Dar es Salaam. Matukio ya wasichana wenye umri mdogo kupevuka (kuvunja ungo) ni ya kawaida katika miaka ya hivi karibuni.
Kutokana na hili, wasiwasi pia umekuwa ukiongezeka miongoni mwa wazazi.
Kuna ushuhuda mwingi wa baadhi ya wazazi, wanaosema watoto wao wa kike wamepevuka wakiwa na miaka minane mpaka 12, tofauti na umri sahihi unaotakiwa ambao kiwastani ni miaka 14.
“Watoto hawa wa kike katika umri huo hata hawaelewi kinachoendelea. Jinsi ya kuweka sodo (pedi) na kwa nini lazima waivae na jinsi gani wanaweka viungo vya ndani safi! Hawajui mengi kuhusu mambo hayo,” anasema mkazi wa Magomeni Mapipa, Hellen Sanga (49), mama wa watoto watano.
Hellen, anayekiri kupevuka akiwa na miaka 15, anasema wakati huo ilikuwa kawaida kwa umri huo, tofauti na binti zake wawili ambao walipevuka mapema.
“Msichana wangu wa kwanza ni mtoto wa tatu kuzaliwa, alipovunja ungo nilishtuka. Nilipigiwa simu na mwalimu wake wa darasa, alikuwa la tano akiwa na miaka minane. Wa pili angalau alifikisha miaka 11, lakini huyu wa tatu amevunja ungo na miaka minane pia,” anasimulia Hellen.
Mkazi wa Tegeta, Rehema Omary anasema: “Miaka tunakua, sisi tulichelewa kupevuka. Binafsi nimevunja ungo nikiwa na miaka 17. Leo unakutana na binti ana miaka 12 matiti yalishachomoza, ukimuangalia utadhani ana miaka 19, binti mdogo tumbo hilo. Mtoto wa kiume miaka 14 tayari ana sauti nzito.”
Sababu kuvunja ungo mapema
Wakati hali hiyo ikitajwa, wataalamu wa afya wameainisha sababu kadhaa zinazochangia wasichana wenye umri mdogo, kupevuka mapema na namna ya kudhibiti hali hiyo.
Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Nathanael Mtinangi anasema licha ya kwamba hakuna sababu ya moja kwa moja, msichana kupevuka mapema husababishwa na mambo kadhaa.
Anataja baadhi kuwa ni makuzi na mazingira, akisema hivyo vitu vinaweza kutofautiana.
Anatoa mfano miaka ya zamani wanawake, hasa vijijini walipevuka kuanzia miaka 14 mpaka 16, lakini maisha yanabadilika.
Kwa mujibu wa Dk Mtinangi, maisha yanabadilika, vyakula vinabadilika na hali ya hewa halikadhalika, huku akitaja kubadilika kwa mtindo wa maisha wa binadamu ambako kumefanya watoto wa kike kupevuka mapema.
“Unakuta mtoto anakuwa mnene akiwa na umri wa kabla ya kuvunja ungo, zamani kumpata msichana mnene sana wa umri wa miaka saba mpaka 12 ilikuwa nadra, sasa hivi vyakula wanavyokula wananenepa mapema.
“Vyakula vimebadilika, mazao tunayovuna tunapanda kwa mbegu zisizo asili, maisha yamebadilika, kwa hiyo kubadilika sana kwa mtindo wa maisha ya binadamu, kunaweza kuwa kumeleta mabadiliko ya binadamu pia,” anasema.
Dk Mtinangi, ambaye ni mkuu wa kitengo cha magonjwa na kinamama na uzazi Muhimbili, anasema hata kuota matiti wasichana kwa sasa wanaanza mapema ikilinganishwa na hapo awali.
“Zamani vijijini kwetu huko maisha ya babu zetu miaka 12 kwenda 14 ndiyo wasichana walianza kuchomoza matiti, yanaanza kuonekana, kubadilika kwa mtindo wa maisha ya binadamu, kubadilika kwa vitu na hali ya hewa, binadamu wa mwaka 1800 au 1900 siyo sawa na binadamu aliyezaliwa miaka ya 2000,” anasema Dk Mtinangi.
Dk Mtinangi anasema umri sahihi wa kupevuka kwa msichana ni miaka 14 na kwamba anaweza kwenda mpaka miaka 16 au akashuka miaka 13, kwa sababu mtoto wa kike anapozaliwa mwili una mabadiliko kwa viungo vya ndani na nje.
Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama, Isaya Mhando anasema mfumo wa kawaida wa kuvunja ungo, kitaalamu ‘menarche’ ni hali ya mwanamke kuona damu ya hedhi kwa mara ya kwanza.
