Dk Mwinyi ataka uadilifu biashara mwezi wa Ramadhan

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewahimiza wafanyabiashara kujiandaa na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kufanya biashara kwa uadilifu na pia wawe na huruma kwa wananchi kwa kutopandisha bidhaa za vyakula kiholela.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo Februari 7, 2025 wakati akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu wa Masjid Jibril Mkunazini alipojumuika katika sala ya Ijumaa.

Amesema kumekuwa na kawaida na tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kupandisha bei za bidhaa wakati huo licha ya kwamba Serikali imekuwa ikipunguza ushuru katika Mwezi wa Ramadhani.

“Hakikisheni hampandishi bei za bidhaa kwani mnawapa mzigo mzito wananchi kwa kutomudu kununua bidhaa hizo muhimu bila sababu za msingi,” amesema.

Akizungumzia suala la uchaguzi mkuu ujao wa Rais, wabunge na madiwani, Dk Mwinyi amewasisitiza waumini hao na wananchi kwa ujumla kudumisha amani ili uchaguzi huo ufanyike kwa utulivu na amani.

Wakati huohuo, Rais wa Zanzibar Dk Mwinyi amefika Jamati la Jumuiya ya Ismailia Aga Khan Kiponda kusaini kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha Imamu wa 49 wa madhehebu wa Shia Ismailia, Mtukufu Aga Khan IV aliyefariki Februari 4, 2025 Lisbon, Ureno akiwa na miaka 88.

Related Posts