Ikanga Speed hakijaeleweka Yanga, azua maswali

KABLA ya kutimka kwa aliyekuwa kocha wa Yanga, Sead Ramovic alikuwa alimkalia kooni winga mpya wa timu hiyo, Jonathan Ikangalombo ‘Ikanga Speed’ na kuibua maswali itakuwaje baada ya jamaa kusepa?

Hata hivyo, Ikanga Speed amebaki kidogo tu kabla ya kuanza kuliamsha Jangwani kwani baada ya kumaliza programu ya kupunguza uzito, sasa ameanza kuuchezea mpira.

Mwanaspoti imepenyezewa, katika mazoezi ya Yanga, Ikanga Speed anagusa mpira kwa muda mchache sana lakini sehemu kubwa ya mazoezi yake ni kukimbizwa kwa mbio za viwango tofauti baada ya makocha wake kushtukia kitu.

Ikanga hakucheza takribani miezi mitatu akipambana kutaka kusitisha mkataba ili aondoke AS Vita hatua ambayo Ramovic na jopo lake la walimu wa mazoezi hasa wale wa utimamu wa mwili, waliona kama ameongezeka uzito kidogo na baada ya hapo alipewa kocha wa utimamu wa mwili ambaye ndiye anayepambana naye kumweka sawa.

Hata hivyo, wiki hii winga huyo alianza kupewa muda mchache wa kucheza mpira na akaanza kuonyesha ubora wake akijua kuwakimbiza mabeki na kupambana na nguvu huku pia akiwa na kasi ya kwenda langoni.

Siku moja kabla ya Ramovic kuachia ngazi kocha huyo akizungumzia Ikanga alisema winga huyo bado anaendelea kuandaliwa ili kuepusha asiumie endapo atawahishwa kucheza kwenye kikosi hicho.

“Jonathan (Ikangalombo) ni mchezaji mzuri, jambo la kwanza tunalopaswa kufanya, bila shaka ni kumfikisha katika kiwango cha utimamu wa mwili tunachotaka kwa sababu si tu kuhusu utimamu wake wa mwili bali pia kuhakikisha hapati majeraha,” alisema Ramovic na  kuongeza;

“Ikiwa hana kiwango sahihi cha utimamu wa mwili na anahitaji kukimbia kwa kasi kwenye mechi, Kuna uwezekano mkubwa wa kuumia na hilo ndilo tunalotaka kupika.”

Winga huyo amezua taharuki na tangu asajiliwe dirisha dogo hajaonekana kwenye mechi yoyote zaidi ya kukaa  jukwaani hatua ambayo mashabiki wa Yanga walianza kupata wasiwasi.

Hata hivyo, winga huyo bado anaonekana atapita njia hiyo hiyo chini ya kocha mpya wa Yanga Miloud Hamdi ambaye naye ni muumini mzuri wa utimamu wa kiwango kikubwa wa mwili.

Related Posts