Coastal Union, JKT TZ kazi ipo Arachuga

UHONDO wa Ligi Kuu Bara unaendelea tena leo kwa kupigwa mechi mbili za kukamilisha raundi ya 17, huku kazi kubwa ikiwa jijini Arusha na JKT Tanzania itakakuwa wageni wa Wagosi wa Kaya, Coastal Unuion kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini humo.

Mchezo mwingine wa leo ni wenyeji Singida Black Stars itakayoikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Liti, mkoani Singida, huku wageni ikitoka kufumuliwa mabao 4-0 na Yanga mechi ya kiporo wikiendi iliyopita jijini Dar es Salaam. Mechi zote mbili zitapigwa kuanzia saa 10:00 jioni.

Tuanzie na pambano la Arachuga baina ya Wagosi na maafande wa JKT, kila upande umetamba kutoka na ushindi ili kuzoa pointi tatu, ili kutoka eneo walililopo katika msimamo. Kabla ya mechi za jana Coastal ilikuwa nafasi ya 11, wakati JKT ikiwa ya nane zikitenganishwa na pointi moja tu, kwani Wagosi wana 18 na wageni wao wana 19, huku katika mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Dar es Salaam wagosi walipoteza kwa mabao 2-1.

Rekodi zinaonyesha katika mechi tisa za Ligi Kuu, Coastal imeshinda nne, huku Wagosi wakishinda mbili na zilizosalia ziliisha kwa sare tofauti, hali inayofanya mchezo wa leo kuwa mgumu kwa pande zote kama walivyokaririwa makocha wa timu hizo.

Kocha wa Coastal, Juma Mwambusi alisema maandalizi kwake yamekamilika, hivyo anaamini  timu itapata matokeo.

“Lengo letu ni kumaliza nafasi za juu hivyo ushindi wa kesho utatusogeza mbele,” alisema Mwambusi aliongeza JKT ni timu nzuri ina wachezaji wengi wenye uzoefu waliowahi pia kufanya makubwa kwenye mashindano ya Ligi Kuu Bara, hivyo mchezo hautakuwa mwepesi kwake ila amejipanga kutumia vyema uwanja wa nyumbani kuiadhifu kutokana na mapungufu yao ambayo amekuwa akiyaona.

Kocha wa JKT, Ahmad Ally alisema amefanya marekebisho katika kikosi kwa sehemu zote zilizokuwa na mapungufu hivyo anaamini watapata matokeo mazuri.

Katika mchezo wa Singida itakayokuwa nyumbani mjini Singida kuipokea Kagera kuna vita nyingine kwa timu hizo zinazokutana kwa mara ya nane Ligi Kuu baada ya awali kukutana mara saba na wenyeji kuwa na rekodi tamu zaidi.

Katika mechi saba za awali, Singida imeshinda mechi nne, huku Kagera ikishinda mbili na mmoja uliisha kwa sare na mara ya mwisho zilipokutana msimu huu, Singida ikiwa ugenini ilishinda 1-0, kitu kinachoifanya Kagera kupambana ili kutaka kulipa kisasi hicho.

Singida itaendelea kuwategemea nyota wake, akiwamo Elvis Rupia anayepambana kurejea katika orodha ya wafungaji baada ya kung’olewa na Clement Mzize wa Yanga mwenye mabao tisa (kabla ya mechi za jana), huku Mkenya huyo akiwa na manane.

Timu hiyo ina wachezaji wengine wakali wakiwamo wapya waliosajiliwa dirisha dogo kama Jonathan Sowah na Serge Pokou watakaoungaa na Victorien Adebayor aliyeanza kuitumikia mwishoni mwa duru la kwanza, huku Kagera ikimtegemea zaidi Moubarack Amza na Peter Lwasa kuichachafya ngome wa Singida.

Kocha wa Singida, David Ouma ametamba kushinda mchezo huo kutokana na maandalizi waliyoyafanya na hawana cha kupoteza uwanja wa nyumbani.

“Tutaingia kwa kumheshimu mpinzani wetu, tunaamini hautakuwa mchezo rahisi kutokana kila timu kuhitaji matokeo mazuri lakini kwa upande wetu maandalizi yamekwenda vizuri na wachezaji wapo kwenye hali nzuri,” alisema Ouma, huku kocha wa Kagera, Melis Medo akisisitiza dakika 90 zitaamua.

Kagera imekuwa na msimu mbaya ikiwa nafasi ya pili kutoka mkiani na pointi 12, huku Singida ikiwa nafasi ya nne ikichuana na vigogo, Simba, Yanga na Azam FC zilizopo juu yake.

Related Posts