MAGARI mawili aina ya Buty ya rangi nyeusi yalikuwa yakielekea kiwanja cha ndege kumpokea mgeni wa shani kutoka Ethiopia, Myra Christopher Lee, binti wa bilionea wa Kiingereza Christopher Isaac Lee.
Mzee Christopher Lee, mmiliki wa kiwanda kikubwa cha saruji kilichopo Dar alikuwa na viwanda vingine vya saruji katika nchi za Ethiopia, Ghana na Afrika Kusini.
Huko England kampuni yake ndiyo iliyokuwa ikiunda magari aina ya Buty ambayo pia ilikuwa ikiunganisha magari ya aina hiyo nchini Afrika Kusini.
Mzee Christopher Lee katika ujana wake aliwahi kuishi Dar es Salaam wakati baba yake alipokuwa balozi wa Uingereza hapa nchini katika miaka ya nyuma.
Mtoto wa kwanza wa kiume wa mzee Christopher Lee, Isaac Lee ndiye aliyekuwa akisimamia kiwanda cha saruji kilichoko Dar akiwa afisa mkuu wa kiwanda hicho. Mdogo wake wa kike Myra Christopher aliyekuwa akisoma Marekani alikuwa anazuru viwanda vya baba yake vilivyopo Afrika kuanzia vile vilivyoko Afrika Kusini, Ghana, Ethiopia na Dar es Salaam. Alishatembelea Afrika Kusini, Ghana na Ethiopia. Sasa alikuwa anakuja Tanzania.
Ndege aliyopanda ilikuwa inafika saa sita mchana. Kaka yake Isaac Lee ndiye aliyekuwa mwenyeji wake ambaye angempokea kiwanja cha ndege cha Dar es Salaam.
Akiwa kwenye Buty iliyomtangulia mwenzake, Isaac alifahamu alikuwa amebakisha nusu saa kwa ndege iliyompakia Myra kutua katika kiwanja cha ndege.
Alishampangia chumba kwenye hoteli ya kifahari ambapo angekaa siku atakazokuwa hapo Dar.
Nyuma yake kulikuwa na Buty nyingine ambayo ilikuwa na dereva na ilikuwa maalumu kumpakia Myra na kumpeleka katika hoteli atakayofikia.
Wakati wanakikaribia kiwanja cha ndege, Isaac aliona polisi wawili wa usalama barabarani wakimpungia mkono kumsimamisha. Pia aliona Land Rover jeupe lililokuwa limeegeshwa kando ya barabara.
Isaac alipunguza mwendo na kulisimamisha gari pembeni mwa barabara. Gari lililokuwa nyuma yake nalo likasimama. Polisi hao wawili mmoja alilifuata gari alilokuwa akiendesha Isaac na mwenzake alilifuata gari lililokuwa nyuma yake.
Polisi hao waliwambia Isaac na dereva wa gari la nyuma yake washuke kwenye magari. Waliposhuka watu hao walishituka walipowaona polisi hao wakichomoa bastola na kuwaamuru waongoza njia kuelekea walipoliegesha gari lao.
Walipofika kwenye gari hilo kulishuka watu wawili waliovaa kiraia ambao waliyafuata magari yaliyosimamishwa. Mtu mmoja aliingia katika gari alilokuwa akiendesha Isaac na mwingine alijipakia kwenye gari la nyuma yake. Wakaondoka na magari hayo haraka haraka.
Isaac na dereva wake walipakiwa katika Land Rover walilohisi halikuwa la polisi. Land Rover hilo liligeuza njia na kurudi nyuma.
Jijini London, Uingereza, saa nane kamili kwa saa za Afrika Mashariki, mzee Christopher Lee alikuwa akijiandaa kuondoka ofisini kwake, simu yake ilipoita kwenye mtandao wa WhatsApp. Aliona namba ya mwanawe Myra ikiwa hewani. Akafahamu kwamba Myra alikuwa ameshawasili Tanzania na kwamba alitaka kumfahamisha kuwa amefika salama. Akaipokea simu na kuiweka sikioni.
Badala ya kusikia sauti ya kike ya mwanawe alisikia sauti kavu ya kiume.
“Natumaini unafahamu Kiswahili na tutaongea kwa Kiswahili.”
“Wewe nani?” Mzee Christopher Lee aliuliza kwa taharuki.
“Sisi ni watekaji. Tumemteka mwanao Myra kiwanja cha ndege alipowasili Dar es Salaam akitokea Ethiopia. Ana siku saba za kuishi. Tunataka Dola milioni mia moja ili tumuachie kwa usalama….”
Simu ikakatwa. Christopher Lee alishituka na alitaka kujua watekaji hao walikuwa wapi na mwanawe lakini simu ilikuwa imeshakatwa. Akapiga namba ya Myra. Data ilikuwa imeshazimwa.
Alipoingia katika eneo la WhatsApp aliona alikuwa ametumiwa picha ya mwanawe akiwa amefungwa kamba mikono na miguu kwenye chumba kidogo huku mitutu mwili ya bunduki imeelekezwa kichwani mwake na watu wawili waliojiziba nyuso kwa vitambaa. Chini ya picha kulikuwa na maneno yaliyosema.
“Baba okoa maisha yangu.”
Christopher Lee alifahamu Myra alikuwa apokewe na kaka yake Isaac. Sasa ni kitu gani kimetokea? Akajiuliza bila kupata jibu. Akaamua kumpigia Isaac. Simu ikapokewa haraka.