Anasema kuna sababu nyingi, lakini mzunguko wa hedhi huanzia kwenye ubongo, kuna tezi ambazo hupokea homoni kutoka kwenye ubongo, ikipokea nayo hutoa taarifa kupitia homoni nyingine ambayo huenda kusisimua mayai.
Anasema homoni hizo ni za aina mbili, moja husisimua mayai yakue. Yanapokua ndiyo yanatoa homoni nyingine inayokuja kusisimua ukuta wa mimba, kwa hiyo hapo ndipo msichana anapopevuka.
Hata hivyo, Dk Mhando anasema si kila msichana anapoona damu hiyo huwa amepevuka au damu hiyo imetokana na hiyo homoni.
“Kuvunja ungo na kukomaa, hatua ya pili ni kuona nywele sehemu za siri na kuona matiti. Lakini kule kuona nywele na kuona matiti haitegemei, mtoto anaweza kuwa na mafuta mengi akaona matiti kwa sababu mafuta hutengeneza homoni ambayo inaweza kusisimua ukuta wa mimba na kuona damu.
“Kuwahi kuona damu kabla ya wakati wake, inaweza kusababishwa na unene uliopindukia au na matatizo mengine ya tezi ambayo yanaweza kuleta madhara kwa msichana,” anasema.
Dk Mhando anasema hali hiyo huonyesha kuwa mtoto anaweza kuwa na matatizo ya saratani ya mayai, inayosababisha kutolewa kwa homoni nyingi, akapata hali ya kutoka kwa damu mithili ya hedhi na hali hiyo huwapata wasichana kadhaa.
Kwa mujibu wa daktari huyo, tatizo kubwa ni mtindo wa maisha, lishe, aina ya vyakula wanavyokula pia husababisha utengenezwaji wa homoni nyingi kwa watoto, hali inayosababisha kupevuka kabla ya umri wake.
Pamoja na hali hiyo, Dk Mhando anasema msichana aliyeona hedhi kabla ya wakati anaweza kupatiwa tiba, ikiwa atapitia mfumo wa vipimo vyote.
“Anaangaliwa sababu ya hiyo hali, kama ni saratani au uvimbe pia inaangaliwa. Ikibainika hana changamoto yoyote, anaweza kuchomwa sindano hiyo kila mwezi kwa kipindi cha miezi sita, pamoja na dawa za homoni, kisha huja kupevuka wakati wake ukifika,” anasema.
Hata hivyo, anatoa ushauri kwa wazazi kuzingatia afya iliyo bora kwa watoto wa kike, ikiwemo kufanya mazoezi na kula lishe bora.
“Sababu kubwa ni lishe na ulaji kupindukia na kingine hawafanyi mazoezi, wanapelekwa shule na magari na wakirudi hawashughulishi mwili,” anaeleza.
Alipoulizwa iwapo msichana atapevuka mapema inamaanisha ukomo wa hedhi nao utakuja kuwa mapema, Dk Mhando anasema:
“Hiyo inatokana na sababu nyingine, si lazima wapate menopause (kukoma kwa hedhi) mapema. Ila unapovunja ungo mapema maana yake ni kwamba mwanamke hujiweka katika nafasi kubwa ya saratani za mayai, kizazi, shingo ya kizazi na zingine zitokanazo na homoni.”
Utafiti uliofanywa wa hivi karibuni uliochapishwa Mei 29, 2024 umeonyesha umri wa wastani wa kupata hedhi ya kwanza, umekuwa ukipungua miongoni mwa vizazi vya hivi karibuni nchini Marekani.
Umri huo umekuwa ukipungua hasa kwa watu wa hali ya chini kiuchumi, kwa mujibu wa utafiti mpya ulioongozwa na watafiti kutoka Shule ya Afya ya Umma ya Harvard T.H. Chan.
Utafiti huo pia umegundua kuwa muda unaohitajika kwa mzunguko wa hedhi kuwa wa kawaida, unaongezeka.
Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la JAMA Network Open ni chapisho la hivi punde kutoka kwa Apple Women’s Health Study, utafiti wa muda mrefu kuhusu mizunguko ya hedhi, magonjwa ya wanawake, na afya ya wanawake kwa ujumla.
“Matokeo yetu yanaweza kusaidia kuelewa vyema afya ya hedhi katika kipindi chote cha maisha na jinsi mazingira yetu ya kuishi yanavyoathiri ishara hii muhimu ya mwili,” alisema Shruthi Mahalingaiah, mtafiti mwenza mkuu na profesa msaidizi wa afya ya mazingira, uzazi na wanawake katika Shule ya Harvard Chan.