijazo, hivyo ni vema kila nchi kushiriki kikamilifu kumaliza tatizo hilo.Hatuwezi kuendelea kusema mabaya mazuri na mazuri mabaya, bali ni wakati wa kushikamana kwa kufanyia kazi maazimio ambayo yanatolewa mara kwa mara,”ameeleza.

Ameongeza huwa wanajiuliza nani anafaidika na watu kuuwawa.Ukiangalia sababu kubwa ni watu kukosa utu na kuamua kuuwa watu bila kosa lolote, hivyo asasi za kiraia wapo tayari kushirikiana na kila mdau kuhakikisha vita inakwisha.

Akieleza zaidi katika mkutano huo amesema katika Mji wa Goma hali ni mbaya , hivyo ni wakati muafaka kwa kila mpenda haki kuungana na asasi za kiraia kuhakisha mauaji yanakoma.

Ameongeza kwamba wao asasi za kiraia hawana silaha silaha za moto za kukabiliana na waasi lakini kupitia mshikamano wa wananchi katika nchi hizo utasaidia kurejesha hali ya amani.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Asasi za Kiraia za Nchi za Maziwa Makuu, Joseph Butiku ametumia kikao hicho kutoa pongezi kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuwapokea viongozi wa EAC na SADC ili kutafuta suluhu ya mgogoro unaondelea DR Congo.

Butiku ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF ) amesema maamuzi yatakayotolewa na viongozi watayaunga mkono kwa sababu wanaamini yatamaliza vita hiyo na kufafanua DR Congo ni nchi kubwa na ina utajiri wa kutosha, ili amani na usalama ndio vitafanya wananchi wake kunufaika na rasilimali zilizopo.

Amesema kuwa Nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inapakana na nchi nyingi na matatizo ya vita vinavyoendel ea yamesababisha wengi kuikimbia nchi yao na tatizo hilo ni dharura ndio maana wamekutana jijini Dar es Salaam hapa kuwaonesha viongozi wetu kwamba tupo nao katika kutafuta suluhu.

“Niwapongeze viongozi wetu kwa kuona uzito wa jambo hili na tunampongeza Rais wetu, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuita wenzake nchini, aliombwa lakini amekubali kuzungumza tatizo hili, matumaini yetu watapata suluhu ya DRC iwe na amani,” amesema.

Awali Kennedy Walusala kutoka Asasi ya Kiraia nchini Kenya, a mauji ya watu 850 sio ya kufumbiwa macho hivyo wameamua kukutana kuzungumza an kujadiliana namna ambayo itawezesha DR Congo itapata amani na kwamba wao kama asasi za kiraia wanapambana kutafuta amani.

Ametumia nafasi hiyo kutoa rai vyombo vya habari na waandishi kufanya kazi kizalendo ili kuepuka utoaji wa habari zenye utata kwani hivi sasa vyombo vya habari kila wakati vinaonesha mauaji yanayoendelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mji wa Goma umeingia kwenye mapigano kati ya Waasi wa Kundi la M23 ambapo inadaiwa zaidi ya watu 850 wameuwawa kwa kipindi cha wiki moja.





Related Posts