Kitendo cha mwamuzi Abel William wa Arusha jana kumuonyesha kadi mbili (ya njano na nyekundu) kwa pamoja kipa wa Fountain Gate, John Noble katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyomalizika kwa sare ya 1-1 dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Februari 6, 2025, kimezua mijadala mikali katika mitandao ya kijamii kama ni tukio sahihi ama alikosea.
Mwamuzi Abel alionekana akikimbia kwa kasi kumfuata kipa huyo huku akiwa ameinua juu mikono yake yote miwili kila mmoja ukiwa na kadi wakati alipoenda kumwadhibu mlinda mlango huyo kwa makosa mfululizo ya kupoteza muda katika mechi hiyo ambayo ililazimika kuchezwa kwa dakika 90+14.
Hata hivyo, Abel sio mwamuzi wa kwanza kuinua juu kadi zote mbili kwa pamoja wakati wa mechi. Haya hapa matukio ya waamuzi kutoa kadi zilizozua utata duniani:

1. Mmoja njano, mwingine nyekundu
Lazio ilipoteza dhidi ya AC Milan katika mechi ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) iliyochezwa Machi 1, 2024 huku wachezaji wake watatu wakitolewa kwa kadi nyekundu.
Luca Pellegrini alikuwa wa kwanza kutolewa nje baada ya kumfanyia rafu Christian Pulisic, jambo lililomfanya aonyeshwe kadi ya pili ya njano.
Noah Okafor alifunga bao la ushindi kwa AC Milan katika dakika ya 88 kwa shuti kali kutoka yadi 16, baada ya kipa Ivan Provedel kufanya makosa mawili katika kuokoa.
Katika muda wa nyongeza, Lazio walipoteza wachezaji wawili zaidi kwa kadi nyekundu za moja kwa moja. Adam Marusic alitolewa kwa kumbwatukia mwamuzi, huku Matteo Guendouzi akitolewa nje baada ya kumsukuma Pulisic chini kwa hasira, kufuatia kufanyiwa rafu na mshambuliaji huyo wa zamani wa Chelsea.
Staa wa zamani wa Arsenal, Guendouzi kwanza alichezewa faulo na Pulisic, kwa hasira (Guendouzi) akamvuta na kumbaga chini Mmarekani huyo. Kwa kuonyeshana ubabe huo, mwamuzi alitoa kadi nyekundu kwa Guendouzi aliyoishika katika mkono wake wa kushoto huku mkono wa kulia akishika ya njano aliyomuonyesha Pulisic.

Lazio walimaliza mechi wakiwa na wachezaji wanane tu uwanjani. Mechi hiyo ilikuwa na mvutano mkubwa, huku wachezaji sita wa AC Milan wakipewa kadi za njano, na wachezaji wengine watatu wa Lazio pia wakiwa na onyo.
2. Kadi zote mbili mkono mmoja
Robin van Persie alilimwa moja ya kadi nyekundu za utata zaidi katika historia ya soka wakati Arsenal alipocheza dhidi ya Barcelona katika Ligi ya Mabingwa mnamo Machi 8, 2011.
Arsenal ilikuwa na uongozi wa mabao 2-1 baada ya kushinda mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Emirates, lakini hali ilibadilika katika mechi ya marudiano kwenye Uwanja wa Camp Nou.
Lionel Messi aliitanguliza Barcelona kwa bao 1-0 muda mfupi kabla ya mapumziko kwa bao maridadi. Arsenal walirudi mchezoni baada ya Sergio Busquets kujifunga na kuwapa Gunners faida ya mabao 3-2 kwa jumla.
Hata hivyo, dakika chache baadaye tukio tata lilitokea. Van Persie alijikuta anaelekea kumkabili kipa Victor Valdes wa Barca, lakini alipiga shuti nje kwa mguu wake dhaifu. Mwamuzi Massimo Busacca alimshangaza mshambuliaji huyo wa Uholanzi kwa kumlima kadi ya pili ya njano na kumtoa nje kwa kadi nyekundu. Mjadala mwingine ulikuwa ni vile mwamuzi alivyozishika kadi zote mbili katika mkono mmoja, nyekundu ikiwa juu na ya njano ikiwa katika vidole alivyovikunja vya mkono huo huo.
Mwamuzi alimwadhibu Van Persie kwa kupiga shuti ilhali filimbi ilishapulizwa, lakini Van Persie alidai kuwa hakusikia filimbi hiyo kutokana na kelele za mashabiki 95,000 waliokuwa uwanjani. Licha ya malalamiko yake, Van Persie alitolewa nje, jambo lililobadilisha kabisa mwelekeo wa mechi na kuwa moja ya maamuzi yenye utata zaidi katika historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Arsenal ikafa 3-1.