“Isaac yuko mikononi mwetu. Tulimteka ili kufanikisha mpango wetu wa kumteka nyara Myra. Lakini huyu tutamuachia…”
“Ninyi ni kina nani?” Christopher Lee aliuliza kwa taharuki.
Hakukuwa na jibu. Simu ikakatwa. Namba ya Isaac na Myra zikawa hazipatikani.
Akiwa ametaharuki na akiliona tukio zima kama ndoto mzee Christopher Lee alimpigia Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Augustino Niwako.
“Mheshimiwa waziri. Habari yako,” alimsalimia waziri baada ya kupokea simu yake.
“Nzuri. Sijatambua naongea na nani.”
“Unaongea na Christopher Lee, mwekezaji wa kiwanda cha saruji kutoka London.”
“Oh nimekupata. Mzee Lee habari za siku.”
“Si nzuri. Nimepata taarifa sasa hivi kwamba wanangu wawili wametekwa nyara huko Dar es Salaam. Unayo taarifa hiyo?”
“Ndiyo nimeingia ofisini sasa hivi, sina taarifa yoyote. Ni wanao gani waliotekwa?”
“Mwanangu Myra ambaye alikuwa anasoma Marekani na alikuwa na ziara nchini Tanzania. Alifika Dar es Salaam saa sita kwa saa za huko. Muda mchache uliopita simu yake imetumika kuelezwa kwamba ametekwa nyara na yuko mikononi mwa watekaji. Nikampigia kaka yake ambaye ni afisa mkuu wa kiwanda chetu cha saruji, simu ikapokewa na watu hao hao wakanifahamisha kwamba na yeye wamemteka nyara ili kufanikisha zoezi la kumteka Myra. Ninashangaa unaponiambia kuwa huna taarifa wakati mimi nimeshaipata taarifa huku.”
“Huenda si taarifa za kweli lakini nitampigia mkuu wa jeshi la polisi atanifahamisha kama kuna tukio kama hilo.
“Si taarifa za kweli? Hao watu wamepataje namba za simu za wanangu?”
“Unasikia mheshimiwa. Subiri kwanza nimuulize mkuu wa jeshi la polisi halafu nitakupigia simu kukupa uhakika.”
Christopher Lee akakata simu. Baada ya kukata simu waziri akampigia mkuu wa jeshi la polisi Inspekta Jenerali Damian Lymo.
“Habari ya mchana IGP Lymo?”
“Nzuri mheshimiwa. Kuna taarifa yoyote?”
“Kuna tukio gani limetokea huko?”
“Mpaka sasa tuko shwari. Kama kuna tukio sijapata taarifa.”
Waziri akamueleza taarifa aliyoipata kutoka London.
“Kama kuna tukio kama hilo mkurugenzi wa upelelezi atakuwa anafahamu. Niache nimpigie halafu nitakujulisha.”
Simu ya waziri ilipokatwa, IGP Lymo akampigia mkurugenzi wa upelelezi Amir Fakih.
“Nimesikia kuna watu wametekwa nyara uwanja wa ndege.”
“Sijapata taarifa bado. Kama tukio kama hilo lingetokea ningeshaarifiwa.”
“Huenda watekaji wamelifanya kimya kimya ili lisiingie mikononi mwa polisi. Fanya uchunguzi wa haraka.”
Dakika chache baadaye kachero Inspekta Temba wa idara ya upelelezi makao ya polisi aliitwa na mkurugenzi wa upelelezi.
Alipoingia ofisini humo, mkurugenzi wa upelelezi alimuuliza.
“Una kazi gani kwa hivi sasa?”
“Bado ninaendelea kuwahoji wale mahabusi wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya polisi wa benki ili kuandaa ushahidi.”
“Iache kazi hiyo. Nimepata taarifa kwamba binti wa Bilionea Christopher Lee ambaye ni mwekezaji hapa nchini anayemiliki kiwanda kikubwa cha saruji ametekwa nyara na watu wasiojulikana kiwanja cha ndege wakati anawasili kutoka Ethiopia. Kadhalika afisa mkuu wa kiwanda hicho ambaye alikuwa anakwenda kumpokea naye ametekwa. Ninataka uende kiwanja cha ndege ukathibitishe habari hizo.”
Alipoondoka makao ya polisi Temba alikwenda moja kwa moja kiwanja cha ndege. Aliposimamisha gari kwanza alikwenda kituo cha polisi cha kiwanjani hapo.
“Kuna taarifa gani hapa?” Temba aliwauliza polisi aliowakuta kaunta.
“Taarifa ni za kawaida tu. Bado hakujakuwa na tukio lolote la kushitua.”
“Tumepata taarifa makao makuu ya polisi kwamba kuna utekwaji wa mtu mmoja aliyekuwa anatoka Ethiopia.”
“Ndiyo unatueleza wewe. Hilo tukio hatujalisikia au niseme halijaripotiwa kituoni kwetu lakini ni kweli kwamba ndege iliyotoka Ethiopia ilitua kiwanjani hapa saa sita mchana.”
Temba hakutosheka na maelezo aliyoyapata kituoni hapo aliingia ndani ya kiwanja na kuanza dodosa dodosa.
Kwanza alitaka kujua kama ndege ya kutoka Ethiopia iliwasili. Baada ya kupata jibu kwamba ndege hiyo iliwasili saa sita, alitaka kukagua orodha ya abiria waliokuwamo katika ndege hiyo. Baada ya kuisoma orodha hiyo aliliona jina la Myra Christopher Lee.
Hata hivyo, Temba alithibitishiwa kwamba abiria wote waliondoka kwa usalama.