Kibano watumishi wa ardhi Dodoma

Dodoma. Bunge limeitaka Serikali ifanye tathmini na uhakiki wa huduma zinazotolewa na kila mtumishi katika ofisi ya ardhi jijini Dodoma, ili kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wasio waaminifu.

Azimio hilo limefikiwa bungeni leo Februari 7, 2025 baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mnzava kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kamati hiyo kwa mwaka unaoishia Februari 2025, ikibainisha uwepo wa migogoro mingi ya ardhi.

Baada ya kusoma maazimio hayo Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliwahoji wabunge iwapo wanaafiki azimio hilo, wengi walijibu kwa sauti ya ‘Ndiyoo’.

Awali akiwasilisha taarifa, Mzava amesema Jiji la Dodoma ni miongoni mwa sehemu zenye migogoro mingi ya ardhi nchini, hivyo kamati iliitaka Serikali kuwasilisha hatua ilizochukua kukabaliana na changamoto hiyo.

Amesema baada ya Serikali kuwasilisha taarifa katika uchambuzi, kamati ilibaini kuwapo vyanzo mbalimbali vya migogoro, ikiwemo utaratibu wa uendelezaji mji kwa njia ya maboresho, uliotekelezwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA).

Amesema utaratibu huo haukutambua ardhi tupu kuwa na thamani, hivyo kutwaa sehemu kubwa ya ardhi ya wenyeji bila kuwafidia.

Amesema kulikuwa na udhaifu katika usimamizi na utekelezaji miradi ya urasimishaji makazi, katika maboresho ya makazi na upimaji shirikishi, ambako pia kulikosekana uwazi.

Mzava amesema wananchi wengi wanadai kudhulumiwa ardhi na baadhi ya watendaji walioendesha mpango huo.

Amesema sababu nyingine ni utwaaji, upangaji na upimaji wa ardhi katika miradi ya Serikali kufanyika bila kulipa fidia. Katika utekelezaji wa miradi ya uwanja wa mpira Nala, mradi wa barabara ya mzunguko (ring road) na reli ya kisasa (SGR) wananchi bado wanadai fidia ya maeneo yao.

“Baadhi ya watumishi kutokuwa waadilifu, wamekuwa wakitoa miliki pandikizi (double allocation) na kuchelewesha huduma za ardhi kwa wananchi ili kuvutia rushwa,” amesema.

Amesema Serikali imechukua hatua kadhaa ikiwemo kampeni ya ya ‘Zero migogoro Jiji la Dodoma’ mwaka 2021, kuunda kamati ya utatuzi wa migogoro ya ardhi mwaka 2022 na kuendesha kliniki za ardhi mwaka 2023.

Mzava amesema pamoja na hatua hizo kutatua sehemu ya migogoro, bado Jiji la Dodoma limeendelea kuwa na mingine mingi.

Kamati pia imebaini migogoro mingi ni zao la watumishi wa sekta ya ardhi wasio waamini wanaoshirikiana na walanguzi katika sekta ya ardhi, ili kujitajirisha kinyume cha sheria.

“Kwa hiyo, Bunge linaazimia kuwa, Serikali ihakikishe miamala yote ya ardhi katika Jiji la Dodoma inafanyika katika Mfumo wa e-Ardhi ambao tayari unafanya kazi katika jiji hilo,” amesema.

Wakati huohuo, baada ya taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Maji na Mazingira kuwasilishwa, Bunge limeazimia mambo manne kuhusu upatikanaji na usambazaji wa maji katika majiji sita, ikiwemo mamlaka za maji kushirikiana na kubadilishana uzoefu.

Majiji hayo ni Dodoma, Dar es Salaam, Tanga, Mbeya, Mwanza na Arusha.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jackson Kiswaga akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kamati kwa mwaka unaoishia Februari 2025, amesema majiji hayo yameendelea kuwa na changamoto mbalimbali zinazokwamisha utendaji wa mamlaka za maji nchini.

Alipendekeza wizara zishirikiane na kuchukua hatua madhubuti kudhibiti ujenzi wa makazi holela kwa kuzingatia kanuni za mipango miji ili kuwezesha uwepo wa miundombinu muhimu kama vile ya majisafi na majitaka katika maeneo yote yaliyopangwa.

“Bunge linaazimia mikakati endelevu ibuniwe na kutekelezwa kuhakikisha maeneo yote yenye vyanzo vya maji au miundombinu ya maji iliyokamilika yanapata maji ili kuleta tija ya fedha zilizowekezwa na Serikali,” amesema.

Kiswaga ametaka Serikali ihakikishe huduma ya maji katika maeneo yote ya umma zinapatikana wakati wote, ili kukidhi mahitaji ya wananchi na kuchukua tahadhari juu ya magonjwa ya mlipuko katika maeneo hayo.

Related Posts