3. Kadi Tatu kwa Mchezaji Mmoja
Katika mechi kati ya Croatia na Australia kwenye Kombe la Dunia 2006, mwamuzi Graham Poll alimwonyesha mchezaji wa Croatia, Josip Simunis, kadi ya njano mara tatu kabla ya kumtoa nje kwa kadi nyekundu. Kwa kawaida, mchezaji anapaswa kutolewa nje baada ya kadi mbili za njano.
Picha zima lilikuwa hivi: Awali, Simunic alionyeshwa kadi ya njano na mwamuzi Graham Poll katika dakika ya 61 kwa kumfanyia rafu Harry Kewell.
Katika dakika ya 90, Poll tena alimwonyesha Simunic kadi ya njano kwa rafu nyingine, lakini hakufuata utaratibu wa kutoa kadi nyekundu ambayo ilikuwa ya lazima baada ya kadi ya pili ya njano, akionekana kwamba alisahau.
Katika dakika ya 90+3, baada ya Poll kupuliza filimbi ya mwisho, Simunic alimfuata mwamuzi kwa hasira na kumsukuma. Poll kisha akampatia Simunic kadi ya tatu ya njano na mara moja akamwonyesha kadi nyekundu.
Tukio hili lilimgharimu Poll, kwani hakuruhusiwa tena kuchezesha mechi za kimataifa baada ya Kombe hilo.

4. Njano mbili tukio moja
Kadi nyekundu ya kushangaza alionyeshwa kiungo wa Chris Baird katika mechi ya kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Ulaya (Euro) kati ya Ireland Kaskazini na Hungary baada ya nyota huyo kufanya makosa mawili yanayostahili kadi ya njano ndani ya sekunde saba katika dakika ya 81.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Septemba 7, 2015, kiungo huyo wa Ireland ya Kaskazini na Derby County alionyeshwa kadi mbili za njano na mwamuzi wa Kituruki, Cuneyt Cakir, kwa makosa mawili yaliyofuatana – ingawa mchezo haukusimama baada ya tukio la kwanza.
Akiwa mbele ya mwamuzi, Baird alimchapa kiatu mchezaji wa Hungary, lakini kwa kuwa mpira ulikuwa bado katika umiliki wa Hungary, refa akaachia advantage pale Hungary walipokuwa wakifanya shambulizi la kaunta, lakini Baird akaja mbio na kumchapa tena kiatu mchezaji wa upinzani kuzuia shambulizi hilo. Hapo ndipo refa Cakir alipomwonyesha kadi ya kwanza ya njano kisha akamwonyesha ya pili ya njano na kisha akammalizia na nyekundu, huku akimfafanulia kwa ishara ya vidole inayotafsirika kama “ulicheza faulo ya njano pale na kisha umecheza faulo nyingine ya njano hapa, hivyo unakula na red.”
Baada ya kumalizika kwa mechi hiyo ya kufuzu fainali za Euro iliyochezwa kwenye Uwanja wa Windsor Park, kocha wa Ireland Kaskazini, Michael O’Neill alisema uamuazi haukuwa sahihi kwa sababu kama Baird angejua kwamba alikuwa tayari amepewa kadi ya njano kwa rafu ya kwanza, basi asingefanya kosa la pili.
“Sijawahi kuona mchezaji akipewa kadi mbili kwa tukio moja, hii ni mpya kwangu,” alisema O’Neill. “Nilimwambia mwamuzi, ‘sikubaliani na hili’.”
“Chris asingefanya rafu ya pili kama angejua tayari ameonywa kwa tukio la kwanza. Kwa hiyo, ni hali ya kushangaza kuona jambo kama hilo, na sijawahi kulishuhudia kabla.”
5. Hamburger SV vs Fortuna Dusseldorf – Bundesliga ya Pili
Katika mechi ya Hamburger SV dhidi ya Fortuna Dusseldorf iliyochezwa Septemba 29, 2023 kwenye Uwanja wa Volksparkstadion huko Hamburg, mchezaji Matthias Zimmermann wa Fortuna Düsseldorf alionyeshwa kadi ya pili ya njano, kisha kadi nyekundu na mwamuzi Felix Zwayer. Tukio lililozua gumzo ni namna mwamuzi alivyozishika kadi zote mbili katika mikononi yake.
Refa wa zamani, Osmani Kazi ametoa ufafanuzi kuhusu kitendo cha mwamuzi Abel William kuinua juu kadi mbili kwa wakati mmoja katika mchezo wa jana wa Ligi Kuu Bara ambao uliing’oa Simba kileleni mwa msimamo, akisema ni tukio ambalo halina makosa yoyote.
“Hamna shida yoyote kufanya vile,” alisema Kazi na kuongeza: “Lakini inakuwa vizuri mwamuzi akitanguliza kadi ya pili ya njano na kisha kutoa nyekundu.”