KILOSA WAANZA KUNUFAIKA NA BIASHARA YA HEWA UKAA

FARIDA MANGUBE, KILOSA MOROGORO

MKUU wa Wilaya ya KIlosa, Shaka Hamdu Shaka, amewataka wakazi wa wilaya hiyo kujikita katika biashara ya hewa ukaa, kutambua kuwa ni moja miongoni mwa njia mkakati za ukombozi kwao kuanzia ngazi ya vijiji na halmashauri.

Ameyasema hayo wakati akifungua na kuiongoza kikao cha kamati ya uvunaji misitu kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Amesema kwa sasa utajiri mkubwa upo katika biashara hiyo na kusema mfano umeonekana baada ya kazi kubwa iliyofanyika matokeo yake wameanza kuyaona.

Amefahamisha kuwa waliingia katika majaribio na kuangaliwa kama wanaweza kufanya biashara hiyo wakapiga hatua, anaamini watakwenda kuwa mfano mzuri wa kusimamia rasilimali zilizopo katika wilaya hiyo.

“Ninaimani sana na ninyi kwamba mtakwenda kufanya mageuzi ya kulinda na kutunza rasilimali tulizonazo ili tija iweze kuonekana, lazima tukiri kwamba bado tunachangamoto, mfano mzuri ni migogoro kati ya kijiji na kijiji, kamati za maliasili za kijiji fulani kuvamia kijiji fulani.

“Tunajivunia mafanikio haya tulidhamiria na kuhakikisha tunatekeleza maelezo ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kututaka kutumia vizuri fursa ya biashara ya hewa ukaa, kwa kutunza mazingira na misitu yetu ili tija ionekane, tunamshkuru kwa maono yake asali ya hewa ukaaa tumeanza kuionja Kilosa” alifafanua Shaka

Amebainisha kuwa kwa mara ya kwanza Wilaya hiyo imeweza kuzalisha tani 545,433 ambazo ziitaingizia mapato ya sh. bilioni 1,171,478,458 ambapo ni gawio kulingana na mchanganuo wa mapato ambayo yamepatikana katika misitu ya vijiji huku kijiji Cha Malolo, msiba na Mhenda vikifanya vizuri zaidi katika kipindi cha 2023 mpaka Feb 2024.

“Tunauwezo wa kupunguza umaskini kupitia bishara hii ya hewa ukaa, lakini pia tunauwezo wa kuifanya halmashauri hii kuwa ya mfano kupitia mapato haya ya biashara ya hewa ukaaa kadri uwekezaji huu utakavyozidi kutanuka” ameeleza.

Hata hivyo Shaka amepiga marufuku Uvunaji na usafishaji mashamba holela huku akisitiza kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria kwa wote wataobainika kufanya hivyo bila ya kuwa na vibali halali

“Vijiji kwa kushirikiana na Halmashauri ya nendeni mkaboreshe sheria ndogo ndogo za usimamizi wa misitu ili kuweka adhabu kali zaidi kwa mtu yoyote atakayehusika na ukataji wa miti hovyo na uharibifu wa misitu” alisema Shaka


Related Posts